Kitaifa

Serikali yavuna Sh15 bilioni ushuru wa korosho Kusini

Mbeya. Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), imesema Serikali imepokea zaidi ya Sh15 bilioni ikiwa ni mapato yatokananyo na ushuru wa zao korosho kwa mikoa ya Lindi na Mtwara.

Hii ni baada ya vyama vya ushirika kulipwa Sh2.9 trilioni kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo.

Malipo hayo yalihusisha vyama vya ushirika 7,391 vyenye wanachama milioni 12 huku tani 1.092 milioni za mazao ya kimkakati (tumbaku, pamba, korosho, kahawa, mkonge, chai, Soya, Choroko na dengu) yaliuzwa na kulipwa kwa wakulima kupitia vyama hivyo.

Takwimu hizo zimetolewa leo Jumanne, Januari 9, 2024 na Naibu Mrajisi, Divisheni ya Usimamizi na Udhibiti wa Vyama vya Ushirika, Colllins Nyakunga wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya usimamizi wa vyama vya ushirika kwa maofisa ushirika nchini yanayofanyika Kanda ya Mbeya na kuhusisha mikoa mitano.

“Kati ya mauzo hayo pia Sh1.041 bilioni zimetokana na ushuru wa zao kahawa kwa Mkoa wa Kagera pekee, mafanikio hayo yanaifanya Serikali kuweka mikakati ya kuwezesha vyama vya ushirika,” amesema.

Amesema ili kufikia malengo wamehamasisha uanzishwaji wa viwanda vidogo vya kati huku kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita jumla ya viwanda vya kati 279 vilianzishwa kupitia sekta ya ushirika kwa lengo la kuongeza thamani ya mazao.

“Pia tume inahamasisha wanachama wa vyama vya ushirika kujiunga na mifuko ya bima za afya na mazao sambamba na kupata pembejeo bora za kilimo ili kufikia malengo ya Serikali katika kwenye kilimo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Msaidizi (sehemu ya masoko na mazao) kutoka Wizara ya Kilimo, Dk Abel Mtembeji amesema ili kufikia mipango ya Serikali ya ajenda ya 10/30 ni lazima kuwepo kwa mipango mikakati ikiwa ni pamoja na kuanzisha benki ya wana ushirika.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema: “Serikali kupitia Wizara ya fedha imekuwa ikiwezesha TCDC ili kutekeleza majukumu yake ya kusimamia sekta ya ushirika kwa lengo la vyama vipate kusimamia.”

Amesema vyama vya ushirika vimekuwa na changamoto nyingi ikiwepo ukosefu wa watumishi wenye sifa na hivyo kuchangia wizi, ubadhirifu na kujiendesha kwa hasara, pamoja na uwekezaji mdogo usio na tija na kuwataka kutumia mafunzo hayo kuondokana na changamoto hizo.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi