Kitaifa
Matumaini mapya Rais Samia akitarajiwa kuzuru Hanang leo
Hanang. Waathirika wa janga la maporomoko ya matope wilayani Hanang, Mkoa wa Manyara wamepaza sauti zao wakitoa maombi maalumu kwa Rais Samia Suluhu Hassan anayetembelea eneo la maafa hayo leo.
Licha ya maafa hayo yaliyotokea Desemba 3 mwaka huu kusababisha vifo 69 hadi jana jioni na wameruhi zaidi ya 110, yaliharibu makazi ya watu, maeneo ya biashara na miundombinu mbalimbali, ikiwemo ya afya, barabara, umeme na maji.
Kutokana na maporomoko hayo, Rais Samia, aliyekuwa Dubai akishiriki Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28), anatarajiwa kutua katika eneo hilo kufuatilia shughuli zinazoendelea, zikiwemo za uokoaji na huduma mbalimbali kwa waathirika.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilieleza Rais Samia atatembelea maeneo yaliyoathirika na maporomoko hayo katika Mji wa Katesh, wilayani humo.
Mara baada ya taarifa hiyo iliyotolewa juzi jioni, timu ya waandishi wa gazeti hili walioweka kambi wilayani humo, walizungumza na waathirika wa janga hilo kupata mtazamo wao juu ya ziara hiyo ya mkuu wa nchi na kile wanachokitarajia.
Miongoni mwa waathirika hao ni wafanyabiashara ambao bidhaa zao za chakula kama mahindi, maharage na mchele zikiharibika vibaya, wengine wameachwa bila makazi kutokana na nyumba zao kubomoka. Pia, wapo waliowapoteza ndugu na wapendwa wao.
Nicholaus Lucas, mfanyabiashara wa mazao mchanganyiko anayemiliki stoo sita za kuhifadhia mazao kama mahindi, maharage na mbaazi ambayo anayauza mikoa ya Arusha, Dar es Salaam na Mwanza, ambazo zote zimefunikwa na tope, ni miongoni mwa waathirika hao.
Mwananchi ilishuhudia mfanyabiashara huyo akishirikiana na vijana wake kuondoa tope na kutoa baadhi ya magunia ya mazao mbalimbali.
Alisema mwaka jana alikopa Sh30 milioni benki kuendeleza biashara yake na sasa hajui atalipa vipi marejesho ya mkopo huo kutokana na mazao mengi kuharibika.
“Ofisi hii ina gunia zaidi ya 1,300 za mazao hayo na siwezi kujua gharama yake, kwani kila zao lina thamani yake na hasa maharage, kuna ambayo thamani yake ni kubwa, hapa nimeanza katika ofisi hii moja kwa leo, tukiweza kumaliza kesho tutaendelea na kwenye ofisi nyingine, mpaka sasa hatujaweza kufungua zote, tuna ofisi sita zote zimeingia tope na maji na kila ofisi tunashindwa kukadiria, mzigo ni mkubwa sana,” alisema.
“Ombi letu kwa Serikali na tunamuomba mama Samia atuangalie kwa jicho namba moja, siyo kwa jicho la pili, tuna mikopo huku na tukiachwa tunafia mbali,” alisema.
Mfanyabiashara huyo alisema “hali ya mahindi ni mbaya kama unavyoona, magunia yameloana, mahindi yameloana, maharage mengine ni ya kumwaga, si ya kupigia hesabu, kwani yameharibika sana.”
Mwenzake, Aziza Abdallah, muuzaji wa jumla wa mchele, alisema amepata hasara ya zaidi ya Sh15 milioni kutokana na mchele aliokopa kwa mfanyabiashara mkoani Shinyanga ambaye huwa anampatia kwa ‘mali kauli.’
“Nimeokoa mali kidogo sana, magunia mengi yameharibika, kuna mwingine nimeuanika sijui kama utafaa. Nina maduka mawili, ila moja matope yalilizingira tu bila kuingia ndani ila changamoto katika duka lililoharibiwa huwa natumiwa mchele kutoka Shinyanga na nikishauza ndiyo nalipa deni,” alisema.
Aziza alisema “anayenidai alinipigia simu kudai hela zake, nikamwambia wewe huangalii TV? Akaniongelesha Kisukuma ‘mayo mayo’ (mama mama), sasa nikamwambia ongea Kiswahili mimi hali yangu hii, wewe unataka hela?”
“Rais Samia ninachomwambia anisaidie deni kwa sababu nyumbani sijaathirika chochote, ni tope tu limezunguka lakini anisaidie kunipa hela niwape wakulima (Shinyanga), ninaomba Mwenyezi Mungu amjalie atuonee huruma sisi,” alisema Aziza.
Mfanyabiashara huyo alisema analea watoto watatu wa mke wa kaka yake ambaye alishafariki dunia, hivyo hana namna ya kuendelea kuwalea kwa kuwa alikuwa anategemea biashara hiyo.
“Mimi nimefiwa na wifi yangu, aliniachia watoto watatu nawalea na mmoja yuko kidato cha pili, mwingine amemaliza kidato cha nne na mwingine nilimuozesha na nikampa duka ili auze alishe familia yake, ana mke mjamzito na sijui namsaidiaje,” alisema.
Naye Justce Kalaghe ambaye ni mfanyabiashara wa duka la pembejeo, alisema hadi sasa amepata hasara ya zaidi ya Sh5 milioni na bidhaa nyingi zimesombwa na mafuriko, chache zilizobaki zimeharibiwa kwa kufunikwa na tope.
Kilio pia kiko kwa Victoria Kimambo, mkazi wa Mji wa Katesh, aliyesema ombi lake Rais Samia awasaidie kupata mitaji kwani mitumba aliyokuwa anauza imesombwa na matope na mtaji wake ukaishia hapo.
“Nilikuwa nauza nguo za mtumba, ila maafa haya yamechukua mitaji yetu yote, hivyo tunamuomba Rais Samia atusaidie, kwani tumepoteza kila kitu na hatuna pa kuanzia,” alisema
Kilio kama hicho kilitolewa na waathirika waliopo kwenye kambi maalumu baada ya makazi yao kuharibika, ambao nao walimwomba mkuu huyo wa nchi awasaidie kupata makazi.
Flaviana Gabriel, kutoka Kijiji cha Jorodon ambaye nyumba yake imebomolewa, amemuomba Rais Samia na Serikali anayoiongoza iwajengee nyumba, kwani kwa sasa yeye na watoto wake wanne hawajui wataelekea wapi wakitoka kambini.
“Tope liliingia kijijini kwetu na mawe makubwa na miti na kubomoa nyumba yetu, hatuna mahali pa kuishi kwa sasa, tunalala hapa Shule ya Msingi Katesh,” alisema.
Kwa upande wake mkazi wa Katesh, John Mathias naye aliiomba Serikali iwasaidie kujenga nyumba, kwani hivi sasa yeye na familia yake ya watu 15 hawana makazi tena na hawajui wataelekea wapi, kwa kuwa hata nyumba yake ya kupangisha yenye vyumba saba pia imebomoka.
“Nilikuwa na nyumba ya kuishi pamoja na nyumba ya wapangaji yenye vyumba saba, ila janga hili limenisababishia umasikini, namuomba Rais Samia atuangalie wanyonge,” alisema.
Shughuli zaanza kurejea
Tofauti na ilivyokuwa katika siku tatu za mwanzo, jana huduma mbalimbali, ikiwemo biashara za maduka ziliendelea kurejea katika hali yake ya kawaida, ambapo wengi walianza kufungua maduka na wengine wakiendelea kufanya usafi kuondoa tope lililozingira maduka yao ili waweze kufungua.
Wengine ambao maduka yao hayakuwa yameathiriwa na matope walifanya usafi kwa kuondoa matope yaliyokuwa yameyazingira ili waweze kufungua, huku ambao maduka yao yameharibiwa au kujaa tope ndani, wakichambua bidhaa ambazo zimesalia ili wazitafutie wateja.
Katika baadhi ya maeneo, miundombinu ya barabara imeendelea kusafishwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa alisema Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) zimeunganisha nguvu kuhakikisha maeneo yaliyoharibika yanarejea katika hali ya kawaida.
Mikakati ya Serikali
Jana, Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi alisema Serikali inafanya tathmini ya uharibifu wa miundombinu ya eneo la Katesh na vijiji vinne kuangalia uharibifu wa barabara, mfumo wa maji na umeme.
“Hayo ni maporomoko ya tope, mawe na miti, kwa hiyo yameharibu banio la maji yaliyokuwa yakitoka Mlima Hanang, hivyo Wizara ya Maji inachimba visima ili watu wapate maji,” alisema.
Katika hilo la maji, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama alisema kutokana na Mlima Hanang kuwa na chanzo cha maji ambacho nacho kimeharibika, wameanza kusambaza maji kwa maboza.
Mhagama alisema Wizara ya Maji imeanza kusambaza huduma hiyo muhimu katika kambi maalumu ambazo zina waathirika wa janga hilo na kwenye vituo vya afya na zahanati ili kuepuka magonjwa ya mlipuko yanayoweza kujitokeza.
Kuhusu uharibifu wa nyumba, Matinyi alisema hadi sasa kuna kaya 1,150 zenye wananchi zaidi ya 5,600 waliopoteza makazi.
“Kuna nyumba zimevunjika, nyingine zimesombwa na matope na nyingine zimeingia matope, hivyo hao wamehifadhiwa na ndugu zao.”
Alipoulizwa kama kuna mkakati wa Serikali wa kuwajengea nyumba, alisema ni mapema mno kuzungumzia.
“Kwa sasa Serikali inakwenda kufanya tathmini ya kina kwa kushirikisha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Serikali za mitaa kwa kutumia ripoti za Sensa ya Watu na Makazi iliyoangalia makazi na wenye makazi,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu wananchi waliohifadhiwa kwenye kambi za muda, alisema kamati ya maafa ya mkoa huo itatafuta suluhisho la makazi, akieleza hadi sasa wananchi 190 wamehifadhiwa kwenye kambi hizo.
Alisema pia Serikali inahakikisha janga kama hilo linadhibitiwa na hata likitokea tena kuwe na mikakati ya kukabiliana nalo na shughuli za uokoaji zinaendelea zikihusisha askari 1,285, wakiwamo mgambo, askari wa hifadhi, Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Magereza na Polisi.
Matinyi alisema miili mitano kati ya waliofariki ilikuwa imeharibika “kiasi kwamba itahitaji Mkemia Mkuu wa Serikali kufanya vipimo vya DNA ili kuwatambua ndugu.”
Wazee wa mila wakutana
Jana, viongozi wa mila katika eneo la Katesh wakiongozwa na mwenyekiti wa mila wilayani humo walikutana na uongozi wa kamati ya maafa kitaifa na kufanya maombi maalumu.
Katika kikao hicho, Mwenyekiti wa mila wilayani Hanang, Mathayo Sixtus alisema wanaamini Mungu ni mwaminifu na wanamuomba aepushe janga hilo lisijirudie tena.
Ujumbe wa Bunge, TEC
Viongozi mbalimbali wa Serikali waliendelea kutembelea maeneo hayo, akiwemo Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ambaye alisema pamoja na mambo mengine kazi ya Bunge ni kuishauri Serikali na changamoto zilizojitokeza katika mchakato wa uokoaji zitasaidia kujipanga zaidi kama Taifa. Alizipongeza timu zote za uokoaji chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na wadau wengine walioshiriki mchakato huo.
“Changamoto zilizojitokeza nyingine tumeziona na nyingine tutaenda kuziona ili yale tutakayojifunza kutokana na hili yatusaidie huko mbele, tunamuomba Mwenyezi Mungu atuepushe huko mbele, lakini yale yatakayoendelea kujitokeza lakini tuwe na utayari kama taifa.
Wakati huohuo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Mkuu, Gervas Nyaisonga alikutana na waandishi wa habari jijini Mbeya na kutuma salamu za pole kwa Rais Samia na Taifa kwa ujumla kufuatia tukio hilo.
Alisema tayari Baraza hilo kupitia kitengo cha maafa linaendelea kuratibu mipango ya kuwasilisha msaada wa vitu mbalimbali kwa waathirika.