Connect with us

Kitaifa

70 wajitokeza kuongezwa shepu Mloganzila

Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili – Mloganzila, inatarajia kuanza rasmi upasuaji rekebishi (Bariatric and Reconstructive surgery) wa kuongeza shepu (makalio) Desemba 10, 2023, ikiwa ni awamu ya pili baada ya ule wa kupunguza unene.

Oktoba 27, 2023, Mloganzila ilifanya upasuaji kwa wagonjwa waliokuwa wakirekebisha maumbile ikiwemo wanaopunguza unene, mafuta ya mwilini na kurekebisha maungo ikiwemo kupunguza tumbo au nyama kwenye mikono na sehemu nyingine za mwili.

Akizungumza na Mwananchi wiki hii, Mkuu wa Idara ya Upasuaji Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dk Eric Muhumba amesema wagonjwa watakaoongezwa shepu na maumbile wanatarajia kuanza kuwafanyia Desemba 10.

“Tulianza na upunguzaji wa uzito kwanza ambapo tuliwafanyia wagonjwa wanne, rasmi kwa wale wanaoongeza shepu na makalio tutaanza mwezi ujao na tayari kuna wagonjwa wapo kwenye orodha yetu,” amesema.

Dk Muhumba amesema mwitikio wanajitokeza ni wengi ambao wanafika wenyewe katika hospitali hiyo ya Taifa na wengine wanapiga simu.

“Mtaalamu bobezi ambaye atakuja kwa ajili ya kurekebisha maumbile atafika Desemba na kwenye hiyo kambi mpaka sasa kwenye orodha yetu kuna wagonjwa 70, hatuwezi kuwafanyia hao wote tumepanga kuwafanyia wagonjwa 10 kwanza kisha tutaendelea nao siku zinazofuata,” amesema Dk Muhumba

Amesema wamekuja na huduma hiyo kufuatia matokeo ya huduma ya kupunguza unene kwa puto ambayo imefanikiwa na wengi wanahitaji kurekebishwa maumbile yao baada ya kupungua unene: “Wamepungua lakini wengine nyama zinatepeta hivyo wanahitaji mtaalamu anayefanya huduma hizo awarekebishe maungo.”

Dk Muhumba amesema wamesogeza huduma hizo kwa maana awali Watanzania wengi walikwenda nje ya nchi na kwamba gharama itaanzia Sh15 milioni mpaka Sh22.5 milioni.

“Gharama itakuwa rahisi tofauti na mtu akienda nje ya nchi, hatujaweka gharama halisi maana mteja akifika kila mmoja ana namna yake ya huduma hivyo itategemea huduma gani anapewa na itaanzia Dola za Marekani 6000 mpaka 9000,” amesema.

Daktari bingwa wa kurekebisha maumbile Hospitali ya Muhimbili – Mloganzila, Dk Lauren Rwanyuma amesema mara nyingi wamekuwa wakipokea wateja wa kupunguza matiti na tumbo, hata hivyo alisema huenda gharama kubwa inachangia.

“Lakini mwitikio siyo sana tunahisi kwa sababu ya gharama na labda hatujajitangaza sana, Mloganzila watafanya hivi karibuni tunataangalia wao tuone mwitikio utakuwaje,” amesema Dk Rwanyuma.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi