Kitaifa
Bajeti ilivyoleta elimu bila ada kidato cha tano, cha sita
“Napendekeza kufuta ada ya kidato cha tano na sita ili kuwapunguzia wazazi na wanafunzi mzigo wa gharama,”alisema.
Alisema wanafunzi wa kidato cha tano ni takriban 90,825, huku wale wa kidato cha sita wakiwa 56,880, na kwamba mahitaji ya fedha kuwagharimia ni Sh10.339 bilioni.
Kwa hatua hiyo, elimu bila ada sasa itaanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita na mwaka huu, Serikali ilisema imetenga fedha kwa ajili ya kugharamia programu hiyo ambapo hadi Aprili 2023, jumla ya Sh661.9 bilioni zilikwishatolewa.
Mpango wa elimu bila ada
Rais wa awamu ya tano, hayati Dk John Magufuli mwaka 2015, alisema Serikali yake ingefuta ada kwa wanafunzi wa darasa la kwanza hadi kidato cha nne. Kauli yake ilikuwa ni marejeo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) alichokuwa akikiwakilisha.
Mwaka 2016 Rais Magufuli akiwa madarakani, wanafunzi walianza kunufaika kusoma bila kulipa ada ambapo Serikali kila mwezi ilitenga Sh28 bilioni kufanikisha mpango huo.
Mafanikio ya mpango huo wa Serikali yalionekana, hasa upande wa ongezeko la usajili wa wanafunzi shuleni.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa Novemba 2017 na Ofisi ya Rais Tamisemi, idadi ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza iliongezeka kutoka 1,282,000 mwaka 2015 hadi 1,896,000 mwaka 2016, likiwa ni ongezeko la asilimia 84
Wanachosema wadau
Mwanaharakati wa masuala ya elimu, Alistidia Kamugisha, anasema elimu bila ada itaipaisha Tanzania kimataifa.
Anasema elimu bila ada itaifanya Tanzania kuwa nchi inayoenda kasi kuchangia mpango mkakati wa Afrika wa kuboresha eliimu kwa watu wake ukiwa unachangia kutimiza Lengo la Maendeleo Endelevu namba (4) (SDGs 4) linalopigia upatu elimu bora na jumuishi kwa watu wote na kuhimiza fursa za kujifunza maishani kwa watu wote.
Kwa mujibu wa Alistidia, kufutwa kwa ada kidato cha tano na sita kumeifanya Serikali kujiongezea thamani kwa wananchi wa kawaida ambao walihangaika kupata ada ili kuwasomesha watoto wao.
Alisema hatua hiyo ya Serikali imewafanya wazazi wa kipato cha kati na wale wenye utashi kupata nafuu ya mzigo wa maisha kwa kuwatoa watoto wao shule za kulipia na kuwapeleka shule za Serikali.
“Elimu bila ada imewapa nafasi wazazi nafasi kutimiza majukumu mengine yaliyokuwa yakiahirishwa ili wapate fursa kwanza ya kulipa ada za watoto wao,”anasema.
Mbali na hayo, anaeleza kuwa wanafunzi wenyewe wamejengewa mazingira ya amani na utulivu wa akili na kuzingatia masomo, badala ya kufikiria kufukuzwa darasani kwa kukosa ada.
“Mwaka 2024 nashauri tujiimarishe zaidi kuingia kwenye mabadaliko makubwa ya mfumo wa elimu, kuboresha Sheria ya Elimu na kuandaa mpango mkakati jumuishi wa utekelezaji unaolenga zaidi ufadhili wa ndani kwa asilimia kubwa,”anasema.
Anashauri Serikali kufanya tathmini ya mpango mkakati wa Elimu wa Umoja wa Afrika unaofikia ukomo wake 2025.
Kwa upande wake, Mwalimu Samson Sombi kutoka mkoani Morogoro, anasema mpango wa Serikali kuondoa ada kwa kidato cha tano na sita, umesaidia wanafunzi kuwa na morali ya kusoma.
Anasema kabla ya kuondolewa ada hiyo, wanafunzi wengi waliishia kidato cha nne baada ya kukosa ada.
“Mwanafunzi anapangwa shule ya mbali, ada na nauli mzazi hana hivyo mtoto anatafutiwa chuo chenye ada ndogo anaanza kusoma. Lakini kwa sasa huu utaratibu wa kusoma bila ada, utawafanya wazazi kuwahimiza watoto wao kusoma kwa juhudi zaidi,”anasema.
Mwalimu Sombi anasema, idadi ya wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne na sita na kujiunga na vyuo, itazidi kuongezeka kwa kiwango kikubwa.
Hata hivyo, kwa mwaka ujao, Mwalimu Sombi anashauri Serikali iboreshe zaidi mazingira ya kufundishia na kujifunzia, walimu wa masomo ya sayansi pamoja na maabara.
Kwa upande wake Mtheolojia wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Usharika wa Boay wilayani Babati, mkoani Manyara Elieth Mtaita, anasema kufutwa kwa ada ina maana kubwa kwa wazazi na walezi ambao kipato chao ni kidogo.
“Lakini ni vema kuchukua tahadhari kwa kuwa tuliwahi kushuhudia ada ikifutwa kwa daraja fulani la elimu lakini michango ikawa mikubwa kuliko ada iliyofutwa, hii ilikuwa kero zaidi,”anaeleza.
Anachoshauri Mtaita Serikali itoe elimu ya kutosha kuhusu mfumo wa elimu nchini na kudhibiti utitiri wa michango ambayo humuumiza zaidi mzazi au mlezi.
“Serikali iboreshe elimu kwa viwango vyote na isimamie kwa uhakika elimu inayotolewa,”anasema.
Tugeukie mitalaa
Pamoja na mafanikio kwa upande wa ada, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) Christian Bwaya, anasema hatua ya Serikali kusuka upya mitalaa kwa elimumsingi, imekuja wakati mwafaka.
“Kama mdau ninayeshughulika na walimu, natambua changamoto iliyokuwepo ya nyaraka za maalaa (mfano mihutasari ya masomo) kwa ngazi ya sekondari kujikita zaidi kwenye maudhui badala ya mahiri.
Katika mazingira ambayo mwalimu alitarajiwa kufundisha kwa mbinu zinazokuza mahiri, kazi ilikuwa ngumu sana tofauti na ngazi ya awali na msingi ambapo mtalaa ulikuwa wa umahiri,”anasema.
Bwaya anasema kazi hiyo ilileta mkanganyiko mkubwa, wakati mwingine kuwaingiza walimu kwenye mgogoro na wathibiti ubora. Hii ni kutokana na mwalimu kugeuzwa mkuza mitalaa anayelazimika kufikiri namna ya kugeuza malengo mahususi na shughuli za ujifunzaji ziwen na mrengo wa umahiri.
Anasema tatizo hilo halitakuwepo sasa, kwani mwalimu anakutana na nyaraka zenye umahiri kwa uwazi, na sasa kazi yake itakuwa kutekeleza kwa kuzingatia mazingira ya shule yake.
“Changamoto ninayoiona ni kiwango cha maandalizi kwa walimu. Namna gani mwalimu ameandaliwa kutekeleza mtalaa huu utakapoanza kutumika? Natamani Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iwekeze kwa kiasi kikubwa kwenye mafunzo ya walimu. Iwaandae kikamilifu namna ya kutafsiri nyaraka za mitalaa katika mazingira yao ya darasanI,” anasema.
Bwaya anasisitiza kuwa endapo hakutakuwa na uwekezaji wa kutosha, kazi kubwa iliyokwisha kufanyika haitaleta matokeo yanayokusudiwa.
Jambo lingine, Bwaya anasema kwa ngazi ya msingi na awali, changamoto kubwa anayoiona, ni namna ya kuandaa shughuli mahususi za ujifunzaji zinazokuza umahiri mahususi kama mitalaa inavyotaka.
Pia, Bwaya anasema kuna changamoto katika maandalizi ya ujifunzaji hasa yale ya nusu mwaka au mwaka mzima, yanayofahamika kama maandalizi ya somo
Anaeleza kuwa, walimu wengi wanahamisha tu yaliyoandikwa kwenye mihutasari kwa minajili ya kuwaridhisha wathibiti ubora, lakini hakuna namna mwanafunzi anashirikishwa kutafuta na kuchambua maarifa nje ya darasa.