Connect with us

Kitaifa

Joto pwani lavunja rekodi, wataalamu waeleza athari kiafya

Kwa mujibu wa TMA, ongezeko hilo si kwa Tanzania pekee, kwa kuwa taarifa zinaonyesha wastani wa ongezeko la joto la dunia mwaka jana ulifikia nyuzi joto 1.40 za sentigredi na kuufanya kuwa mwaka wenye joto zaidi katika historia.

Hali hiyo inaelezwa imechangiwa na uwepo wa El-Nino (mfumo wa hali ya hewa unaosababishwa na ongezeko la joto la bahari katika eneo la kati la kitropiki kwenye Bahari ya Pasifiki) na mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi Mtendaji wa TMA, Dk Ladislaus Chang’a alisema kiwango hicho cha joto kimepatikana baada ya kukokotoa wastani wa nyuzi joto katika kipindi cha miezi 12 na kuthibitika ongezeko la nyuzi joto 1.0 ambalo halijawahi kurekodiwa nchini.

“Unapozungumzia wastani ni mjumuisho wa muda mrefu, baada ya kurekodi kiwango cha joto cha mwaka mzima ndipo tulipopata ongezeko la nyuzi joto 1.0, kiwango ambacho hakijawahi kurekodiwa, ndiyo maana tunasema mwaka 2023 umevunja rekodi,” alisema Dk Chang’a.

Alisema kwa miaka ya nyuma walikuwa wakirekodi chini ya hapo, akitoa mfano mwaka 2022 ilikuwa nyuzi joto 0.5. Vingine vilivyorekodiwa kwa miaka mingine ni 0.3, 0.6 na 0.7.

Kwa upande wa viwango vya dunia, alisema wastani wa nyuzi joto 1.2 sentigredi kilirekodiwa mwaka 2022 na mwaka 2021 ilikuwa 1.1.

Kiwango cha juu cha joto kimeripotiwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro na Dodoma, pia Zanzibar.

Taarifa ya TMA inaeleza ongezeko la joto ni matokeo ya kusogea kwa jua la utosi na upungufu wa mvua unaojitokeza katika maeneo mbalimbali.

Kwa mujibu wa TMA, kwa kawaida vipindi vya jua la utosi nchini hufikia kilele mwishoni mwa Novemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini na hali hiyo hujirudia Februari wakati jua la utosi likielekea kaskazini.

“Katika kipindi cha Desemba, 2023 kumekuwa na ongezeko la joto kwa baadhi ya maeneo nchini, hasa nyakati ambazo kumekuwa na vipindi vichache vya mvua. Hadi kufikia Desemba 29, 2023 kituo cha Morogoro kiliripoti kiwango cha juu zaidi cha nyuzi joto 33.9 sentigredi, ikiwa ni ongezeko la nyuzi joto 1.3 ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa Desemba,” inaeleza taarifa ya TMA.

Kituo cha Tanga kiliripoti nyuzi joto 33.6 °C Desemba mosi, 2023 ikiwa ni ongezeko la nyuzi joto 1.5, Dodoma iliripotiwa nyuzi joto 33.5 °C Desemba 19, mwaka jana (ongezeko la nyuzi joto 2.9), Dar es Salaam nyuzi joto 33.2 °C ziliripotiwa Desemba 2 (ongezeko la nyuzi joto 1.2) na Zanzibar nyuzi joto 33.4 °C ziliripotiwa Desemba 2, 2023 (ongezeko la nyuzi joto 1.6).

Ushauri wa wataalamu

Akizungumzia hali hiyo, daktari wa binadamu, Chris Cyrilo alisema kiwango cha joto kilichopo jijini Dar es Salaam bado si kikubwa kiasi cha kuleta maafa kama ambavyo imekuwa ikitokea katika nchi nyingine, ikitoa mfano wa India ambayo hufikia nyuzi joto 40 za sentigredi.

Alisema ili kujiweka salama kwa kuwa mwili hupoteza maji mengi kupitia jasho, unywaji wa maji ni muhimu.

Mengine anayoshauri ni kuacha kufanya shughuli kwenye joto na jua kali, pia kuepuka kutumia mafuta mazito ya kupaka mwilini.

“Ni kweli joto lipo lakini si la kuleta maafa, kinachotakiwa ni kunywa maji mengi kwa kuwa inapotokea hali hii mwili hupoteza kiasi kikubwa cha maji na upo uwezekano wa enzymes (vimeng’enya) na homoni kushindwa kufanya kazi pale joto linapozidi,” alisema.

Dk Cyrilo alisema, “watoto wanaweza kuathiriwa zaidi na joto kwa kuwa ngozi zao ni laini, hivyo ni rahisi kupata vipele, ngozi kuwasha au matatizo mengine ya ngozi. Ili kujiweka salama ikiwezekana mavazi mepesi ndiyo yavaliwe zaidi wakati wa hali hii, kinyume cha hapo upo uwezekano wa kupata maradhi ya ngozi.”

Kwa upande wake, Dk Jacob Ekusa alisema joto kali husababisha mwili kupoteza maji na madini chumvi.

Alisema endapo mwili utaendelea kupandisha joto, mtu anaweza kupata madhara kadhaa, yakiwamo mwili kuelemewa na joto, misuli kukakamaa na kiharusi kinachosababishwa na joto kali.

Alisema wanaoathirika zaidi na joto ni wazee, watoto, wanene kupita kiasi na watu wenye magonjwa ya kudumu kama vile ya upumuaji na moyo.

“Joto kali huweza kusababisha tatizo la misuli kukakamaa. Hili hutokana na mwili kupoteza maji mengi na madini chumvi muhimu kama sodium. Inapotokea hali hii, kunywa maji mengi, hasa yenye chumvi kiasi. Hili linaweza kusaidia kurudisha mwili katika hali ya kawaida,” alisema Dk Ekusa.

Naye Dk Sadick Sizya, alisema joto linapozidi watu hukimbilia kutumia viyoyozi na feni, wengi wakishindwa kuvitumia kwa usahihi na matokeo yake huishia kupata matatizo mengine.

Akizungumzia matumizi ya feni, Dk Sizya alisema kifaa hicho kazi yake ni kuzungusha hewa iliyopo, hivyo kuitumia bila kuruhusu hewa nyingine kuingia ndani inaweza kumsababishia madhara mtumiaji. Anashauri ni muhimu kufungua madirisha na milango kuruhusu hewa kupita.

“Feni kazi yake kuzungusha hewa iliyopo, kama nyumba ina vumbi au uchafu utakuwa unazunguka. Kwa kufunga madirisha na milango, ina maana hewa haitoki inaishia kuzunguka ndani, mwisho mtu anaweza kupata tatizo mfano mwili kuchoka, kichwa kuuma, mafua na kupata kizunguzungu,” alisema Dk Sizya.

Alisema joto la mazingira linapobadilika linaweza kuathiri joto la mwili, na hilo likitokea linaweza kuathiri utendaji kazi wa homoni. “Homoni ni kemikali zinazoongoza mwili, hivyo kukiwa na changamoto ya joto haziwezi kufanya kazi vizuri na matokeo yake utendaji kazi wa mwili unaathirika.

Ukiathirika mwili hauwezi kufanya kazi vizuri, ina maana mapigo ya moyo yanaweza kuathirika, ukapata changamoto ya ufanyaji kazi wa figo au hata mtu kuanguka ghafla kwa sababu ya kiharusi cha joto.”

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi