Kitaifa
Bunge la Ulaya laishauri Tanzania kuwahamisha Wamasai Loliondo, yenyewe yajibu
Dar es Salaam. Wakati Bunge la Ulaya likitoa azimio la pamoja la kuishauri Serikali ya Tanzania kuhusu suala la kuhamishwa jamii ya Wamasai eneo la Loliondo linapaswa kuzingatia haki za binadamu, yenyewe imesema inaziheshimu haki hizo.
Azimio hilo lilitolewa Desemba 13 mwaka huu, Bunge hilo likisema halijapinga suala la uhifadhi wa mazingira isipokuwa limejikita kwenye utekelezwaji, unaopaswa kuzingatia haki katika kuleta usawa na bayoanuwai.
Hii ni mara ya pili kwa Bunge la Ulaya kutoa azimio hilo kwani mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 2014 lililoegemea kwenye hoja hiyo na kuishauri Serikali ya Tanzania kuzingatia haki na Serikali ilisitisha mpango huo.
Juni 2022, Serikali ilihuisha tena mpango huo wa kubadilisha kilomita 1,500 za ardhi ya Loliondo kuwa pori tengefu na iliamriwa wakazi waliokuwa wakiishi eneo hilo kuhamishiwa Msomera, Handeni mkoani Tanga kupisha uhifadhi huo.
Tayari baadhi ya kaya zimehama kwa hiari na sasa zinaendelea na maisha Msomera ambako Serikali imewajengea nyumba za kuishi.
Kwa mujibu wa azimio la Bunge hilo, kutengwa kwa eneo hilo kumesababisha zaidi ya watu 70,000 kukosa ardhi ya malisho ambayo ni muhimu kwa afya ya mifugo yao na maisha yao.
Limesema pamoja na Serikali kuja na mpango wa kuwahamisha lakini limebaini kuna mashauriano duni kati ya Serikali na jamii za Wamasai zilizoathirika na ukosefu wa uwazi.
“Tangu Juni 2022 katika Hifadhi ya Ngorongoro, Serikali imezuia upatikanaji wa huduma muhimu kama vile chakula, elimu, maji na huduma za afya, hivyo kulazimisha kuondoka kwa jamii nyingi za Wamasai,’’ imeeleza taarifa ya Umoja huo
Bunge hilo limeishauri Tanzania, kusitisha mara moja uhamishaji wa kutumia nguvu kwa jamii ya Kimasai, ili kuepuka hatua zozote zitakazoathiri maisha, na tamaduni za jamii hizo.
Bunge hilo limeshauri Serikali ya Tanzania kuruhusu taasisi za Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya kutembelea Ngorongoro.
Kauli ya Serikali
Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, alisema ni kweli Bunge hilo lilikaa kupiga kura na kufikia azimio hilo.
Alisema Serikali ina uhusiano mzuri na Umoja wa Ulaya (EU) na hivi karibuni kamishna wa umoja huo alisema Tanzania ni mshirika wa kimkakati na ushirikiano huo utaendelea.
Matinyi alisema ushirikiano wa Tanzania na EU katika kipindi hiki umeendelea kuwa mzuri hasa katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na inaheshimu uhuru wa Tanzania.
Alisema umoja huo umeipongeza Tanzania kwa kuweka asilimia 43.7 ya eneo la nchi yake chini ya hifadhi na ni mfano wa nchi zinazohifadhi maeneo yake vizuri, akisisitiza Ngorongoro na Serengeti ni maeneo nyeti.
“Huyo ni kamishna wa Umoja wa Ulaya akiielezea Tanzania na kilichotokea mwaka jana Mei kulikuwa na kundi la wananchi waliotoka maeneo ya Ngorongoro na walikwenda kule (EU) kwenda kutoa hoja zao na Serikali ilipata nafasi ya kujieleza,” alisema.
Alisema Agosti baadhi ya wabunge wa Bunge la Ulaya waliiomba Serikali kuja kutembelea eneo la Ngorongoro, na walitoa siku chache kwani waliomba Agosti mwishoni na walitaka kuja mwanzoni mwa Septemba.
Matinyi alisema Serikali iliwakaribisha lakini wakawaeleza ombi lao wamelitoa kwa muda mchache, muda wa kujiandaa kuwapokea haukutosha waliwaomba wajipange na Serikali ijiandae kuwapokea waone Ngorongoro na mambo yake.
“Kwa hiyo Serikali haijawahi kuwazuia wanaotaka kuja katika eneo hilo,” alisema.
“Lakini tunapozungumzia kufanya ukaguzi wa kitaalamu wataalamu wa Unesco wanatarajia kuja kujionea na kufanya ukaguzi Januari 2024 iwapo kweli kuna madai ya ukiukwaji wa haki za kibinadamu na wafahamu wananchi wanaoishi Ngorongoro wanaishi kwenye hali gani na wafahamu Serikali inataka kuwapeleka kwenye eneo gani,” alisema.
Alisema Serikali inaheshimu haki za binadamu, inawajali watu wake na wasingependa waendelee kuishi kwenye ufukara uliopitiliza wakati nchi yote ikiendelea mbele.
“Kwa hiyo tunachoweza kusema ni kwamba taasisi na watu mbalimbali wanaweza kutoa maoni lakini ukweli uko hapa na nchi yetu inaheshimu haki za binadamu na itafanya zoezi hili kwa hiari hakuna kutumia nguvu,” alisema.