Kitaifa
Serikali yasitisha bei mpya vitita vya NHIF, kuunda kamati
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesitisha bei mpya za kitita cha matibabu zilizowekwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) huku ikitangaza kuunda kamati huru itakayofanya mapitio ya maboresho yaliyofanyika.
Bei hizo mpya ambazo zilipangwa kutekelezwa kuanzia Januari Mosi, 2024 zimesitishwa hadi itakapotangazwa tena.
Kusitishwa huko kunafuatia tishio la hospitali binafsi la kusitisha huduma za matibabu kwa wenye kadi za NHIF na hivyo kulazimu mazungumzo ya mezani na Waziri mwenye dhamana ya afya, Ummy Mwalimu.
Desemba 18, 2023 NHIF ilifanya mapitio ya kitita cha mafao kwa mwaka 2023, ambayo kwa mujibu wao, yalilenga kuongeza au kupunguza gharama katika baadhi ya huduma ili kuendana na bei halisi ya soko.
Kufuatia mabadiliko hayo, iliibuka sintofahamu baada ya madaktari bobezi kuyalalamikia wakidai kutoshirikishwa huku wamiliki wa hospitali binafsi wakidai kwamba hawakuafikiana.
Uamuzi huo umefikiwa leo Alhamisi, Januari 4, 2024 baada ya mkutano wa ndani kati ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na wawakilishi wa wamiliki wa hospitali binafsi wakiwamo Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC), Chama cha Wamiliki wa Vituo vya Aafya Binafsi Tanzania (APHFTA) na Bakwata.
Katika kikao hicho, Waziri Ummy amewataka wawakikishi hao kujadiliana na kutoa maoni yao kwa uwazi na kwa kutanguliza maslahi mapana ya Watanzania ili kuwezesha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wananchi bila kikwazo cha fedha.
Taarifa iliyotolewa kwa wanachama wa CSSC, Bakwata na Aphfta kuhusu bei mpya za NHIF imeeleza baada majadiliano ya kina, Waziri Ummy ametoa maelekezo kuwa kitita kipya cha matibabu cha NHIF kisitumike hadi hapo Wizara itakapo toa maelekezo baada ya mazungumzo ya kina baina ya pande hizo mbili.
Waziri Ummy ataunda kamati huru itakayofanya mapitio ya bei za kitita cha huduma za afya cha NHIF.
“Tunapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru watoa huduma wote walio wanachama wa Aphfta, CSSC na Bakwata kwa utulivu mlio uonyesha katika kipindi hiki cha sintofahamu.
“Tunaomba muendelee kuwa wavumilivu na watulivu wakati ufumbuzi wa kudumu ukifanyiwa kazi na viongozi wa Wizara wakishirikiana na sisi viongozi wa sekta binafsi,” imeeleza taarifa hiyo.
Malalamiko makubwa ya watoa huduma ilikuwa ni kupungua kwa ada ya usajili na ushauri wa daktari katika kitita kipya.
Katika mabadiliko ya ada ya usajili na ushauri wa daktari, viwango ambavyo vilipunguzwa ni kwa mgonjwa kumuona daktari Hospitali ya Taifa kufikia Sh25,000 kutoka Sh35,000 kwa daktari bingwa mbobezi na Sh20,000 kutoka Sh 25,000 kwa daktari bingwa.
Mabadiliko mengine ni kwenye Hospitali ya Rufaa ya kanda na kumuona daktari bingwa mbobezi ni Sh25,000 kutoka Sh35,000 na kumuona daktari bingwa ni Sh20,000 kutoka Sh25,000.
Hospitali ya mkoa, kumuona daktari bingwa mbobezi ni Sh25,000 kutoka Sh Sh15,000 na kwa daktari bingwa ni Sh20,000 kutoka Sh15,000.
Pia, kwa kliniki bobezi, kumuona daktari bingwa mbobezi na daktari bingwa ni Sh10,000 kutoka Sh15,000 na kwenye kliniki nako kumuona daktari bingwa na bingwa mbobezi ni Sh10,000.
Kwa mujibu wa mfuko huo, maboresho hayo pia yalienda kupunguza gharama kwa wanachama waliolazimika kununua baadhi ya dawa ambazo hazikujumuishwa kwenye mfuko wa mafao ambapo jumla ya dawa 124 kwenye orodha ya Orodha ya Dawa Muhimu ya Taifa (NEMLIT) zimeongezwa.
Kwenye huduma za dawa, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga alisema mwaka 2021 kulitolewa muongozo na NHIF kuchelewa kufanyia maboresho hivyo kujikuta ndani ya muongozo kuna dawa ambazo hazipo kwenye kitita.
“Dawa 124 tumezijumuisha kwenye kitita cha mafao ili zikatoe ahueni na kuongeza ukubwa wa kitita katika utoaji wa huduma, tumezihuisha bidhaa za dawa 374 ambazo zimeongezewa bei kwa wastani wa asilimi 10 hadi 20,” amesema katika mkutano wake na vyombo vya habari Desemba 18, 2023.
Konga amesema kuna maeneo dawa walikuwa wakilipa kwa gharama ndogo lakini sasa watalipa kulingana na bei ya soko.
Vilevile, ada ya kumuona daktari bingwa mbobezi katika rufaa za Taifa zitakuwa sawa rufaa za mikoa lengo kupunguza msongamano katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuhakisha uwekezaji ulifanywa na serikali kwenye sekta ya afya unakuwa na tija.
Baada ya taarifa hiyo, wadau mbalimbali walilalamika kutoshirikishwa lakini NHIF ilisisitiza wadau wote walishirikishwa na Januari hii utaratibu huo ungeanza rasmi na dirisha la wadau hao kuendelea kutoa maoni lipo wazi.
Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, Konga amesema wadau hao walishirikishwa na walitoa maoni ambayo yalifanyiwa kazi na mengine yatachukua muda kuendelea kufanyiwa kazi.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dk John Jingu, Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Tumaini Nagu, Mwenyekiti wa APHFTA Dk Egina Makwabe, Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF Juma Muhimbi, Mfamasia Mkuu wa Serikali Daud Msasi na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Bernard Konga.
Pia, kikao hicho kimehudhuriwa na wawakilishi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) pamoja na wawakilishi kutoka Bohari ya Dawa (MSD).