Kitaifa

Tanesco yaomba radhi, yataja chanzo umeme kukatika

Dar es Salaam. Baada kukosekana umeme katika mikoa mbalimbali nchini kwa saa kadhaa, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limetoa ufafanuzi kuhusu changamoto hiyo, likieleza imetokana na hitilafu.

Hatua ya Tanesco imekuja baada ya umeme kukatika kwenye mikoa unayohudumiwa an gridi ya Taifa alfajiri ya leo, Desemba 8,2023.

Kwa mujibu wa taarifa ya kitengo cha mawasiliano Tanesco, ambayo imesambazwa kwa vyombo vya habari leo Ijumaa Desemba 8, 2023 umeme huo ulikatika baada ya nguzo  kubwa za kusafirisha umeme kutoka katika kituo cha kuzalisha umeme cha Ubungo III eneo la Mto Gide, Ubungo Kibangu jijini Dar es Salaam, kusombwa na maji.

Taarifa hiyo ambayo haikutaja kwa majina mikoa iliyohusika na kadhia hiyo, bali imeeleza kiujumla kuwa ni ile inayohudumiwa na umeme wa gridi ya Taifa.

Hata hivyo taarifa hiyo imeeleza kuwa umeme umeanza kurejea kwa awamu katika baadhi ya mikoa na  jitihada zinaendelea kuhakikisha mikoa yote inarejea katika hali ya kawaida.

Jitihadi nyingine zinazofanywa ni kuhakikisha miundombinu iliyoharibika inajengwa ndani ya muda mfupi, kuruhusu kusafirisha umeme unaokosekana katika gridi ya Taifa kutoka kituo cha kuzalisha umeme kwa gesi asilia cha Ubungo III.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi