Connect with us

Kitaifa

Rais Samia azindua mradi nishati safi ya kupikia Afrika

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, ametumia dakika 15 kushawishi mataifa ya Afrika kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mradi wa nishati safi ya kupikia kwa wanawake Afrika (AWCCSP), inayokusudia mageuzi na kumkomboa mwanamke.

Tukio hilo limefanyika leo Desemba 2, 2023 wakati wa uzinduzi wa mradi huo ikiwa ni sehemu ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) unaoendelea huko Dubai.

Wakati wa uzinduzi, washiriki wote walisimama huku wakitizama video iliyohesabu namba kutoka tisa hadi moja, kisha kuonekana jiko lenye gesi na herudi za AWCCSP, ambazo ni ufupisho wa jina la mradi huo.

Rais Samia amezindua mradi huo ngazi ya Afrika baada ya kuanza utekelezaji wa Dira ya miaka 10, inayokusudia kuongeza matumizi ya nishati safi za kupikia kwa asilimia 80 ya watanzania wote.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba alikuwa mratibu wa tukio hilo lililotanguliwa na makala maalumu iliyoonyesha athari za kiafya na kielimu kwa wanawake, zinazotokana na matumizi nay a mkaa na kuni kama vyanzo vya nishati ya kupikia.

“Tunazindua mradi huu COP28 ili kuonyesha uwajibikaji wetu licha ya kuwa na uchangiaji mdogo wa kaboni duniani, suala la nishati safi ni sehemu ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi na usalama wa mwanamke,” amesema rais Samia akifafanua;

“Wanawake wanaathirika kiafya wakati wa kupika kwa kuni na mkaa, watoto wa kike wanapoteza muda mwingi kutafuta kuni na hivyo kukosa muda wa kutosha katika masomo. Karibu asilimia 80 ya mataifa ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, hutumia nishati chafuzi.”

Rais Samia amesema mradi huo unashawishi mageuzi ya kisera kwa mataifa hayo yanayokusudia kuimarisha mafunzo kwa akina mama kuhusu teknolojia za matumizi ya nishati safi.

“Mimi najitolea kuwa mstari wa mbele katika kampeni hii, nimefurahi kuona wafadhili wa miradi ya nishati safi ya kupikia wako hapa. Suala hili ni hatua, linahitaji mageuzi ya kisera na motisha kushawishi teknolojia kwenye matumizi ya nishati safi, pia ushirikiano wa sekta binafsi,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amehitimisha kwa pendekezo la kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa wa kimataifa kuhusu nishati safi ya kupikia kwa ajili ya kuweka msingi utakaosaidia mafanikio ya mradi huo. Amesema maoni yaliyotolewa na wadau hao yatatumika kama mwongozo kwenye mkutano huo.

Baada ya kumaliza hotuba yake, washiriki kutoka mataifa mbalimbali wameboresha na kushawishi utekelezaji wa mradi huo huku wakiahidi kutoa ushirikiano ili kupunguza uzalishaji wa kaboni duniani, vifo vitokanavyo na hewa chafu ikiwamo kuni na kukuza elimu kwa watoto hususani wa kike.

Kauli hiyo inatolewa wakati ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka jana ikionyesha idadi ya watu bilioni 2.4 duniani, sawa na robo ya watu wake, hutegemea nishati chafuzi kwa ajili ya kupikia, jambo ambalo limesababisha hekta milioni 3.9 za misitu, kupotea kila mwaka barani Afrika.

Ripoti hiyo imefanunua kuwa kutokana na matumizi ya nishati chafu ikiwamo kuni na  mkaa, watu milioni 6.7 hufariki kila mwaka duniani, kutokana na uzalishaji wa hewa chafu wakiwamo milioni 3.2 wanaopoteza maisha kutokana na hewa chafu inayozalishwa katika kaya kwa njia za kuni na mkaa.

Ripoti hiyo inasema bila kuwa na utekelezaji wa sera thabiti, watu bilioni 2.1 wanakadiriwa kuendelea kukosa huduma ya nishati safi na teknolojia ifikapo mwaka 2030.

Inashauri hatua za haraka kwa mataifa ya Kusini mwa Jangwa la Sahara.

WHO inatafsiri nishati safi na teknolojia kwa afya ni pamoja na umeme-jua, gesi asilia, gesi ya kimiminika ya petroli (LPG), pamoja na majiko ya biomasi yanayokidhi malengo ya utoaji wa hewa safi katika miongozo ya shirika hilo.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi