Kitaifa

Papa atangaza Mafinga jimbo jipya Katoliki

Dar es Salaam. Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Fransisko ametangaza eneo la Mafinga mkoani Iringa kuwa Jimbo Jipya Katoliki na kumteua Padri Vincent Mwagala wa Jimbo Katoliki la Iringa kuwa askofu wa kwanza wa jimbo hilo jipya.

Kwa mujibu wa taarifa ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) iliyosainiwa na katibu wake mkuu, Padri Charles Kitima, leo Desemba 22, 2023, uteuzi huo unaanza leo huku jimbo hilo likipewa jina katika lugha ya kilatini ‘Mafingens’.

Askofu Mteule Mwagala amezaliwa Desemba 11, 1973 huko Makungu Wilaya ya Mufindi, Jimbo Katoliki la Iringa.

Baada ya masomo ya upadri, alipewa daraja takatifu la upadri Julai 11, 2007 jimboni Iringa na kuhudumu katika nafasi tofauti za utume nchini Italia na jimboni Iringa.

Mwaka 2018, Askofu Mwagala aliteuliwa kuwa Makamu wa Askofu na mwaka 2019 aliteuliwa kwenye baraza la washauri wa Askofu jimboni humo hadi kupata uteuzi huo mpya.

“Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, linamwombea Mhashamu Askofu Mteule, Vincent Cosmas Mwagala afya ya roho na mwili katika utume huo mpya jimboni Mafinga,” imesema taarifa hiyo.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi