Connect with us

Kitaifa

Usasa unavyobadili sikukuu mwisho wa mwaka

Dar es Salaam. Maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa kiasi kikubwa yamebadilisha utamaduni wa maadhimisho ya Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya nchini.

Ingawa sherehe hizi za mwishoni mwa mwaka huadhimishwa kwa namna tofauti kulingana na muktadha wa ama jamii au kikundi cha watu, lakini mambo ni tofauti na zilivyosherehekewa miaka ya nyuma.

Mathalani, teknolojia ya mawasiliano imekuwa na athari kubwa, watu wanatumia simu za mkononi, mitandao ya kijamii na zana nyingine za kidijitali kutuma salamu za Krismasi na Mwaka Mpya, picha au hata kushiriki matukio ya sherehe na familia na marafiki mbalimbali.

Hali hii imebadilisha jinsi watu wanavyoshirikiana na kusherehekea pamoja, hata kama wapo umbali mrefu.

Si hivyo tu, watu hivi sasa wanaweza kufanya ununuzi wa zawadi za sikukuu mtandaoni, hivyo kuwa na uwezo wa kupata bidhaa kwa wauzaji wa kimataifa au hata kushiriki kwenye mauzo ya mtandaoni.

Huduma kama vile kuchangia na kutoa zawadi za kielektroniki zinaweza kuwa njia mpya za kushiriki furaha za Krismasi.

Hivi sasa watu wanaweza kutoa zawadi za kielektroniki kama vile kadi za zawadi za mtandaoni au huduma za muziki, ambazo zinaweza kuwa tofauti na utamaduni wa kawaida wa kutoa zawadi.

Baadhi ya familia na marafiki wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kushiriki picha, video na hadithi za sherehe zao za Krismasi.

Wasemavyo wananchi

Dk Hellen Kijo-Bisimba anasema kila mtu au watu walikuwa na mitindo ya kusherehekea sikukuu za mwishoni mwa mwaka, ingawa sasa kuna mabadiliko makubwa.

“Nimekulia Moshi (mkoani Kilimanjaro), Krismasi ilikuwa suala la dini si sherehe tu, ikikaribia kokote walipo watu ilibidi waje nyumbani, haikuwa sawa kula sikukuu nje ya nyumbani (Moshi). Tulikuwa tunajipanga kwa ibada ya Desemba 24 usiku kwa kwenda kanisani,” anasema na kuongeza:

“Sasa ikifika Desemba 25 ilikuwa lazima tuvae nguo mpya, usipovaa unalia na watu wanakushangaa unaendaje kanisani bila kuvaa nguo mpya? Tukirudi baada ya kula chakula cha mchana tulikuwa tunaenda KCMC ambako kulikuwa na lifti, ni jengo pekee lililokuwa na huduma hii kwa wakati huo.”

Dk Bisimba, Mkurugenzi wa zamani wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), anasema kulikuwa na utaratibu wa kusalimiana kwa kadi zinazopambwa katika mti wa Krismasi.

Anasema sasa utaratibu huo ni kama umekufa, watu wanatumiana kadi za mtandao wa simu.

“Sasa hivi sikukuu zinachukuliwa kama ni likizo badala ya ibada, ingawa baadhi yao wanaichukulia kama ibada lakini si kwa ukubwa unaotakiwa kama zamani. Bado kuna watu wana utamaduni wa kwenda Moshi kusherehekea,” anasema.

Akizungumzia Mwaka Mpya, anasema waliungojea kwa hamu wakijiandaa kuupokea kwa shangwe, vigelegele na kupiga madebe.

“Sasa hivi kunapigwa fataki, watu wanakwenda kwenye nyumba za starehe, wengine nyumba za ibada hadi asubuhi,” anasema.

Mkazi wa Ubungo jijini Dar es Salaam, Almandus Boniface anasema zamani kulikuwa na utamaduni wa ndugu kutembeleana au majirani kupika chakula na kubadilishana.

Anasema ufukwe wa Bahari ya Hindi eneo la Posta Mpya ilikuwa eneo la kutembelea watoto kusherehekea sikukuu.

“Watu wazima walikuwa na kumbi zao za DDC Magomeni Kondoa na Kariakoo, Mlimani Park, Kimara Resort. Watoto walikuwa wanaenda Posta Mpya,” anasema na kuongeza:

“Nyakati kama hizi Kariakoo haishikiki, lakini sasa mambo yamebadilika, sikukuu ni kama jambo la ziada. Sikukuu imekuwa tarehe si tukio kama zamani, hapo awali mzazi kununua nguo ya mtoto ilikuwa lazima, asipokununulia anaonekana mtu mwenye roho mbaya.”

Kulingana na mabadiliko ya utamaduni wa maisha, anasema hivi sasa watu wa maisha ya chini na kati ndio utawakuta ufukweni Coco Beach wakiogelea, lakini wengine kila wikiendi kwao ni jambo la kawaida kutoka na familia kutembelea maeneo kama hayo.

“Sasa hivi familia zinakula pilau mara mbili au tatu kwa wiki, tofauti na zamani ulikuwa unakula sikukuu pekee,” anasema.

Mkazi wa Ubungo, Dk Aviti Mushi anasema: “Kulikuwa na utamaduni wa familia moja kupika chakula kingi na kuwakaribisha ndugu, jamaa na marafiki, watu wanakula na kufurahia hadi usiku. Sasa kuna tofauti, ni familia chache zina utamaduni kama huu, wengi ni kila mtu kivyake.”

Mkazi wa Njombe, James Lugome anasema kwao sherehe za mwisho wa mwaka zilikuwa na taswira ya kifamilia zaidi, akisema mambo kadhaa yalifanyika tofauti na sasa.

Mbali ya kufurahi pamoja, sherehe zilitumika kusuluhisha migogoro ya kifamilia iliyojitokeza ndani ya kipindi cha mwaka mzima.

Anasema kama kuna ndugu mkorofi alikuwa anakanywa ili asiendelee kuleta mgawanyiko kwenye familia.

“Sherehe za mwisho wa mwaka zilikuwa ishara ya mshikamano wa kifamilia na kijamii. Kuna wale ambao katika imani zao walikuwa wanaandaa maombi maalumu ya kumshukuru Mungu,” anasema.

Anasema uwepo wa simu za mkononi kwa kiasi kikubwa umepunguza haja ya watoto kurudi kwa wazazi mwisho wa mwaka kwa sababu wanaona muda mwingi huwa wanawasiliana na kuwajulia hali.

Yasir Marijani anasema ni muhimu watoto kuwa karibu zaidi na wazazi kusikiliza yanayowasibu na kuona namna ya kuyatatua.

“Katika hili baadhi ya familia kuna watoto zaidi ya wawili au watatu, mnaweza kukaa na kujipangia nani atafanya nini na kupeana muda wa kulikamilisha tena mbele ya wazazi ili wajue kuna wanaowafikiria,” anasema Marijani.

Elisante Tarimo anasema kipindi cha sherehe ni vizuri kurekebisha nyumba za wazazi kama jambo hilo halikufanyika kwa mwaka mzima.

Tarimo anasema unapofanya ujenzi unaongeza furaha kwa wazazi.

Issa Njarabi anasema kwa kuwatembelea wazazi unaweza kubadilisha mwonekano wa ndani ya nyumba kwa kubadilisha mpangilio wa samani za ndani au hata kununua mpya.

Ernest Mkali anasema wazazi hupenda kuona unawajali ndugu zao, ikiwamo kwenda kuwasalimia.

Hivyo, katika kipindi hiki mtu atakapoenda kwao anasema ni vizuri kutembelea jamaa wengine.

Mayasa Rashid anasema baadhi ya watoto wakienda nyumbani kwa wazazi ni kama wanaenda kujionyesha kwamba wana magari mazuri na nguo nzuri na wanapoondoka huwaacha wazazi wao kama walivyowakuta.

“Baadhi kipindi hiki wapo tayari kuazima magari ya watu kwenda kujionyesha kwa ndugu na jamaa huko walikozaliwa. Fedha ya kukodi gari angeweza kuwafanyia jambo wazazi wakamuongezea baraka kwa kumuombea,” anasema Mayasa.

Umakini kwa watoto

Kuongezeka kwa matukio ya ndugu wa familia moja kuwafanyia vitendo vya ukatili watoto kama vile kuwabaka, kuwanajisi na kuwalawiti pia kunatajwa kuathiri sherehe za pamoja za familia.

Hisia ya unyanyasaji inaweza kufanya iwe vigumu kwa watoto kujisikia kuwa salama.

Martin Liamba, mkazi wa Tabata anasema imefika wakati ambao haamini na anashindwa kuruhusu ndugu wa jinsi moja kulala na mtoto wake wa kiume.

“Ijapokuwa nimemfundisha lakini inanipa ugumu sana, matukio ni mengi, tahadhari kama wazazi inabidi tuchukue ili kuhakikisha kipindi hiki cha furaha hakiathiri ukuaji wa watoto,” alisema Liamba.

Vicent Maugo anasema huwazuia watoto wake walio na umri chini ya miaka 18 kwenda sehemu peke yao na kulala hukohuko.

“Hali ilivyo sasa, watoto watawafahamu ndugu wakiwa wakubwa, wanajielewa, wanajua namna ya kujilinda, siwezi kukosa amani kwa sababu ya kumruhusu mtoto kwenda kumsalia mtu mwingine,” anasema.

John Ambrose, ambaye ni mwanasaikolojia anasema kipindi cha sikukuu ambacho familia zinajumuika ni muhimu kwa wazazi kuhakikisha wanalinda malezi na makuzi ya watoto waliyoyajenga ndani ya familia.

Anasema ni vyema wazazi kulinda watoto wao kuhakikisha hawaathiriwi na mila na desturi na muingiliano wa wageni watakaowatembelea.

“Pia ni vyema kuhakikisha wanawalinda na vishawishi na vichocheo vya mahusiano vinavyoweza kuleta athari kwa watoto wa eneo husika,” anasema.

Anasema kuna umuhimu wa watoto kufundishwa ulinzi binafsi hasa unaohusu miili yao.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi