Connect with us

Kitaifa

COP28 kuanza leo, wadau wataja matarajio

“Tunapoelekea kwenye COP28, hatuna budi kuinuka kama sauti ya Afrika kuhusu uanzishwaji wa mfuko maalumu kwa ajili ya Afrika. Wanapaswa kusema ni asilimia ngapi ya ahadi zao Afrika na si vinginevyo,” alisema Rais Samia katika mkutano huo.

Akizungumza na Mwananchi, Profesa Pius Yanda katika Kituo cha Mafunzo ya Mabadiliko ya Tabianchi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema nchi zilizoendelea zinahitaji kutoa fedha kutokana na uchafuzi zilioufanya na zimekubali kufanya hivyo.

“Nchi za Afrika ndizo zinazoathirika zaidi, licha ya mchango wake kuwa mdogo kwenye uchafuzi. Sababu kubwa ni mapinduzi ya viwanda na nchi hizo zinakiri na ziliahidi kutoa Dola za Marekani bilioni 100 (Sh2.5 trilioni) kila mwaka, lakini hazikufanya hivyo,” alisema.

Profesa Yanda alisema jambo litakalowafanya wawajibike ni diplomasia, ndiyo sababu ya uwapo wa mkutano mkubwa wa nchi wanachama na kuongeza kuwa hii ni miongoni mwa hoja muhimu ambazo nchi inapaswa kuzichukua kama ajenda.

Alisema, “hivi sasa kuna madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi kama mafuriko na ukame, ambavyo vinahitaji kufidiwa na fedha hizo, lakini tunahitaji kufanya kilimo kinachokabiliana na mabadiliko ya tabianchi, mambo ambayo yanahitaji fedha.”

Alisema ili kukifikia kilimo hicho, zinahitajika teknolojia na wataalamu waliowezeshwa kuzitumia. Haya yote alisema yana gharama.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande alitilia shaka iwapo dunia iko kwenye njia sahihi ya kukabiliana na janga hilo linaloendelea kuathiri maisha ya mamilioni ya watu duniani, akitoa wito kwa mataifa tajiri kuwajibika kwa kutoa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Chande alisema hayo kwenye kongamano la kimataifa la uwazi na uwajibikaji 2023 (ITAC 2023).

Alihoji, “je, tuko katika mwelekeo sahihi, hasa katika kutoa ahadi za fedha ambazo nchi huweka ili kufikia malengo yake. Ahadi iliyotolewa tangu COP15 mpaka sasa fedha zilizotoka ni robo tu ya Dola za Marekani 100 bilioni.”

Akizungumza wakati wa mkutano huo ulioandaliwa na taasisi ya Wajibu, Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlotta Macias alibainisha kuwa uwajibikaji ni muhimu kwa hatua zozote za maana kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

“Kwa sababu inasaidia kuhakikisha juhudi za kukabiliana na changamoto ya mabadiliko haya na kuhakikisha juhudi zinafanikiwa, unapatikana usawa na kuhakikisha kuwa mataifa na viongozi wanawajibika kwa ahadi walizotoa,” alisema.

Mwelekeo sahihi

Mjumbe wa bodi ya muungano wa asasi za kiraia na vyama vya wafanyakazi, Stephen Msechu alisema anatambua umuhimu wa COP28 na kushauri nchi itumie fursa hiyo kwa manufaa ya pande zote.

“…tunatakiwa kutumia jukwaa hili muhimu kujadiliana na kuingia makubaliano yenye manufaa kwa pande mbili, tukitambua hakuna mtu atakayeleta pesa bure bila yeye kunufaika,” alisema, akitoa mfano wa biashara ya kaboni.

Msechu, ambaye pia ni mwanasheria, alisema nchi haiwezi kukaa pembeni na kukataa biashara hiyo, isipokuwa inatakiwa kuhakikisha mikataba mizuri inaingiwa na fedha zinakwenda kweli kutatua changamoto za wananchi wanaoathirika zaidi.

Mdau kutoka taasisi isiyo ya kiserikali ya Power Shift Africa, Amos Wemanya pia alisema Afrika inahitaji haraka fedha kwa ajili ya kukabiliana na suala hilo.

Inakadiriwa kwa Bara la Afrika pekee, gharama za kukabiliana na hali hiyo zinaweza kufikia Dola 50 bilioni (Sh1.25 trilioni) kwa mwaka ifikapo 2050.

“Gharama za kuhama kutoka matumizi ya nishati chafu ni Dola 125 bilioni kwa mwaka kati ya 2026 na 2030,” alisema Wemanya katika mjadala ulioandaliwa na chombo cha habari za mazingira, sayansi za afya na kilimo (Mesha) na ofisi ya Afrika ya IDRC Mashariki na Kusini.

Alisema nchi tajiri lazima zitoe fedha kwa kuzingatia athari kubwa zilizosababisha kihistoria na fedha hizo ziwezeshe nchi za Kiafrika katika urekebishaji unaohitajika na kugharimia mahitaji yote ya hasara na uharibifu unaojitokeza.

Katika mjadala huo, mwanasayansi wa hali ya hewa, Patricia Nying’uro alisema wanatarajia COP28 itakuja na mapendekezo ya kwanza ya kidunia ambayo yatatoa mwongozo kwenye utoaji wa mapema wa taarifa za hali ya hewa.

Mdau kutoka Chama cha Wanaharakati wa Mazingira (Leat), Clay Mwaifwani anashauri Serikali kuhakikisha inatimiza ahadi ilizojiwekea kwa mujibu wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC).

“Kabla ya kuangalia nchi nyingine tujiulize, je, Tanzania tunatekeleza ahadi zetu? Tuna mpango mkakati wa nishati ambayo inakinzana na malengo yetu ya kupunguza nishati chafu? Pia tuangalie namna nzuri ya kufanya biashara ya kaboni,” anashauri.

Katika makubaliano ya Paris mwaka 2015 (Cop21) nchi ziliweka mikakati ya kupunguza matumizi ya nishati chafu ili kudhibiti ongezeko la joto libaki chini ya nyuzijoto 1.5 za sentigredi ifikapo 2030.

Hata hivyo, hadi sasa kwa mujibu wa UNFCCC dunia ipo kwenye nyuzijoto 1.1 za sentigredi, ambazo zinakaribia ukomo uliowekwa ikilinganishwa na 0.7 mwanzoni mwa mwaka 2000.

Taarifa iliyochapishwa Novemba 8, 2023 kwenye tovuti ya Mpango wa Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) ilibainisha kuwa Serikali duniani zinapanga kuzalisha takribani asilimia 110 zaidi ya nishati chafu (makaa ya mawe, mafuta na gesi) tofauti na malengo yaliyowekwa.

Jambo hilo linafifisha uwezekano wa kudhibiti ongezeko la joto.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi