Kimataifa
Kenya yapindua meza biashara na Tanzania
Unaweza kusema Kenya imepindua meza kwa kurejea kwenye nafasi yake katika biashara baina yake na Tanzania, baada ya kuipoteza mwaka uliopita.
Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliyochapishwa Desemba 31, 2023 inaonyesha, Kenya iliuza bidhaa zake nchini kwa asilimia 31 zaidi ya kiwango ambacho Tanzania iliuza kwao, ikiwa ni tofauti na mwaka uliotangulia ambapo Tanzania iliuza katika nchi hiyo kwa asilimia 10 zaidi.
Hiyo ikiwa na maana kuwa, bidhaa za Sh1.06 trilioni ziliingizwa nchini kutoka Kenya ikilinganishwa na bidhaa za zaidi ya Sh724.32 bilioni za Tanzania zilizouzwa nchini kwao mwaka 2022/2023.
Hiyo ni tofauti na mwaka 2021/2022 ambapo Tanzania iliuza zaidi nchini Kenya bidhaa za zaidi ya Sh993.42 bilioni, huku ikinunua bidhaa za Sh892.82 bilioni.
“Huenda hali iliyotokea sasa hivi kati ya biashara ya Kenya na Tanzania ilitokana na sitofahamu iliyokuwa ikiendelea nchini huko,” alisema Mtaalamu wa masuala ya biashara na uchumi, Oscar Mkude.
Anasema hali ya kisiasa iliyokuwapo nchini humo kwa kipindi cha nyuma, watu kupinga kupanda kwa baadhi ya bidhaa, ikiwemo za chakula hali iliyozua maandamano huenda ikawa chanzo cha wafanyabiashara wa Tanzania kushindwa kupeleka bidhaa zao nchini humo.
Licha ya hali hiyo, alisema kama nchi inatakiwa kuangalia zaidi namna ya ufanyaji wa biashara yake na nchi nyingine, kwani imekuwa ikinunua zaidi kuliko inavyouza.
Katika kununua huko pia alisema ikiwa vitu vinavyonunuliwa ni vya thamani sana kama mitambo, magari na nchi ikiuza bidhaa ndogondogo kama kahawa, korosho mara zote inafanya urari wa biashara, unapoangaliwa unakosa usawa.
Lakini ili kuondokana na suala hilo anasema ni vyema Tanzania ikaanza kuuza bidhaa zilizoongezewa thamani ambazo zitaingia sokoni moja kwa moja pindi zinaposafirishwa badala ya kufikia katika viwanda vya nchi nyingine kuongezwa thamani na kurudishwa nchini.
“Tutoke kuuza vitu ghafi, tunakosa ajira, thamani ya malighafi ni tofauti na bidhaa”.
Kwa muda mrefu Tanzania na Kenya zimekuwa nchi zinazoshirikiana kibiashara kwa miaka mingi, japo mara kadhaa kumekuwa kukiibuka hali inayotatiza ushirikiano huo.
Ili kumaliza sitofahamu zilizojitokeza, hivi karibuni marais wa nchi hizo, Samia Suluhu Hassan na William Ruto walilazimika kuwa na vikao vya mara kwa mara vilivyolenga kuondoa vikwazo vya ufanyaji biashara kati ya nchi hizo.
Kupitia mikutano hiyo, vikwazo visivyokuwa vya kikodi 55 kati ya 64 viliondolewa kwa mujibu wa Rais Samia, huku akieleza kuwa mazungumzo yalikuwa yakiendelea, huku akikiri kuimarika kwa biashara kati ya nchi hizo mbili.
“Vivyo hivyo tumefanya na nchi nyingi na shughuli zinakwenda. Na nyie katika shughuli zenu za kisheria za kuvuka mipaka, kajipangeni ili biashara yenu iende vizuri mtuletee nini mnaweza kufanya, nini nchi zenu zinaweza kufanya, ili biashara yenu ivuke mipaka kwa malengo ya kusaidia jamii,” alisema Samia.
Tanzania huuza zaidi nafaka, madini na bidhaa za mbao nchini Kenya, huku Taifa hilo la kwanza kiuchumi likiiuzia zaidi Tanzania bidhaa viwandani kama sabuni na nyingine.
Kuhusu kukuza urari wa biashara, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu Huria (OUT), Dk Lawi Yohana anasema ili kuepuka kuwa soko la bidhaa za nchi nyingine, ni vyema Tanzania ikaongeza uzalishaji wa bidhaa za viwandani ili ziweze kuuzwa si Kenya pekee, bali pia nchi nyingine za karibu.
Kuendelea kuuza bidhaa ghafi ni kutengeneza ajira katika nchi jirani na kuwapatia soko la bidhaa zao.
“Serikali ifanye mikakati ya makusudi ya kuimarisha sekta ya viwanda ili tuweze kukidhi soko la Afrika Mashariki na Kati ambalo ni kubwa.”
Anasema hilo linaweza kufanyika vizuri zaidi ikiwa sekta binafsi itapewa kipaumbele, huku akitaka nguvu zaidi zitumike kuvutia wawekezaji.
Profesa Aurelia Kamuzora kutoka Chuo Kikuu Mzumbe anasema Tanzania imekuwa ikiingiza bidhaa za kilimo kutoka Kenya ambazo wameziongezea thamani.
“Sisi tunauza sana bidhaa za mazao kama viazi, Kenya wakinunua wanaenda kuongeza thamani wanatengeneza pingles wanatuletea tena sisi na zinauzwa kwa bei juu, ipo haja ya kuongeza thamani ya vitu vyetu,” anasema Profesa Kamuzora.
Anaongeza kuwa Tanzania tayari ina malighafi za kutosha kama kahawa, pamba, tumbaku ambazo zote zinaweza kutumika kutengeneza bidhaa tofauti, lakini kutokana na kukosekana kwa viwanda nchi imekuwa ikiuza bidhaa ghafi na kuletewa bidhaa zilizoongezwa thamani kama nguo ambazo huuzwa bei juu.
“Hivyo ni vyema tuwekeze katika viwanda, tuongeze thamani, ndiyo njia pekee ya kufanya biashara yetu kwa faida.
Biashara na nchi nyingine EA
Ukiachilia mbali kwa Taifa la Kenya, Tanzania ilifanya vizuri katika uuzaji wa bidhaa zake katika nchi nyingine za Afrika ya Mashariki, ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) ambayo imejiunga hivi karibuni katika jumuiya hii.
Kwa sasa DRC ndiyo inaongoza kuwa soko kubwa la bidhaa za Tanzania ndani ya ukanda huo ambapo ripoti hii inaonyesha kuwa, Tanzania iliuza bidhaa za zaidi ya Sh769.6 bilioni, huku ikinunua bidhaa za zaidi ya Sh6.79 bilioni.
DRC imeipiku Kenya ambayo awali ilikuwa soko kuu la bidhaa za Tanzania kwa miaka ya nyuma ndani ya ukanda huo.
DRC ilikubaliwa rasmi kujiunga katika jumuiya hii Machi 2022, ikiwa ni mwanachama wa saba huku kujiunga kwake kukitajwa kuwa na faida lukuki, ikiwemo kupanua wigo wa kibiashara kutokana na idadi ya watu waliopo nchini humo.
Nchi nyingine za Afrika ya Mashariki ni Burundi ambapo Tanzania ilifanya biashara ya zaidi ya Sh518.09 bilioni, huku ikinunua bidhaa za zaidi ya Sh7.54 bilioni pekee.
Nchini Uganda, Tanzania iliuza bidhaa za Sh719.29 bilioni na kununua bidhaa za takribani Sh286.71 bilioni.
Kwa upande wa Rwanda, Tanzania ilinunua kutoka kwao bidhaa za Sh4.275 bilioni, huku ikiuza bidhaa za zaidi ya Sh530.66 bilioni.
Hata hivyo, biashara kwa ujumla katika kipindi cha mwaka 2022/2023 Tanzania iliuza katika nchi za Afrika ya Mashariki bidhaa zilizo na thamani ya zaidi ya Sh3.26 trilioni, huku ikinunua bidhaa za Sh1.37 trilioni.
Wakati Tanzania ikifanya vizuri katika uuzaji wa bidhaa zake, Juni mwaka jana, nchi wanachama wa EAC zilikubaliana kuondoa vikwazo kumi vya kibiashara na visivyo vya kiforodha (NTBs), huku vikwazo nane vikiendelea kushughulikiwa.
Pia vikwazo vingine vipya vinne vya ufanyaji biashara katika nchi hizo ziliwasilishwa ili kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara baina ya nchi hizo.
Makubaliano ya uondoshaji vikwazo hivyo yalifanyika katika mkutano wa 42 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji la Jumuiya ya Afrika Mashariki (SCTIFI), uliofanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo, Jijini Arusha.
Mbali na kuondoa vikwazo, pia nchi hizo zilikubaliana kutoza Sh25,120 kwa kilomita 100 kwa ajili ya matumizi ya barabara kwa magari ya mizigo kutoka nchi moja kwenda nyingine katika Jumuiya hiyo badala ya kila nchi kuwa na viwango vyake vya tozo.
Lakini pia baraza hilo la mawaziri la kisekta, limekubaliana kuondoa gharama ya viza kwa watu wanaotaka kusafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine kwa shughuli mbalimbali, zikiwemo za kibiashara, ili kukuza mahusiano miongoni mwa wakazi wa Jumuiya hiyo pamoja na kuchochea ukuaji wa biashara na uchumi wa nchi husika.