Connect with us

Kitaifa

Viwanda bubu chanzo kuzagaa bidhaa bandia

Dar es Salaam. Ongezeko la viwanda bubu vinavyozalisha bidhaa mbalimbali nchini, limeelezwa kuwa pigo kwa wazalishaji halisi, huku Serikali ikiwataka wafanyabiashara kuungana kukabiliana na changamoto hiyo.

Kauli hiyo ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Hashil Abdallah inakuja baada ya wasilisho la Tume ya Ushindani (FCC) jijini Dar es Salaam jana iliyoonyesha kuwa bidhaa nyingi bandia ilizokamata zimetoka viwanda bubu.

“Adui anaweza kuwa miongoni mwetu kwa sababu, kila mfano niliousikia katika kongamano hili ulihusisha kiwanda (bubu), ipo haja ya kufanya jitihada za makusudi kuondoa hali hii katika nchi yetu kwa ajili ya viwanda vyetu,” amesema Dk Abdallah wakati wa kongamano la kupambana na bidhaa bandia ili kuwalinda watumiaji na kuimarisha ushindani wa viwanda nchini.

“Watu hao ndio wanaoharibu dira ya Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) dhidi ya bidhaa bandia na kwa kufanya hivyo, wanaharibu mwelekeo wa Serikali na nchi kwa jumla.”

Hata hivyo, Mwenyekiti wa CTI, Paul Makanza alisema kutokana na kanuni zinazotumika sasa nchini, si lazima kwa kila mmiliki wa kiwanda kuwa mwanachama wa CTI, hivyo kufanya ufuatiliaji wa viwanda kuwa na changamoto.

“Moja ya changamoto tunayokumbana yazo ni kutokuwa na sera wala kanuni inayomlazimisha mwenye kiwanda kuwa mwanachama wa CTI, kungekuwa na sera au kanuni ya namna hii ingekuwa rahisi sana kufanya ufuatiliaji,” amesema Makanza.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Kuzuia bidhaa bandia kutoka FCC, Khadija Ngasongwa alisema ni muhimu kwa wadau wa biashara, Serikali, sekta binafsi na CTI kuungana ili kuweza kuwafichua wahusika wa bidhaa bandia nchini ili viwanda vinavyotengeneza bidhaa halisi viweze kustawi.

“Watu hawa wanaojihusisha na bidhaa feki wanaharibu biashara zingine za watengenezaji waaminifu, hivyo kuathiri uchumi wa Taifa,” amesema Ngasongwa.

Pia, alisema ni vyema kwa yeyote atakayeona dalili za kuwepo kwa kiwanda cha aina yoyote ambacho utaratibu wake wa kufanya kazi haueleweki, atoe taarifa FCC ili wafanye uchunguzi wa haraka kubaini iwapo kinafanya kazi kihalali au la.

“Kwa bahati mbaya, watu wengi hawatuelezi. Kutoa taarifa ni muhimu sana katika kupambana na bidhaa za kughushi nchini. Ni jukumu la kila mmoja wetu, kwa sababu sote tumeathiriwa na bidhaa hizo feki,” ameeleza.

Onyo kwa wafanyabiashara

Oktoba 25 mwaka huu, FCC Nyanda za Juu Kusini iliwaonya wafanyabiashara wasiowaaminifu kujiepusha na uagizaji, uzalishaji na uuzaji wa bidhaa bandia ambazo zimekuwa zikiwadhuru watumiaji hapa nchini.

Mkuu wa Kanda, Ofisi ya FCC Nyanda za Juu Kusini, Dickson Mbanga alitoa onyo hilo katika viwanja vya Maonesho ya Nne ya Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) mkoani Njombe.

Amesema wafanyabiashara na wazalishaji wana wajibu wa kusajili nembo zao ili kulindwa na sheria ya alama za bidhaa zao dhidi ya wazalishaji wanaoiga bidhaa zao kwa nia ya kudanganya au kutapeli.

Mbanga alisema wazalishaji au wajasiriamali wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanaonyesha taarifa zote muhimu katika vifungashio kama Sheria ya alama za bidhaa ya mwaka 1963 inavyoelekeza.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi