Connect with us

Kitaifa

‘Maboresho bandari yazaa matunda’

Dar es Salaam. Mradi wa mradi wa maboresho katika Bandari ya Dar es Salaam umeanza kuleta matokeo chanya ikiwamo kuongezeka idadi ya shehena ya makasha kutoka 80,000 hadi 100,000 yanayohudumiwa kwa mwezi, mamlaka zimesema.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumanne Desemba 5, 2023 na Wizara ya Uchukuzi, imesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ili kurahisisha usafirishaji na shughuli za uchukuzi.

Taarifa hiyo ambayo inazungumzia juu ya kupokewa kwa meli ya makasha ya Kampuni ya Emirates Shipping Lines (ESL), iliyoanza kufanya safari za moja kwa moja kutoka China hadi Tanzania, imemnukuu Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile akisema ujio wa meli hiyo utapunguza gharama za usafirishaji.

“Ujio wa meli hizi utapunguza gharama za usafirishaji kwani mzigo utapakiwa China na kuja moja kwa moja Tanzania, hivyo kupunguza gharama za usafirishaji wa shehena hususani makasha. Huu ni mwendelezo wa matokeo chanya ya maboresho yanayofanyika katika bandari ya Dar es Salaam,” amesema Kihenzile.

Hata hivyo, Waziri Kihenzile ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kuhakikisha meli zote zinazotoa huduma kupitia bandari mbalimbali nchini, zinapewa huduma stahiki na zenye viwango vinavyohitajika.

Kwa upande wake Mrisho Mrisho, ambaye ni Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, amesema kuwa baada ya maboresho makubwa yaliyohusisha ujenzi wa gati na uongezaji wa kina katika lango la kuingilia bandarini hapo, kumewezesha kuongezeka kwa idadi ya mizigo na magari yanayohudumiwa kwa wakati mmoja.

Mrisho amesema bandari hiyo imejipanga kuhakikisha inatumia vizuri mitambo iliyonayo kutoa huduma kwa uharaka na ufanisi hasa katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka.

Mkurugenzi Mtendaji wa ESL, Kanda ya Afrika Mashariki, Nithin Nath amesema kuanza kutoa huduma za kusafirisha mizigo moja kwa moja kutoka China hadi Tanzania, kutapunguza muda wa safari wa usafirishaji kutoka siku 45 hadi 22.

Amesema ESL imeweka mikakati ya kuhakikisha inaanzisha safari za kusafirisha makasha ya mizigo kutoka China kwenda bandari za Tanga, Mtwara na Zanzibar.

Bandari ya Dar es Salaam inafanya maboresho katika maeneo mbalimbali ili kuleta ufanisi wa utoaji wa huduma bora pamoja na kuboresha eneo la forodha linalotumiwa na wasafiri wanaokwenda Zanzibar na kurudi Dar es Salaam.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi