Kitaifa
Othman ataka maoni ya wananchi yasikilizwe, miswada ya uchaguzi
Othman aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar (AG) ametoa nasaha hizo leo Jumatano, Januari 3, 2024, jijini hapa katika ufunguzi wa mkutano maalumu wa Baraza la Vyama vya Siasa unaoshirikisha wadau mbalimbali wa demokrasia.
Lengo la mkutano huo ni kujadili na kutoa maoni ya miswada ya sheria za uchaguzi na muswada wa sheria za vyama vya siasa iliyowasilishwa bungeni Novemba 10, 2023. Tayari Bunge limewaalika wadau mbalimbali kuwasilisha maoni na mapendelezo mbele ya kamati zake.
Katika hotuba yake, Othman amesema inawezekana baadhi wanaweza kuuchukulia utamaduni unaoendelea kujengeka wa kuwashirikisha wadau mbalimbali katika masuala yenye masilahi mapana ya kitaifa kama ni jambo tu la kawaida.
Amesema utaratibu huo wa kukutana na kuzungumza, unatoa fursa kwa Watanzania kushirikishwa kupitia taasisi mbalimbali zinazowawakilisha.
“Hivyo sauti zao zimesikilizwa kupitia viongozi wao. Ninawasihi sana na kwa heshima kubwa, mkutano huu uache alama ya utamaduni mwema wa majadiliano.
“Uwe mkutano wa utajiri wa mawazo ya washiriki na sio mkutano wa mapambio na kutimiza tu utaratibu tunaoanza kuuzoea wa kusema wadau walishirikishwa japokuwa kiuhalisia hawakusikilizwa,” amesema.
Amesema kuna maoni mbalimbali amekuwa akiyasikia kuhusu miswada hiyo. Othaman ametolea mfano, “Nimesikia maoni ya watu wengi kuhusu usimamizi wa uchaguzi kuepuka wasimamizi wenye rekodi za kisiasa.
“Hili linaweza kuepukwa kwa kuweka vifungu bayana katika sheria vinavyokataza mtu yeyote ambaye ana rekodi ya kushiriki siasa waziwazi kwa kipindi fulani, kutofaa kuwa msimamizi wa uchaguzi.
“Vilevile kwenye jopo la uteuzi wa Tume ya Uchaguzi, nimesikia maoni ya viongozi wa kisiasa kuwa na uwakilishi, hili ni jambo linalowezekana kwa kujadiliana namna bora ya kupata jopo la uteuzi bila ya viongozi wa kisiasa kutilia shaka. Mwisho, nimesikia kilio cha muda mrefu cha vyama vya siasa kuhusu kanuni ya kukokotoa ruzuku kwa vyama,” amesema.
Othman ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa chama cha ACT- Wazalendo, Zanzibar akifafanua suala la ruzuku amesema hilo linawezekana bila kuathiri kiwango cha bajeti ya ruzuku kwa kutekeleza mapendekezo ya Kikosi Kazi, kwamba asilimia 10 ya bajeti ya ruzuku igawiwe kwa vyama vyote kwa usawa.
Othman amesema kuna kanuni za majadiliano ambazo washiriki wa mkutano huo wanapaswa kuzizingatia.
“Ni vyema tukumbuke miswada hii sio tu ya kurekebisha sheria bali ni sehemu ya kutekeleza maono mapana ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo wadau wengi wanayaunga mkono. Maono hayo ni ya ujenzi wa Taifa yaliyojengwa katika 4R ambazo ni maridhiano, mageuzi, kujenga upya na ustahimilivu.
Amesema katika R hizo 4, kwa maoni yake R mama ni ile ya mageuzi. Endapo tutatekeleza R hii kwa dhati na kwa weledi, utekelezaji wa R nyingine tatu utakuwa mwepesi.
Othman amesema miongoni mwa mageuzi muhimu ambayo nchi inahitaji bila kuchelewa ni kujenga misingi ya uwajibikani katika ngazi zote.
“Moja kati ya maradhi yanayolitafuna Taifa letu ni kulegalega kwa uwajibikaji katika ngazi na daraja zote,” amesema Othman.
Amesema bila ya shaka, kama tunataka kufanya mageuzi katika suala la uwajibikaji hatuna budi kufanya mageuzi katika mfumo wetu wa uchaguzi.
“Mageuzi ya kweli, mageuzi ya dhati yatakayozaa kilicho bora kwa Taifa letu na sio kilicho bora kwa wachache wanaofaidika na kukosekana kwa uwajibikaji katika Taifa. Uchaguzi ndio unaozaa uongozi wa kitaifa na utendaji wa taasisi zote,” amesema.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama amewaambia wajumbe wa mkutano huo wa demokrasia ya vyama vingi kuwa, maoni yao watakayatoa watayachukua kama yalivyo bila kuchakachuliwa.
“Maoni yatakayotolewa hapa yanawekwa sawa na kuwasilishwa mahali panapohusika bila kuchakachuliwa hili litakuwa ni jambo jema, hata Serikali ingependa kupata nafasi ya kujifunza kwa wadau, kusikia wanafikiria nini katika kuimarisha demokrasia ndani ya Taifa letu.
“Serikali inaweza ikapata nafasi nzuri kwa sababu elimu haina mwisho kupitia maoni ya wadau na ushauri utakaotolewa katika mkutano huu, niwahakikishie wajumbe tutashiriki mkutano huu kwa siku zote mbili ili kuyachukua yote,” amesema Mhagama.
Msimamo huo umetolewa pia na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungia, ambaye amewaondoa hofu wadau kuwa maoni yao hayatachakachuliwa bali yatachukuliwa yote tena kwa kuandikwa.