Kitaifa
BoT yaja na mwarobaini ‘kausha damu’
Dar es Salaam. Huenda kesi za mikopo umiza maarufu kama ‘kausha damu’ na viwango vya mikopo chechefu katika benki vikapungua baada ya kuzinduliwa kwa mtalaa wa mpango wa elimu kwa wakufunzi wa elimu ya fedha.
Kuzinduliwa kwa mtalaa huo kunalenga kuongeza ufahamu juu ya namna ya kusimamia mikopo, madeni na majukumu ya kifedha, ulinzi wa fedha binafsi
unaojumuisha uelewa wa umuhimu wa bima na usimamizi wakati wa tahadhari.
Pia kozi hiyo itatoa ujuzi wa hesabu za fedha na kuboresha usimamizi wa fedha ikiwemo kuongeza ufahamu wa masoko na taasisi.
Akizungumza katika uzinduzi wa mtalaa huo, Gavana wa Benki kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba alisema kuzinduliwa kwake kunalenga kutatua changamoto mbalimbali zenye madhara kwa wananchi, taasisi, vikundi na hata mnyororo wa upatikanji fedha na ukuzaji uchumi.
Alisema anaamini itakuwa ni fursa ya kuonekana kwa matokeo chanya katika upatikanaji mikopo, matumizi na urejeshaji.
“Tunafahamu katika benki ile hali ya mikopo chechefu inatokana na kutokuwepo kwa ujuzi au elimu stahiki kuhusu masuala ya kifedha. Hata unapokuta katika taasisi za mikopo zimekusanya Tv, redio na friji huenda inatokana na watu kukosa elimu ya fedha,” alisema Tutuba.
Alisema kukosekana kwa elimu ya fedha kumewafanya baadhi ya watu wakiwemo watumishi wa umma kama walimu na wauguzi, kuchangamkia mikopo wanapoisikia bila kujua nini wanataka kufanya.
“Huwa hawafikirii
gharama za mikopo zikoje, afanyie nini, yeye anawaza kwanza apate fedha na akishakuwa nazo mkononi ndiyo atajua anafanya nini. Hakuna maisha ya hivyo, ukiwa mtu wa kuchukua fedha bila kujua shughuli ya kuzifanyia hautakuwa mtu wa kupiga hatua kutoka ulipo,” alisema Tutuba.
Alisema tayari, Chuo cha Benki Kuu cha Mwanza kimeshapewa maelekezo kitengeneze moduli za kufundishia wanaotoa mikopo ya ‘kausha damu’ wafundishwe.
“Kupitia mtaala huu kama wanaofanya biashara hizo watapata elimu na wakopaji wakapata elimu, tutapunguza changamoto ya kuwa na mikopo umiza,” alisema Tutuba.
Wakati haya yote yakifanyika, Tutuba alisema ili kuhakikisha mikopo inayotolewa haiendelei kuumiza watu, Serikali imeendelea kusisitiza uwepo wa uwazi kwa taasisi zinazojihusisha na biashara hiyo na sasa wamezitaka kuwa na sera ya ukopeshaji.
Hiyo inalenga kuwafanya watu kufahamu kwa undani kile wanachokwenda kukifanya kabla ya kuchukua mkopo, ikiwemo masharti na wajue kuwa wanaingia mkataba na kabla ya kufikia makubaliano lazima pande zote ziridhie ikiwemo suala la riba.
“Ikiwezekana, ni vyema kutumia hata ‘kalkuleta’ na mtu akiambiwa riba afahamu kuwa ni ya wiki, mwezi au siku, lakini si kupewa mahesabu ya jumla.
Ili kuhakikisha mtalaa huo unawafikia watu wengi, Gavana ametoa miezi miwili kwa wahusika kuutafsiri na kuuweka katika lugha ya Kiswahili.
Alitaka matokeo ya mtalaa huo kupimwa kila baada ya muda fulani ili kupata taarifa ya watu waliofikiwa na wale waliofundishwa wafuatiliwe ili kujua utaratibu uliotumika kuwafundisha.
Akizungumzia suala hilo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa alisema hatua hiyo ni mahususi inayoweza kutoa Taifa katika shida linayopitia sasa.
Alisema wanawake wengi wameingia katika shughuli za ujasiriamali na wamekuwa wakikimbilia mikopo bila kujua athari zake kwa sababu ya kukosa elimu ya fedha na kiu waliyonayo ya kuboresha mitaji yao