Connect with us

Kitaifa

Rais Samia: 2023 mwaka wa mageuzi, 2024 matokeo

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameutafsiri 2023 kuwa mwaka wa mageuzi, huku akisema 2024 utakuwa wa utekelezaji na matokeo zaidi.

Kauli hiyo ya Rais Samia inatokana na kile alichoeleza katika mwaka 2023, mambo mengi yamefanyika ikiwemo uboreshaji wa utendaji katika taasisi za umma na kinachotarajiwa ni matokeo.

Mkuu huyo wa nchi ameyasema hayo jijini leo, Jumapili Desemba 31, 2023 alipotoa salamu za mwaka mpya 2024 kwa Watanzania.

Amesema katika mwaka 2023 Serikali imeongeza kasi ya utekezaji wa falsafa yake ya R4 ikiwemo ya mageuzi iliyohusisha kuundwa kwa Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu, kutenganisha wizara mbalimbali na kurejesha baadhi ya taasisi ikiwemo Tume ya Mipango.

Ameeleza mageuzi mengine yamefanyika kupitia utekelezwaji wa falsafa hiyo yakiwemo maazimio yaliyotokana na majadiliano na wadau wa demokrasia nchini.

“Ili kutekeleza maazimio hayo, tayari tumewasilisha bungeni miswada mitatu kuhusu Sheria ya Tume ya Uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na Sheria ya Vyama vya Siasa,” amesema.

Kuhusu yanayotarajiwa kufanyika mwaka 2024, Rais Samia amesema ni kuadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuendeleza program ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT).

“Mwakani pia, kwa mujibu wa sheria tutaboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Natoa wito kwa wote wenye sifa wajitokeze pindi zoezi hilo litakapotangazwa na Mamlaka husika,” amesema.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana zaidi na taasisi tanzu za kampuni changa na kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ustawi wake.

“Pamoja na mikutano mingine, tutakuwa wenyeji wa Kilele cha Nchi 25 za Afrika zinazozalisha Kahawa,” amesema.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi