Makala

Kuna la ziada vijiwe vya bodaboda

Dar es Salaam. Kijiwe ni mahali ambapo watu hususani vijana wasiokuwa na kazi hukutana, hukaa bila kufanya kazi.

Hii ni kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili ya Baraza la Kiswahili la Taifa, toleo la pili.

Tofauti na hilo, madereva wa pikipiki maarufu bodaboda wamekuwa na utaratibu wa kuanzisha vijiwe. Hapo hukutana kusubiri wateja lakini wapo pia ambao hawana ajira wakingojea kupewa kazi za siku na wenzao ‘deiwaka’.

Kinapoanzishwa kijiwe, utaratibu maalumu huwekwa ikiwa ni pamoja na kuchagua viongozi. Ni kupitia utaratibu huu, wanaoukiuka huadhibiwa ikiwamo kutozwa faini ya hadi Sh20,000 na hata kufukuzwa kijiweni.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Digital katika vijiwe kadhaa jijini Dar es Salaam, umebaini namna bodaboda wanavyojiendesha kwa kufuata utaratibu na kanuni walizojiwekea.

Kujiunga kijiweni

Kuna gharama hutozwa ili kujiunga kwenye kijiwe. Kiwango cha fedha hutofautiana kati ya kimoja na kingine, wapo wanaolipa Sh50,000 kwa mtu mmoja na wengine hadi Sh400,000.

Salum Rashid ni Makamu Mwenyekiti wa kijiwe cha bodaboda kilichopo Mbezi Tangi Bovu, amesema wao wameenda mbali kwa kuunda kikundi na wana katiba.

Ndani ya katiba hiyo, amesema kuna kiingilio kwa mwanachama mpya anayejiunga na kijiwe hicho ambaye anapaswa kutoa Sh200,000.

Rashid amesema fedha hiyo ya kiingilio humwezesha mwanachama mpya kusaidiwa sawa na wa zamani pale anapopata shida.

“Haiwezekani wewe umejiunga jana, halafu tukupe mchango unapopatwa na matatizo sawa na aliyekuwapo siku nyingi. Kiingilio anachotoa kinaingizwa kwenye mfuko na kuanza kunufaika saa chache tangu alipoingia iwapo atapata tatizo lolote,” amesema kiongozi huyo.

Amesema mwanachama akipata ajali na kulazwa hospitali huchangiwa Sh10,000 na kila mwanachama, lakini wakati mchango ukiendelea huwa wanatoa fedha kwenye mfuko.

“Hapa kijiweni tupo zaidi ya watu 30, wanachama hai wapo 25, hivyo ukijumlisha Sh10,000 kila mmoja ni kwamba mgonjwa atapaswa kupewa Sh250,000. Kutoka kwenye mfuko tunampa hizi, mchango  ukikamilika tunazirudisha,” amesema.

Amesema huendelea kuchanga kumuuguza mwanachama hadi atakapopona na kurejea kazini.

Kwa mujibu wa Rashid, mwanachama pia huchangiwa Sh10,000 na kila mmoja anapouguliwa na baba, mama au mtoto au mmoja kati ya hao anapofariki.

Rashid amesema wana mpango wa kuongeza fedha za kiingilio kutokana na kupanda kwa gharama za maisha, wakilenga kufikia Sh400,000 kwa mwanachama mpya.

Magomeni Mapipa

Daudi Kisoma, Makamu Mwenyekiti wa kijiwe cha Magomeni Mapipa, amesema wapo 32 na kwa sasa hawaruhusu mtu mwingine kujiunga.

Amesema kijiwe hiki walikianzisha kwa utaratibu wa mwanachama kuwa na barua ya utambulisho kutoka Serikali ya mtaa.

Pia kila wiki mwanachama hulazimika  kulipa Sh1,000 ambazo huwekwa kwenye mfuko maalumu ambao hivi sasa una Sh3 milioni.

Kisoma amesema mwanachama aliyepata ajali na kushindwa kufanya kazi huchangiwa Sh300,000.

Amesema iwapo ataendelea kuwa mgonjwa, wataendelea kumchangia hadi atakaporejea kazini. Mchango huo amesema hutokana na makubaliano kati yao yakiwa  kati ya Sh1,000 na Sh2,000.

Kwa waliofiwa na wazazi au mtoto amesema huchangiwa Sh100,000 na iwapo mwanachama atafariki dunia, huchanga Sh300,000.

“Ili isichukue muda mrefu kumpatia muhusika, wakati tukiendelea kuchangishana tunachukua fedha kwenye mfuko na kumpa,” amesema.

Amesema wanatarajia kuja na mpango wa kununua pikipiki na kukopeshana kwa riba nafuu.

“Kuna tajiri anakupa pikipiki yenye thamani ya Sh2.8 milioni anataka katika mkataba wenu umzalishie Sh1.5 milioni yaani kwa ujumla utamkusanyia Sh4.3 milioni fedha ambazo ni nyingi,” amesema.

Kibamba Kwa Mangi

Katibu wa kijiwe cha bodaboda Kibamba kwa Mangi, Azizi Mikidadi amesema kila Jumanne huchangishana Sh2,000 sawa na Sh8,000 kwa mwezi.

Ni kupitia mchango huo amesema hawapitishi daftari la michango kwa jamii wanapofikwa na matatizo.

“Hela hii tunaiingiza kwenye akaunti yetu, kila mwananchama atapata taarifa kupitia simu yake kwa kuwa akaunti imeunganishwa na huduma ya simu kiganjani, hivyo hela itakayoingia na kutoka kila mmoja ataiona,” amesema.

Amesema kabla ya kutoa fedha kwa ajili ya matumizi lazima waitishe kikao na watu wote waridhie.

Mwanachama mpya kijiweni hapo amesema anapaswa kulipa kiingilio cha Sh150,000, fedha itakayomsaidia kwenye matatizo kama vile ajali, kufiwa, kuugua au kuuguza.

Tabata Mwananchi

Francis Gustaph, mhazini wa kijiwe cha Tabata Mwananchi, amesema wapo wanachama 98 na kiingilio kwao ni Sh400,000.

Kiwango hicho amesema hulipwa kwa awamu, akiwa mwanachama mpya hulipa ndani ya miezi sita.

Amesema mwanachama anapougua huchangiwa na kila mwanachama Sh5,000. Akifiwa na wazazi au mlezi huchangiwa Sh10,000 na kila mmoja. Pia kuna wakati huongezwa hela kutoka kwenye mfuko ambao hivi sasa una zaidi ya Sh3 milioni.

Adhabu kwa wakosaji

Kulingana na utaratibu waliojiwekea kwenye vijiwe, bodaboda huwajibishana kwa kutozana faini.

Katika kituo cha Tangi Bovu, Rashid amesema kwa wanaolewa wakiwa kazini hutozwa faini ya Sh5,000 huku pikipiki ikifungwa mnyororo siku nzima.

Kwa kijiwe cha Magomeni Mapipa, Kisoma amesema bodaboda akinywa pombe wakati wa kazi, hutozwa faini ya Sh20,000 na pikipiki hufungwa mnyororo ndani ya saa 24.

“Ukitukana abiria, kupigana wenyewe kwa wenyewe faini yake ni Sh20,000,” amesema.

Gustaph wa Tabata Mwananchi, anasema hawana utaratibu wa kutozana faini isipokuwa pikipiki hufungwa hata kwa siku tatu ili muhusika asiweze kufanya kazi.

“Kwa mfano umemtukana abiria, tutakupiga ‘cheni’ siku tatu, ukikimbilia abiria wakati mwenzako tayari kashaenda, unafungiwa cheni bodaboda yako kwa saa moja. Ukimtolea maneno machafu abiria au kumdhihaki, unaweza kufungiwa cheni chombo chako siku nzima,” amesema.

Kauli ya uongozi

Said Chenja, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Waendesha bodaboda na bajaji Mkoa wa Dar es Salaam, amesema wanatambua utaratibu unaowekwa vijiweni licha ya kuwa katika utekelezaji kuna changamoto, wakati mwingine ikiwemo kuingiliwa na mamlaka za Serikali za mitaa.

Amesema kuwa na uongozi ni moja ya sharti la kuanzisha kijiwe ikiwa ni pamoja na kuwa na katiba.

Chenja ameomba msaada wa Serikali ili kubadili uendeshaji wa kazi ya bodaboda akisema mambo mengine mazuri walijifunza nchini Rwanda walikokwenda kwa ziara mwaka jana.

Amesema kutoka Rwanda walijifunza kuhusu usajili wa madereva ili wawe kwenye kanzi data, kutopiga kelele za muziki, kuwekwa kamera kwenye makutano ya taa za barabarani, abiria na dereva kuvaa helimeti na namna ya kumdhibiti asiyevaa.

“Haya ni mambo tungependa tuyatekeleze nchini, lakini hatutaweza wenyewe bila mkono wa Serikali,” amesema Chenja.

Wenyeviti wa mtaa

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ngobedi, Kata ya Chanika, Mohamedi Kilungi amesema hawaingilii utaratibu wanaojiwekea bodaboda wa kuchangishana fedha, isipokuwa wanapovurugana ndipo hufika ofisi za Serikali ya mtaa.

“Wanapoandikishana hadi katiba ya kufuata huwa hawatukumbuki viongozi, ila wakishatofautiana tu ndio wanakuja jambo ambalo si zuri kwa kuwa nasi tukiwa na ushahidi wa makaratasi yao inakuwa rahisi kuwabana wanaokiuka,” amesema.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nyakwale, Kata ya Kibada wilayani Kigamboni, Said Pazi hatofautiani na Kilungi.

Amesema bodaboda waliwahi kumshtaki katibu wao katika ziara ya mkuu wa wilaya kuwa amekula fedha zao,  lakini ukweli ulibainika kuwa alichelewa kutoa taarifa hivyo mambo yakawa shwari.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Kariakoo Magharibi, Said Omar amesema, “Ukiona tumeingilia kati ni kuhakikisha suala la ulinzi na usalama kwa kujua wapo wangapi na wanafanyaje kazi zao, hili la michango huwa tunawaachia wenyewe.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi