Kitaifa
‘Jengeni maghala kuepuka gharama za kukodi’
Tabora. Vyama vya msingi vya ushirika mkoani hapa vimeagizwa kuhakikisha vinakuwa na maghala yake, ambayo mbali ya kuyatumia katika masoko ya tumbaku pia yatakuwa kama vitega uchumi vya vyama hivyo
Mbali na kutakiwa kuwa na maghala yake, pia vyama hivyo vimehimizwa kujenga ofisi zake ambazo zitatumiwa na wanachama kupata huduma sehemu inayoeleweka.
Akifungua ofisi ya chama cha msingi cha Hekima kilichopo wilayani Kaliua leo Desemba 27, 2023 Mrajis msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Tabora, Venance Msafiri amesema vyama havina budi kuwa na maghala watakayoyatumia wakati wa masoko ya tumbaku na hivyo kuepuka usumbufu wa kukodisha kwa fedha nyingi.
“Jengeni maghala ambayo, mbali ya kuwa vitega uchumi vya vyama pia yataokoa fedha za kukodi maghala au kuhangaika wakati wa masoko kutokana na kutokuwa na maghala ya kuhifadhi tumbaku,” amesema.
Pia amevitaka vyama vya msingi kuhakikisha wakulima wa tumbaku wanajiandikisha katika mfumo ili watambulike kwa ajili ya mahitaji ya pembejeo sanjali na masoko wakati utakapofika wa kuwatambua hata kwenye masoko ya tumbaku.
Mwenyekiti wa chama hicho kilichoanzishwa msimu wa 2020/21, Joshua Madunda amesema wamejenga ofisi yao iliyogharimu zaidi ya Sh24 milioni ikiwa pia na ofisi ya mtendaji wa kijiji na ukumbi wa vikao.
Ameeleza kuwa wanajipanga kujenga ghala la chama na tayari wamekubaliana kuchangia kupitia mapato ya tumbaku huku kikipanga kukusanya Sh80 milioni na kutumia Sh76 milioni msimu ujao wa 2023/24.
“Tumejipanga kujenga ghala letu na tunajivunia kuwalipa wanachama wetu kwa asilimia mia moja katika misimu miwili mfululizo ingawa chama chetu bado ni kichanga kikiwa hakijatimiza hata miaka minne,” amesema.
Mwanachama Mwanaidi Hassan amesifu mafanikio ya chama hicho katika kipindi kifupi akisema wakiendelea kwa kasi hiyo kitakuwa chama kikubwa Wilayani Kaliua
“Mimi napongeza viongozi kwa kuongoza vizuri na kufanya wanachama tulipwe kwa asilimia mia moja kwa miaka miwili mfululizo, hili sio jambo dogo kwa chama ambacho hakina hata miaka minne tangu kianzishwe,” amesema.
Msimu uliopita chama hicho ambacho tayari kimepewa usajili wa kudumu, kilizalisha kilo 273,000 za tumbaku zenye thamani ya zaidi ya Sh600 milioni na msimu ujao kinatarajia kuzalisha karibu kilo 300,000.