Kitaifa
Janga la utoaji mimba kwa wanawake shubiri
Dar es Salaam. Utoaji mimba usio salama na kinyume cha sheria, umekuwa ukihatarisha maisha ya wanawake wengi nchini, huku baadhi yao wakiingia gharama ya kutibu madhara kwa maisha yao yote.
Madhara hayo yaliyotajwa ni ya muda huohuo ikiwamo kutokwa damu nyingi, kizazi kutobolewa au kuoza.
Mengine ya muda mrefu ambayo husababisha mirija ya uzazi kuziba, kizazi kuwa na majeraha, hivyo kushindwa kushika mimba inapohitajika au shingo ya kizazi kulegea, hivyo mimba kutoka kila inapotungwa.
Dawa aina ya misoprostol, waya, spoku za baiskeli, kijiko, miti ya mihogo na hata baadhi ya kemikali vimetajwa kutumiwa zaidi na wanawake wanaofika kuhitaji usaidizi wa madaktari, huku wengine wakipoteza maisha.
Kwa Tanzania, ukosekanaji wa huduma salama za utoaji mimba husababishwa na mazuio ya kisheria ambayo yamefafanuliwa kwenye vifungu namba 150, 152 na 230 vya kanuni ya adhabu Sura ya 16 (Marekebisho ya 2022).
Hata hivyo, Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria (TDHS) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu NBS hivi karibuni imeonyesha asilimia 23 ya mimba kwa Mkoa wa Dar es Salaam huharibika.
“Asilimia 23 ya mimba katika Mkoa wa Dar es salaam kwa mwaka ziliharibika, hiki ni kiwango kikubwa kuliko mkoa wowote na kiwango cha chini zaidi ya asilimia moja kilikuwa Mkoa wa Rukwa,” ilieleza ripoti hiyo.
Changamoto hiyo inazidi kuongezeka, katika robo mwaka ya Januari hadi Juni 2023, Wizara kupitia Bohari ya Dawa (MSD), ilinunua vifaa ambavyo hutumika kuwahudumia kina mama ambao mimba zao zimeharibika au wametoa na kupata matatizo vyenye thamani ya Sh245,447,667.
Mhadhiri wa Chuo cha Sayansi na Afya shirikishi (Muhas), Dk Ali Said alisema utafiti uliofanyika mwaka 2018 ulionyesha mimba takribani milioni 2.9 hutungwa kila mwaka.
‘“Miongoni mwa hizo, utafiti ulionyesha mimba milioni 1.3 hazikupangwa, mimba 430,000 hutoka au kutolewa,” alisema Dk Said.
Ingawaje mimba zinazoharibiwa ambazo hurekodiwa ni 430,000 kwa mwaka, wataalamu hao wanasema idadi ni kubwa zaidi kwa sababu wanaofika vituoni kuhitaji msaada wa kitabibu ni wale waliopata madhara ya papo kwa hapo.
Waathirika
“Niliponea tundu la sindano mwaka 2004 nilipojaribu kutoa mimba ikakwama, damu zilitoka nikahisi tayari. Saa 28 hivi baadaye tumbo liliuma sana mpaka sikuweza kufanya chochote, wazazi wangu walinipeleka Hospitali ya Mwananyamala nikasafishwa,” alisema Joyce Kilindi (34), mkazi wa Kimara.
Binti huyo alikiri kuchokonolewa mimba hiyo na mtu asiye mtaalamu uchochoroni, mitaa ya Magomeni.
Alisema mimba haikutoka ila iliharibika na kizazi kikapata maambukizo, tatizo linalomfanya ahangaike mpaka leo kutafuta mtoto bila mafanikio.
“Sikutolewa kizazi nilisafishwa tu, lakini tangu hapo sina historia ya kushika ujauzito tena,” alisema Joyce.
Mmoja wa wauguzi katika zahanati moja iliyopo Tabata jijini Dar es Salaam (hakutaka kutaja jina lake) alisema kuna changamoto za wanawake wengi kutoa mimba wasizozihitaji.
“Kuna mama alikuwa na watoto wawili wa mwisho alikuwa kidato cha nne, mumewe alifariki miaka mingi, akawa na uhusiano na mwanaume mwingine huku akitumia njia za uzazi wa mpango.
“Alikaa miezi sita hapati hedhi akidhani ni kawaida kutokana na dawa anazotumia, lakini nilipomshauri tupime tulibaini ana ujauzito, akawa haitaki tukamshauri ajifungue akaondoka, kumbe anakula vitu akihangaika kuitoa kimya kimya,” alisema.
Muuguzi huyo alisema mimba ilipofikisha miezi nane akapata maambukizi, mtoto akafia tumboni.
“Alifanyiwa upasuaji wakatoa mtoto, baada ya siku tatu alirudi nyumbani ila akaendelea kuumwa. Alipozidiwa akapelekwa Vingunguti huko wakamtibu kawaida akarudi nyumbani baadaye akaomba kwenda kwao Morogoro.
“Huko nako akaanza tena kuumwa akazidiwa akapelekwa zahanati akawa na hali mbaya wakampa rufaa akapelekwa Hospitali ya Rufaa Morogoro nao wakasema maambukizi akapelekwa Muhimbili, alikaa siku mbili akafariki,” alisimulia kisa hicho.
Muuguzi wa zahanati mojawapo iliyopo Kimara (jina linahifadhiwa) alisema zahanati zimekuwa zikipokea wanawake na wasichana wengi waliojaribu kutoa mimba na wakashindwa kufanikiwa.
“Tatizo ni kubwa, kila mwezi hatukosi wateja 10 walioharibu mimba wakaja kupata huduma. Angalau sasa hawaji wanaotoka usaha kama zamani na hali nzuri si ya kutisha kama zamani, bado changamoto ipo kwa asilimia kubwa,” alisema muuguzi huyo.
Mkurugenzi wa kanda wa mtandao wa kimataifa wa wanawake wa haki za uzazi Afrika (WGNRR AFRICA), Nondo Ejano alisema huduma ya afya kwa ajili ya kudhibiti matatizo ya utoaji mimba usio salama inagharimu mfumo wa afya wa Serikali Sh10.4 bilioni kwa mwaka.
“Gharama hizi za kibinadamu na za kifedha zinaweza kuepukika na hii inaweza kutoa rasilimali kutumika mahali pengine, ikiwa sheria zitafanyiwa marekebisho,” alisema Ejano.
Madhara
Dk Said ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alisema mama akishatoa mimba bila usalama hupata changamoto ya maambukizi.
“Kwa mfano Muhimbili tunaona wengi wanapata maambukizi hasa zile zilizotolewa na vifaa ambavyo si visafi kama waya, spoku za baiskeli, mihogo na wengine wanatumia kemikali sasa ile inaleta maambukizi na wengine wanatoboa vizazi,” alisema.
“Wakiingiza spoku wanadhani wanatoboa mimba kumbe wanatoboa kizazi mpaka utumbo, kwahiyo matibabu yake tunalazimika kutoa kizazi na kukata sehemu ya utumbo ulioathirika,” alisema.
Dk Said alisema wakati wa utoaji mimba mama anaweza kutokwa damu nyingi mpaka kupoteza maisha lakini pia inaweza kusababisha matatizo ya muda mrefu.
“Maambukizi husababisha shida ya kuziba kwa mirija ya uzazi na baadaye asizae tena, wakati mwingine inaweza kuharibu shingo ya kizazi inalegea na mama huyu akija kupata mimba nyingine zinakua hazikai kwakuwa ile shingo haina nguvu ya kushikilia mimba,” alisema.
Dk Said alisema tatizo la wanawake kutokupata ujauzito kwa sasa ni kubwa na linazidi kuongezeka na ripoti ni nyingi kwa sasa ukilinganisha na zamani.
Alisema mama kupata mimba haitegemei mwanaume pekee, bali inatokana na wote asilimia 40 mwanamke, 40 mwanaume na asilimia 20 wote wawili.
“Wapo ni matatizo ya kuzaliwa, lakini wanaopata hivyo kutokana na changamoto ya utoaji mimba wapo, wengi wakishatoa mimba mirija yao inaziba na wapo wanaliokwanguliwa sana kizazi ule ukuta, hivyo unaziba kwa hiyo mimba zinakuwa hazishiki, wanaoshindwa kuzaa wengi walitolewa mimba katika mazingira yasiyofaa,” alisema.
Hata hivyo, alisema lazima wampime mama kuona shida ilikua hiyo au ni vinginevyo, lakini pia wapo wanaopewa tiba ya kuzibua mirija.
Alisema wanaotumia dawa za kutoa mimba maarufu miso, wamekuwa wakikutana na changamoto ya kushindwa kukadiria umri wa mimba na vidonge vingapi atumie, hivyo wengi wanatoa mimba lakini haitoki kikamilifu na wengine kuvuja damu nyingi.
Sheria na tafiti.
Dk Said alisema sheria ya Tanzania haizuii kabisa kutoa mimba lakini ina makatazo katika sehemu fulani, “Sheria inasema mimba inaweza kutolewa wiki ya 28 kama inahatarisha maisha ya mama. Ijapokuwa sheria za kimataifa zinatushauri kama mama amebakwa, amepata mimba kutoka kwa ndugu.”
Hata hivyo alisema kama mama haihitaji mimba bado sheria haimruhusu, hivyo inawasukuma wengi kwenda kwenye njia isiyo sahihi.
Tafiti iliyofanywa na Taasisi ya Guttmacher Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili (MUHAS) ya mwaka 2015/16 ilisema kuwa inakadiriwa kuwa, mimba 405,000 zilitolewa ndani ya mwaka 2013 nchini.
Idadi hii ni kiwango cha utoaji wa mimba 36 kwa kila wanawake 1,000 wenye umri kati ya miaka 15-49 na uwiano wa utoaji mimba 21 kwa kila watoto 100 wanaozaliwa wakiwa hai.
Tafiti iliongezea kuwa utoaji mimba usio salama unachangia zaidi ya theluthi moja ya wanaolazwa hospitalini kutokana na matatizo yanayohusiana na mimba na takribani robo moja ya vifo vya uzazi.
Kauli ya Serikali
Mkurugenzi msaidizi kitengo cha afya ya uzazi na mama Wizara ya Afya, Dk Mzee Nassoro alisema utoaji mimba usio salama bado ni tatizo nchini, linalochangia asilimia 10 ya vifo vitokanavyo na uzazi.
“Sheria za Jinai za Tanzania zinakataza kutoa mimba isipokuwa kwa sababu za kiafya kama vile ujauzito unaohatarisha maisha ya mama, mfano mjamzito mwenye matatizo makubwa ya moyo au kama mtoto aliyeko tumboni atakuwa na matatizo makubwa ambayo hayawezi kumruhusu kuishi,” alisema.
Alisema Serikali inasimamia utoaji wa huduma za uzazi wa mpango katika vituo vya huduma bila malipo, ili kuwezesha wanawake na wanaume kuzuia mimba zisizotarajiwa.
Aliwaasa vijana, kinamama na wanaume wachukue hatua za kuhakikisha kuwa mimba zinazopatikana zinakuwa zimepangwa.
“Wahudhurie katika kliniki za uzazi wa mpango ili wapatiwe elimu ya afya ya uzazi ikiwemo jinsi ya kuepukana na mimba zisizotarajiwa ili kuepukana na kuishia kwenye uavyaji usio salama,” alisema.