Kitaifa

Huduma za kidijitali Tanzania kuunganisha Afrika na dunia

Takwimu zilizopo na imani ya wengi inaonyesha kuwa dijitali ndiyo silaha kubwa ya uchumi hivi sasa ambayo ikitumiwa vizuri inaweza kusaidia kwa kiwango kikubwa kukomboa watu katika wimbi la umasikini na kuinua kipato zaidi.

Ukizungumza na viongozi wa Serikali sasa wanaohudumu katika sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano, kauli yao ni kuwa wanakusudia kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha dijitali barani Afrika.

Kwa kuwa kitovu cha dijitali maana yake ni kuwa inakuwa nchi muhimu katika huduma za kidijitali, ikisaidia mataifa mengine kuunganishwa na kupata suluhu mbalimbali kutokana na uwekezaji na uwezeshaji unaokuwa unapatikana nchini.

Kuhusu uwezo wa kufanikisha hilo na kwa muda gani, bado ni kitendawili, lakini Mkurugenzi wa Mkongo wa Taifa Tanzania, Abdul Mombokaleo anaelezea namna Tanzania inavyojipanga kuwa kitovu cha dijitali barani Afrika, akisema mataifa yasiyo na bahari yanaweza kuitumia Tanzania kama njia ya kuufikia mkongo wa chini ya maji.

“Kwa sasa tunahudumia nchi zote za Afrika Mashariki zisizo na bahari na hata Kenya inatutumia kama njia ya dharura, teknolojia ya dijitali imeonyesha matokeo makubwa katika sekta ya fedha na ukusanyaji mapato ya Serikali, hili tunaweza kuliambukiza kwa nchi nyingine,” anasema Mombakaleo.

Mombakaleo alitoa ujumbe kama huohuo Novemba 14, mwaka huu wakati wa mjadala wa jukwaa la mawaziri wa mawasiliano barani Afrika, ambapo alielezea mipango ya kuongeza zaidi mtandao wa Mkongo wa Taifa katika mataifa mengine.

Wakati huohuo, Meneja mauzo kimataifa wa Tigo Business, Yvonne Mashuda yeye anasema kupitia uwekezaji wao wa Mkongo wa majini wanaunganisha nchi jirani za Tanzania zisizo na bahari, lakini pia kuunganisha mataifa tofauti ndani ya Afrika kupitia mtandao wao.

“Tigo Business si tu kwa ajili ya Tanzania, bali ni kwa bara zima la Afrika na ulimwengu kwa jumla, kwani mbali na huduma za simu, inatoa huduma ya kuhifadhi data. Kwa upande wa mkongo tunahudumia nchi zote za Afrika Mashariki na tunajipanga zaidi kupanua huduma zetu kwenda Congo na Msumbiji,” alisema Mashunda.

Inaelezwa kuwa endapo Afrika itaweza kusambaza mtandao wa 5G katika maeneo yake yote mpaka 2030 itakuza pato lake kwa zaidi ya Dola bilioni 26 ambazo ni sawa na Sh65.13 trilioni.

Katibu Mkuu wa umoja wa watoa huduma za simu Afrika, John Omo anasema Afrika ilishindwa kuchangamkia fursa nyingi za mapinduzi ya kiuchumi huko nyuma, lakini sasa inapaswa kushinda katika fursa ya mapinduzi ya kidijitali, kwa kuwa ina uwezo wa kufanya hivyo.

“Maeneo ya kipaumbele kwa bara letu yanapaswa kuwa matumizi ya akili bandia na mtandao wa 5G ambavyo vinaweza kusaidia kufanikisha shughuli nyingi kwa ufanisi mkubwa. Tupo katika ulimwengu ambao unahitaji taarifa na data za kipindi mwafaka ili kukuza uchumi, hivyo tunapaswa kwenda na kasi hiyo,” anasema.

Aidha, katika hotuba ya Bajeti ya mwaka 2023/2024, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye naye alielezea mpango wa Serikali kuendelea kutanua mtandao wa Mkongo wa Taifa na kuziunganisha nchi jirani.

“Ukamilishaji wa shughuli za ujenzi wa kilomita 1,742 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa kuratibu ujenzi wa kilomita 60 za Mkongo wa mawasiliano kupitia Ziwa Tanganyika kuunganisha Tanzania na Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, kuratibu ujenzi wa kilomita mpya 1,600 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano,” alisema Nape akielezea mipango ya wizara hiyo mwaka huu.

Aliongeza kuwa vilevile Serikali inakusudia kufikisha huduma ya Mkongo kwenye wilaya 14, na kujenga mikongo ya kuunganisha watumiaji ambao ni taasisi 50 kwenye maeneo ya uwekezaji, huduma za afya na elimu ili kuharakisha Taifa kushiriki katika uchumi wa kidijitali.

Katika jukwaa la mawaziri wa Afrika ambalo Nnauye alishiriki nchini Afrika Kusini, alisema miundombinu pekee haitoshi kuwaunganisha watu, hivyo Serikali zinapaswa kuwa na mipango ya kupunguza gharama za vifaa vya kidijitali, kwani kuwa na miundombinu tu haitoshi kama watu hawawezi kuufikia ulimwengu wa kidijitali.

Mkurugenzi wa mawasiliano wa Vodacom, Zuwena Furah anasema Serikali za Afrika kama zinapaswa kutimiza mpango wa kuwaunganishwa watu wake hazina budi kuongeza urahisi wa watu wake kuwa na vifaa kidijitali kwa kupunguza gharama.

Anasema mataifa ya Afrika yanaweza kufanya hivyo kwa kupunguza kodi za uingizaji wa vifaa hivyo au kuvutia uwekezaji wa viwanda vya kutengeneza vifaa hivyo nchini mwao ili kupunguza gharama.

“Kwa mfano Tanzania asilimia 27 tu ndiyo wanatumia simu janja ambazo gharama zake hapa nchini zinaanzia Dola za Marekani 60 (Sh150,000), si wengi wanaweza kumudu gharama hizo, pengine bei ikipungua wengi watanunua vifaa hivyo muhimu vya kuwaunganisha kidijitali,” anasema Furah.

Furah anasema kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa Tanzania inapaswa kuondolewa tena ili kupunguza gharama za vifaa vya kidijitali. “Serikali iliondoa ikarudisha baada ya mwaka mmoja, nafikri inapaswa kuondoa kwa miaka kadhaa ili kuona matokeo, mwaka mmoja hautoshi kupima athari, kama ni kupima basi iwe baada ya miaka kadhaa ndipo unapata uhalisia,” alisema.

Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa Zimbabwe. Tatenda Mavetera anasema ili kufikia manufaa ya kidijitali, mataifa ya Afrika yanapaswa kwa pamoja kuunganisha nguvu kuunganisha miundombinu ya kidijitali ili kunufaisha watu wake.

Naye naibu Waziri wa Tehama wa Afrika Kusini Philly Maphulane aliunga mkono hoja ya Mavetera, akisema kwa pamoja Afrika inapaswa kukuza ubunifu wa kidijitali kwa kuhakikisha kuna kuwa na miundombinu rafiki kwa wabunifu.

“Hata msemo wa Afrika unasema ukitaka kufika haraka nenda peke yako, lakini ukitaka kufika mbali nenda na wenzako,” alisema Maphulane.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi