Kitaifa

RC Chalamila: Wanaopata sifuri kidato cha nne watambuliwe

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema imefika wakati wa kuanza kuwatambua watu wanaopata daraja sifuri katika mitihani ya kidato cha nne na kuwafanyia utafiti.

Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Desemba 16, 2023 alipokuwa akitoa salamu katika maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), yaliyofanyika ofisi za baraza hilo jijini jijini hapa, huku Rais Samia Suluhu Hassan akiwa mgeni rasmi.

Chalamila amesema, Necta ni sehemu ambayo haiwezi kutazamwa na jicho zuri na wanafunzi ambao hawakufanya vizuri, huku akisikitika kwa nini wanaofanya vizuri pekee ndiyo wanatambuliwa.

“Hapa ndiyo tunawapata wanafunzi wenye vipaji maalumu ingawa masikitiko yangu Necta huangalia tu wenye vipaji maalumu vya kufaulu sana, wale wenye vipaji maalumu vya kufeli waliopata zero (sifuri) ni kama bado hawajatambuliwa lakini muhimu kuwatambua, kuwafanyia utafiti, miaka minne kukaa darasani na kupata sifuri kuna kitu cha kujifunza,” amesema Chalamila.

Chalamila anatoa kauli hiyo ikiwa siku chache tangu wanafunzi wa kidato cha nne wafanye mitihani yao ya mwisho ya kumaliza elimu ya sekondari.

Hata hivyo, amesema idadi ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu jijini Dar es Salaam ni 53,814 ikilinganishwa na wanafunzi 640,000 waliosajiliwa kidato cha kwanza.

Takwimu hizo zinaonyesha, wanaoacha shule wengi ni watoto wa kike huku akieleza kupitia hilo Rais Samia Suluhu Hassan aliuagiza mkoa ujielekeze kujenga mabweni yatakayosaidia wanafunzi wa kike.

“Nikuthibitishie, tumepanga na wenzangu kuhakikisha kwa haraka walau kila shule inakuwa na bweni ili kusaidia watoto wa kike, kufanya hivi tutakuwa tumekomboa Taifa na kumnusuru mtoto wa kike na matendo yanayomuathiri,” amesema Chalamila.

Katika uboreshaji elimu, Chalamila amesema Sh1.243 bilioni zimekuwa zikitolewa kila mwezi katika mkoa wake kwa ajili ya utekelezaji elimu bila malipo, jambo linaloweka uhai wa Necta.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi