Makala
Utafiti wabaini viungo 11 vinavyozeeka haraka kuliko umri wako
Dar es Salaam. Kama ambavyo uchunguzi wa uimara wa gari (MoT) unavyofanyika nchini Uingereza, wanasayansi wanaamini kuwa, wanaweza kuchunguza damu na hivyo kujua viungo vya ndani vya mwanadamu vinavyozeeka na hatari ya kushindwa kufanya kazi.
Shirika la Habari la Uingereza (BBC) limeripoti kuwa wanasayansi hao kutoka Chuo Kikuu cha Stanford, wamesema wanaweza kufuatilia viungo vikuu 11 vya mwanadamu ambavyo ni pamoja na moyo, ubongo, na mapafu.
Viungo vinge ni pamoja na ini, figo, utumbo, mafuta, mishipa ya damu, misuri, chembechembe hai, pamoja na kongosho.
Na kwamba wamejaribu kufanya hivyo kwa maelfu ya watu wazima hususani wenye umri wa kati na wazee.
Imeelezwa kuwa, katika uchunguzi huo, matokeo yanaonyesha kuwa mmoja kati ya watu wazima watano wenye afya njema, na wenye umri kuanzia miaka 50, ameonekana kuwa na kiungo kimoja kinachozeeka kwa haraka.
Aidha, uchunguzi huo umebaini kuwa mmtu mmoja au wawili kati ya watu 100, anaweza kuwa na viungo kadhaa ambavyo vina umri mkubwa kuliko umri wao halisi.
Hat hivyo inaelezwa kuwa japokuwa wazo la kufanya uchunguzi huo linaweza kutisha, hata hivyo watafiti hao wanasema inaweza kuwa ni nafasi ya kuingilia kati na kufanya mabadiliko.
Kujua kiungo gani kinaweza kushindwa kufanya kazi kwa haraka, kunaweza kusaidia kufichua mapema maswala kiafya ambayo yanaweza kumpata mtu, wamesema watafiti hao katika jarida la Nature.
Madhara ya kuwa na kiungo kilichozeeka kwa haraka, mfano moyo; kunaongeza hatari ya kiungo hicho kushindwa kufanya kazi, wakati ubongo unaozeeka haraka, unaweza kukabiliwa na matatizo ya akili.
Katika utafiti huo, kuwa na kiungo kimoja au zaidi vinavyozeeka haraka kumehusishwa na hatari kubwa kukumbwa na magonjwa ambayo yanaweza kusababisha vifo katika kipindi cha miaka 15 ijayo ya mtu husika.
Unapofanyika uchunguzi huo wa damu, maelfu ya protini mwilini hutafutwa ili kuona dalili juu ya viungo vinavyozeeka huku viwango tofauti vya kasi ya kuzeeka huko hutambuliwa.
Mmoja wa wachunguzi, Dk Tony Wyss-Coray, ameeleza: “Tulipolinganisha umri wa kibaiolojia wa viungo hivyo kwa kila mtu, tuligundua kuwa asilimia 18.4 ya wale wenye umri wa miaka 50 au zaidi, walikuwa na angalau kiungo kimoja ambacho kinazeeka kwa kasi zaidi.
“Na tuligundua kuwa watu hawa wako katika hatari kubwa ya kupata magonjwa ndani ya kipindi cha miaka 15 ijayo,” amesema Dk Tony katika taarifa hiyo ilichapishwa na BBC.
Baada ya utafiti huo, chuo kikuu hicho kimewasilisha maombi ya haki miliki ya jaribio hilo, ili baadaye ama liweze kuuzwa au kutumika.
Hata hivyo imeleezwa kuwa tafiti zaidi zinahitajika ili kuangalia namna nzuri ya kugundua umri wa kiungo na afya yake kabla ya hapo.
Profesa James Timmons, mtaalamu wa afya na magonjwa yanayohusiana na umri katika Chuo Kikuu cha Queen Mary cha London, amekuwa pia akifanya uchunguzi wa aina hiyo japo yeye anaangalia zaidi mabadiliko katika ‘genes’ badala ya protini.
Profesa huyo amesema matokeo ya hivi punde ya Dk Tony, yanaonekana kuvutia, hata hivyo anadai kuwa yanahitajika kuthibitishwa kupitia watu wengi zaidi, haswa vijana wanaotoka katika asili ya makabila na mataifa tofauti.
“Je, matokeo ya utafiti huu yanahusu kuzeeka au njia mpya ya kugundua mapema alama za ugonjwa unao husiana na umri? Amehoji.
Kwa upande wake Dk Jony amesema: “Ikiwa tunaweza kutoa matokeo haya kwa watu 50,000 au 100,000 itamaanisha kwamba kwa kufuatilia afya ya viungo vya mtu binafsi kwa watu wanaoonekana kuwa na afya, tunaweza kupata viungo vinavyoendelea kuzeeka kwa kasi katika miili ya watu, na tunaweza kuwatibu watu kabla ya kuugua.”
Profesa Paul Sheils, mtaalam wa biolojia ya uzee katika Chuo Kikuu cha Glasgow, amesema kuna umuhimu kuangalia mwili mzima, na siyo tu viungo pekee ili kujenga picha sahihi zaidi ya afya ya mtu.
Caroline Abrahams kutoka shirika la kutoa misaada la Age UK; amesema ingawa matokeo hayo yangekuwa mazuri kwamba sayansi inachunguza ugunduzi wa mapema wa magonjwa hatari yanayohusiana na uzee.
Iwapo utakuwa wa ukweli, amesema watu wangetaka msaada wa kihisia na kiafya pamoja na matokeo ya mtihani na kwamba taasisi ya afya nchini Uingereza (NHS) ingehitaji kuwa tayari kwa hilo.