Kitaifa
Miradi 296 yatoa ajira 17, 000 Zanzibar
Dar es Salaam. Takwimu kutoka Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa), zimebainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Dk Hussein Mwinyi, miradi 296 imeidhinishwa katika sekta mbalimbali ikiwa na mitaji ya Dola 4.5 bilioni (takribani Sh11.3 trillion) visiwani humo.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, kwa ujumla miradi hiyo imezalisha ajira za moja kwa moja 17,000 ambapo sekta zilizohusika ni zile za hoteli, ujenzi na uzalishaji, huku kati ya miradi yote, miradi 109 yenye thamani ya Dola 2.8 bilioni (takribani Sh7 trilioni), imeelekezwa Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo ajira 7,397 zimezalishwa.
Hayo yameelezwa leo Novemba 25, 2023 na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa wakati wa kampeni ya ‘Mkono kwa Mkono’ inayofanyika katika mikoa mitano ya Zanzibar, huku leo ikiwa katika Mkoa wa Mjini Magharibi.
Lengo la kampeni hii ya siku 60 kwa mujibu wa waandaaji ambao ni na Shirika la Utangazaji wa Zanzibar (ZBC) pamoja na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), ni kuibua fursa, mbinu na suluhisho la changamoto za wananchi kabla ya maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Kuhusu uwekezaji, Mustafa amesema awamu ya tatu chini ya Rais Mwinyi imechochea kasi ya maendeleo baada ya kila sekta na kufungua fursa za uwekezaji, hivyo ameshawishi wakazi wa mkoa huo kuchangamkia fursa hizo.
Hata hivyo, Mustafa amewataka wakazi wa mkoa huo kuachana na utamaduni wa kuchafua mazingira kwenye maeneo ya biashara na kuheshimu maagizo na kufanya kwenye maeneo waliyopangiwa
“Uwekezaji huu mkubwa ni jambo jema kwani mkoa huu ndio lango kubwa la wawekezaji, wenye asilimia 47 ya idadi ya watu wa Zanzibar,” amesema Mustafa akifafanua;
“Kwa hiyo fursa ni nyingi mno, kazi iliyofanyika chini ya Rais Mwinyi ni kubwa, mfano sekta ya miundombinu, Serikali imejenga barabara, madaraja ya juu, hospitali, viwanja vya mpira, huko kote kuna fursa. Kwa wajasirimali pia tunaona mikopo ya boti na vifaa vya uvuvi na kilimo cha mwani vimetolewa.
Aidha, Mustafa ameshauri Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (Zeea) kutazama mkoa huo kwa jicho la kipekee katika uwezeshaji wa mikopo kutokana na wingi wa wananchi wake, akisema: “Bado mikopo haijaakisi idadi ya watu, tunafikiria tuone ni kwa namna gani itaendana na wingi wao.