Makala
Mwanamke anayependa maisha ya gharama hakupendi
Anti habari. Kuna mwanamke nipo naye, lakini watu wananiambia amenipendea pesa kwa sababu mimi na yeye ni tofauti. Kweli nakiri tupo tofauti sana, kwani huyo dada ni pisi kali kwelikweli na anajipenda.
Nisaidie nitamjuaje mwanamke anayenipendea pesa.
Kwanza hizo pesa unazo? Maana nisije kumaliza nguvu bure kumbe huna kitu. Tuachane na hayo kwa vyovyote vile mapenzi yanahitaji uwepo wa pesa, hata kidogo kwa ajili ya kujikimu.
Lakini kuna hawa wanaoitwa kimombo ‘Gold Digger’, ambao ni shida kwa sasa.
Si rahisi kumjua au kuwa na majibu ya moja kwa moja, lakini mara nyingi hupenda kula bata katika maeneo ya hadhi ya juu. Yaani siku zote anapenda vitu vya hadhi na gharama kubwa bila kujali una uwezo au huna, ndiyo maana hawahangaiki na wasiokuwa na pesa kwa sababu nia yao ni kuzichuma.
Hawafikirii maendeleo, kila ukikaa naye anakupanga tu kuhusu matumizi ya pesa, kufanya manunuzi kwenye maduka makubwa na kwenda kula katika hoteli za kifahari kwa madai ya kukutana na watu tofauti.
Pia hupenda zawadi zawadi lakini za gharama kubwa. Akiwa anaadhimisha siku ya kuzaliwa tu utafikiri anaozesha binti msomi jinsi anavyoalika watu, kukodi ukumbi na hafla kubwa. Hayo yote ayatendana na zawadi kubwa kutoka kwako. Yaani umuandalie pati ya kukata na shoka, mashoga zake wale wanywe na umpe zawadi itakayotrendi kwenye mitandao ya kijamii.
Siku jichanganye kumpeleka saluni akaoshe nywele utajuta, atatumia zaidi ya milioni, maana huko ndiyo wanawekeza sana watu hao, wanataka kuonekana nadhifu muda wote na wengi wao ndiyo hawa wanaobadili maumbile yao ili kuwavutia wenye pesa.
Hizi ni miongoni mwa tabia zao, kama huyo wa kwako hata hajadili mtajenga lini, anajadili kubadili magari, kusafiri ng’ambo, mawigi ya gharama, kubandika mikucha kama anaigiza sini ya jini, kuwa makini inawezekana kweli umeuvaa mkenge. Kumbuka si wote wenye sifa hizi wapo wa kimya kimya pia, ndiyo maana nasema ni ngumu kumjua, unaweza kupata mwanamke anajipenda tu, ila siyo Gold Digger.