Connect with us

Kitaifa

MAT yakubali kukaa meza moja na NHIF

Dar es Salaam. Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Deus Ndilanha amesema wamekubali kukaa meza moja na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Januari 5 2024,  ili kujadili ada ya usajili na ushauri wa daktari katika kitita kipya kwa manufaa ya pande zote.

Desemba 18, NHIF ilifanya mapitio ya kitita cha mafao kwa mwaka 2023, ambayo kwa mujibu wao, yalilenga kuongeza au kupunguza gharama katika baadhi ya huduma ili kuendana na bei halisi ya soko.

Kufuatia mabadiliko hayo, iliibuka sintofahamu baada ya madaktari bobezi kuyalalamikia wakidai kutoshirikishwa, huku Wamiliki wa Hospitali binafsi (Aphfta), wakidai kutoafikiana.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi Desemba mwaka jana, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga alisema bado milango ipo wazi kwa wadau kutoa maoni kwa lengo la kuboresha utoaji huduma.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Januari 3, 2024 Ndilanha amesema suala lao limesikilizwa na wanatarajia kukutana na NHIF Ijumaa, huku akisisitiza kuwa kilichopo si malalamiko bali wanataka kufanya majadiliano ya pamoja.

“Tunataka kuona namna ambavyo haya maboresho yafanyike lakini  yasiumize upande wowote. Tunataka anayetoa huduma asiumie, anayepokea huduma asiumie lakini na mfuko wetu usiumie.

 “Kwa hiyo ni majadiliano ya kuona namna nzuri ambayo tunaweza tukalifanyia kazi hili jambo likawa na sura nzuri,” amesema Dk Ndilanha.

Katika mabadiliko ya ada ya usajili  na ushauri wa daktari viwango vilivyopunguzwa  ni kwa mgonjwa kumuona daktari Hospitali za Taifa kufikia Sh25,000 kutoka Sh35,000 kwa daktari bingwa mbobezi na Sh20,000 kutoka Sh25,000 kwa daktari bingwa.

Mabadiliko mengine ni kwenye hospitali za rufaa ya kanda ambapo kumuona daktari bingwa mbobezi ni Sh25,000 kutoka Sh35,000  na kumuona daktari bingwa ni Sh20,000 kutoka Sh25,000.

Hospitali za mkoa, kumuona daktari bingwa mbobezi ni Sh25,000 kutoka Sh Sh15,000 na kwa daktari bingwa ni Sh20,000 kutoka Sh15,000.

Pia kwa kliniki bobezi, kumuona daktari bingwa mbobezi na daktari bingwa ni Sh10,000 kutoka Sh15,000 na kwenye kliniki kumuona daktari bingwa na bingwa mbobezi  ni Sh10,000.

Marekebisho hayo kwa mujibu wa NHIF yamelenga kuongeza wigo wa utoaji huduma za kibingwa kuanzia ngazi ya rufaa ya kanda hadi Taifa.

Awali Dk Ndilanha alisema hawajakubaliana na maboresho hayo na kwamba licha ya baadhi ya wataalamu kushirikishwa, MAT hawakushirikishwa.

Alisema haina tija kwa tasnia ya udaktari ikiwa wataalamu wanaosoma udaktari bingwa na ubobezi kwa miaka mingi wanakandamizwa.

“Badala ya kushusha kiwango cha kumuona daktari wangeongeza, ada hii huwa haishuki, wamewavunja moyo sana na tunaona italeta taharuki kidogo. Huwezi kusema ada ya mwaka 2016 ilikuwa kubwa kidogo na 2023 ukapunguza,” alisema Dk Deus.

Alisema suala hilo haliendani na kujitolea kwa wataalamu na hali halisi ya maisha ya sasa, kwani ada hiyo ilitakiwa kuongezeka.

Mkutano huo unatarajiwa kufanywa kesho Ijumaa, Januari 4, 2024  ambapo Waziri wa Afya Ummy Mwalimu anatarajiwa kukutana na wawakilishi wa wamiliki wa vituo vya kutolea huduma jijini Dar es Salaam.

Desemba mwaka jana, Aphfta walitoa taarifa kwamba wangesitisha huduma ifikapo Januari Mosi kufuatia kutoafikiana na NHIF.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi