Makala
Nini sababu ya mahusiano na ndoa za wengi kuvunjika?
Baadhi ya tafiti zilizofanywa kwenye jamii na maeneo tofauti zinaonyesha sababu zilizo katika makundi mawili zinazoweza kusababisha ndoa nyingi kuvunjika. Kundi la kwanza ni sababu zinazoanzia kabla ya kuanza kuishi pamoja na zinazohusika na mchakato mzima wa maisha ya mtu.
Sababu hizi zinaweza kupelekea moja kwa moja wanandoa kutengana au zinaweza pia kuchangia pamoja na sababu za kundi la pili kuongeza msukumo wa kutengana. Sababu hizi za kundi la kwanza ni kama vile;
• Umri wakati wa kuoa au kuolewa
• Kama mliishi pamoja kabla ya kuoana
• Kiwango cha elimu baina ya wapenzi wawili
• Masuala ya ukabila na tamaduni
• Muda mliokaa kwenye mahusiano
• Mahudhurio katika nyumba za ibada (Hii hutegemea mmoja anavyoichukulia imani)
• Ajira (hususan ya mke)
• Kipato
• Kama mmoja amewahi kuoa au kuolewa tena
• Kama wazazi wamewahi kutengana
Umri wakati wa kuoa au kuolewa
Tafiti zinaonyesha kama wanandoa walioana mmoja wao au wote wakiwa hawajapevuka vema kiumri, mabadiliko ya maisha na majukumu katika ndoa yanaweza kuwa mzigo mkubwa kwao na mmoja kati yao kuhisi kuwa hakufanya chaguo jema kuingia kwenye ndoa na hivyo kujikuta akitengeneza mazingira ya kutoka kirahisi.
Mliishi pamoja kabla ya kuoana?
Tafiti zinaonyesha wanandoa wengi waliowahi kuishi pamoja kwa muda fulani kabla ya kuoana rasmi wana nafasi kubwa zaidi ya kutengana ukilinganisha na wale ambao hawajaishi pamoja kabisa.
Hii inatokana na kwamba thamani, kiu na raha ya kuanza kuishi pamoja kama mke na mume haipo kutokana na ukweli kwamba watu hawa wameshakuwa pamoja muda mrefu na ni kama wanaendeleza kile kile walichokianza tayari.
Kama mlikuwa na misuguano na tofauti, basi hutegemei kule kurasimisha mahusiano yenu kwa kile kinachoitwa ndoa ndiko kutabadilisha tofauti hizo, hata raha ya fungate huwa haionekani ipasavyo kwa sababu hakuna jipya linalotarajiwa.
Bahati mbaya mfumo wa kuishi pamoja ndio umechukua nafasi kwa jamii ya vijana wengi sasa, hususan wa mijini na wale waliosoma na wenye ajira zao. Wakati wazazi wakidhani binti yao au kijana wao anaishi mwenyewe, kumbe walishaamua kuhamia kwa mmoja na kuishi pamoja kitambo tu.
Wanapokuja kuamua kuoana basi siku chache tu binti anajifanya kwenda kwao au kwa ndugu zake kama vile ndio kwanza anamjua kijana, kumbe walishakuwa mke na mume kwa mlango wa nyuma. Huwa najiuliza, hapa mnamdanganya nani, wakati kiuhalisia mnapanda mbegu ya uharibifu wenu nyie wenyewe?
Kiwango cha elimu baina ya wapenzi
Tafiti zinaonyesha wanandoa wengi wasio na elimu au walio na elimu duni wako kwenye nafasi ya kutengana zaidi kuliko wale wenye elimu. Hii inatokana na sababu tofauti, ikiwepo ujuzi wa kuishughulikia migogoro yao na uwezo wa kutafuta msaada kutoka kwa jamii inayowazunguka na ushauri pia.
Inasemekana pia wazazi walioelimika huweza kuziangalia na kuzitathmini athari za kutengana kwao zitakavyowagusa watoto na wao pia, na hii huwafanya kufikiria mara mbili kabla ya kuamua kutengana.
Bahati mbaya tafiti nyingine za miaka ya karibuni zinaonyesha kuwa hata wanandoa walio na elimu huweza kuachana kirahisi kutokana na ufahamu walionao juu ya mambo ya sheria, haki za binadamu, haki za wanawake na mgawanyo sawa wa majukumu ya wanandoa n.k.
Tofauti kubwa ya elimu baina ya wanandoa (mke na mume) yaweza kuwaingiza kwenye migogoro na baadaye kuwatenganisha, hususan katika namna wanavyoyaangalia na kuyatafsiri mambo.
Muda mliokaa kwenye uhusiano
Muda mliokaa kwenye uhusiano kabla hamjaamua kuingia kwenye ndoa umeonekana kuwa muhimu katika kutengeneza kudumu kwenu au kutengana. Wanandoa ambao wameingia kwenye ndoa haraka pasipo muda wa kutosha wa kufahamiana wamekuwa na tabia ya kuingia kwenye misuguano mingi ambayo imewapelekea kutengana.
Kutokana na muda mdogo wa urafiki na uchumba, wengi wanakuja kushangaa baadhi ya tabia wanazokuja kuziona kwenye ndoa na kulalamika kuwa mpenzi mwingine amebadilika siku hizi, wakati ukweli ni kwamba hajabadilika, bali amekuwa kawa kama alivyokuwa awali.
Siku hizi mahusiano mengi hayapitii kwenye urafiki, bali yanaanzia moja kwa moja kwenye uchumba na hii ni hatari zaidi. Wengi wakishapendana tu, hawana muda wa kusubiri, kuwa marafiki na kufahamiana.
Wengi nilioongea nao wamekiri kuwa kama wangeendelea kidogo kuhusiana na kuwajua wapenzi wao kwa kitambo zaidi basi wasingeoana nao. Ya nini kukimbilia kwa kasi kuingia sehemu ambayo unajua utatoka kwa kasi zaidi ya ile uliyoingilia?