Kitaifa
Tanzania yaanika mambo manne inayosimamia COP28
Dar es Salaam. Tanzania imetaja mambo manne kuwa ndiyo msimamo wake katika mkutano wa COP28 ambayo ni fedha za ufadhili zizingatie athari za mabadiliko ya tabianchi, mfuko wa pamoja wa majanga na maafa, matumizi ya nishati safi na jumuishi na mjadala wa jinsia unaompa mwanamke kipaumbele.
Mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC – COP28) ulioanza jana Alhamisi, Novemba 30,2023 na utafikia kilele Desemba 12, 2023.
Rais wa Samia Suluhu Hassan na wadau mbalimbali kutoka nchini, watashiriki katika mkutano huo unaoendelea huko Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), ambapo washiriki zaidi ya 70,000 kutoka nchi takribani 190 wanakutana kuangazia masuala ya mabadiliko ya tabianchi duniani.
Taarifa iliyotolewa katika Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, imesema: “Tanzania inaunga mkono hoja ya kuongeza fedha za ufadhili kwa kuzingatia athari zinazozidi kuongezeka kwa sasa na kuhakikisha ahadi ya nchi zilizoendelea kutoa Dola 100 bilioni (Sh250 trilioni) kila mwaka kwa nchi zinazoendelea ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, zinatimizwa.”
Jambo jingine ni “Kuhakikisha mkutano unaridhia uanzishwaji wa mfuko wa kupambana na majanga na maafa, kuhakikisha juhudi za kuelekea matumizi ya nishati safi zinakuwa jumuishi na mjadala wa masuala ya jinsia unazingatia maadili ya kitaifa na kijamii na wanawake wanapewa kipaumbele.”
Mambo muhimu katika mkutano huo
Kaulimbiu ya mkutano huo ni “Ungana – Tenda – Wasilisha” kitaifa kaulimbiu ni “Kuimarisha Kilimo Himilivu na Uchumi wa Bluu katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi.”
Taarifa ya Ikulu imesema lengo la kaulimbiu hiyo ni kutoa msisitizo katika matumizi ya teknolojia na mbinu bora zinazozingatia changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ili kuongeza tija katika uzalishaji, mnyororo wa thamani wa mazao na masoko.
Wakuu wa nchi na Serikali wanachama wa UNFCCC watahutubia katika mkutano huo leo, ambapo Rais Samia atakuwa mzungumzaji wa 11 miongoni mwa wakuu wa nchi na Serikali takriban 160 wanaoshiriki mkutano huo.
Sambamba na kuhutubia mkutano huo, Tanzania imeandaa na itakuwa mwenyeji wa mikutano mikuu mitatu ya pembezoni (High-Level Side Events), inayohusu nishati safi ya Kupikia, kilimo endelevu, na uchumi wa buluu.
Katika mkutano unaohusu nishati safi ya kupikia, Rais Samia ataongoza viongozi wenzake kutoka nchi mbalimbali duniani na taasisi za kimataifa kuzindua Programu ya Kuwakomboa Wanawake wa Afrika Kupitia Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (African Women Clean Cooking Support Programme – AWCCSP).
Programu hiyo inalenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kukabiliana na changamoto za afya, mazingira, uchumi na kijamii zinazoathiri zaidi wanawake na watoto.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo wanawake hutumia muda mrefu kutafuta kuni hivyo programu hiyo itawasaidia kupata muda wa kutosha kushiriki kwenye shughuli za maendeleo.
Rais Samia atashiriki katika mikutano ya uwili na viongozi wa Serikali za nchi mbalimbali pamoja na mashirika ya kimataifa kwa lengo la kuimarisha mahusiano baina ya Tanzania na nchi hizo pamoja na mashirika husika.
Utiaji saini hati nne
Rais atashuhudia uwekaji saini hati nne za makubaliano baina ya Tanzania na Serikali ya UAE kuhusu ajira, ushirikiano baina ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dk Salim Ahmed Salim na Chuo cha Diplomasia cha Dk Anwar Gargash cha nchini humo.
Nyingine ni inayohusu ushirikiano katika masuala ya usalama na mapambano dhidi ya ugaidi na ushirikiano katika sekta za elimu, sayansi na ufundi.
Katika mkutano huo, ujumbe wa Tanzania utashirikisha mawaziri, makatibu wakuu, mabalozi, viongozi na watalaamu kutoka wizara za kisekta, idara za Serikali, mashirika ya umma, vyuo vikuu, sekta binafsi, asasi za kiraia, vijana na wanahabari kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.