Connect with us

Kitaifa

Uzalishaji umeme Bwawa la Nyerere kuanza Januari 2024

Rais Samia amesema baada ya kuwashwa kinu cha kwanza, cha pili kitawashwa kabla ya Aprili 2024, hivyo kuongeza uzalishaji wa umeme.

Amesema hayo jana usiku Jumapili, Desemba 17, 2023 katika hafla ya utoaji tuzo za Rais kwa Wazalishaji Bora (PMAYA). Pia amesema pamoja na jitihada nyingine uwashaji wa vinu hivyo vitakwenda kupunguza malalamiko la kukatika kwa umeme.

“Pamoja na jitihada nyingine za gesi, sola na mambo mengine, lakini katika umeme wa hydro (maji) tunategemea nadhani katikati ya mwakani malalamiko mengi yatakuwa yamepungua,” amesema Rais Samia.

Pia amesema licha ya sekta ya viwanda kushuka duniani, bado Tanzania imesimama na kufanya vizuri. Kwa mujibu wa Ripoti ya Dunia ya 2024 ukuaji wa viwanda ulimwenguni umeshuka.

Amesema takwimu hizo zinaonyesha mambo mawili ambayo endapo kuna changamoto ya kushuka kwa viwanda, kuna haja ya Serikali kukaa na wenye viwanda ili kuzungumza kwa uwazi na kusema wanayoyaona na wao kupokea na kuyatekeleza.

Jambo la pili ni jitihada za Serikali, lazima kulenga katika utegemezi wa viwanda vya ndani kutumia malighafi kutoka nje na kutafuta mbadala wa malighafi hapa nchini au kuvutia uwekezaji zaidi wa malighafi inayotumika kwenye viwanda vingine.

“Nimeambiwa kuna kufanya ‘assembling’ ya magari kule Kigamboni, lakini vioo wanavyotumia vinazalishwa hapa Tanzania kule Mkuranga. Tukiwa na viwanda vingi vya namna hiyo vitatusaidia kupunguza gharama za kununua malighafi nje na kupunguza uzalishaji,”amesema Rais Samia.

Akizungumzia stempu za kielektroniki, amesema wapo kwenye mazungumzo na shirika linalotengeneza na kuna dalili kukubali kushusha gharama za stempu.

Shirika hilo ambalo limezungumziwa ni la Societe Industielle de Produits Alimentaire (SICPA) la Uswisi linaloendesha mradi wa stempu za kodi za kielektoniki.

Hata hivyo, Rais Samia amesema wanaangalia uwezekana na wameanza mazungumza na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) watumie mfumo wa kielektroni, badala ya kusumbuana na mtu.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi