Kitaifa
TRA yaumaliza mwaka 2023 kwa kishindo
Dar es Saalam. Makusanyo ya kodi katika kipindi cha mwezi Desemba yamevuka lengo kwa asilimia 102.99 na kuweka rekodi mpya ya kiwango cha juu cha ukusanyaji tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo na kusainiwa na Kamishna Mkuu, Alphayo Kidata kiasi cha Sh3.05 trilioni kimekusanywa Desemba wakati lengo lilikuwa kukusanya Sh2.9 trilioni.
Makusanyo hayo ni ongezeko la asilimia 9.2 ukilinganisha na kiasi cha Sh 2.79 trilioni kilichokusanywa katika mwezi kama huu katika mwaka wa fedha wa 2022/23.
Katika taarifa hiyo pia imeelezwa kuwa TRA katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/24 (Julai- Disemba), imefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh13.92 trilioni ambayo ni sawa na ufanisi wa asilimia 97.98 ya lengo la kukusanya Sh14.21 trilioni.
Makusanyo hayo ya nusu mwaka ni ongezeko la asilimia 11.5 ikilinganishwa na makusanyo ya Sh12.49 trilioni yaliyofikiwa katika kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha uliopita, 2022/23.
Kamishna Kidata amesema mafanikio hayo yamechagizwa na juhudi za mamlaka katika kutekeleza kwa vitendo maelekezo na miongozo mbalimbali inayotolewa.
Aidha, TRA imeendelea na utekelezaji wa mpango mkakati wake wa sita (CP6) wenye athari chanya katika ukusanyaji wa mapato nchini ambapo miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na maboresho katika muundo wa mamlaka hiyo.
Maboresho hayo yanahusisha uanzishwaji wa divisheni mpya za walipakodi wa kati na walipakodi wadogo, ili kutoa huduma bora na stahiki kwa makundi tofauti ya walipakodi kwa kuzingatia tofauti ya mahitaji yao.
Eneo lingine ni kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini, hali iliyochangia kuongezeka kwa uwekezaji, uzalishaji wa viwandani na uingizaji wa mizigo nchini.