Kimataifa

Weah anavyotuaminisha yasiyowezekana siasa za Afrika

Kutoka Kenneth Kaunda, Zambia mwaka 1991, Goodluck Jonathan, Nigeria mwaka 2015, Edgar Lungu, Zambia mwaka 2021, Joyce Banda, Malawi mwaka 2014, sasa ni George Weah, Liberia mwaka 2023.

Uchaguzi wa kisiasa Afrika ni vita ya kufa au kupona. Ni ndoto ya mchana rais aliye madarakani kushindwa uchaguzi. Ni tendo la kimalaika kwa aliyeshindwa kukubali matokeo na kumpongeza mpinzani wake.

Jonathan, akiwa Rais wa Nigeria, alikubali kushindwa na Muhammadu Buhari, akampigia simu na kumpongeza kwa ushindi. Weah, ameridhia matokeo yaliyomnyima ridhaa ya kuongoza Liberia kwa muhula wa pili. Alinyanyua simu na kumpongeza mpinzani wake, Joseph Boakai.

Weah, hakungoja Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Liberia (Nec), Jerome Korkoya, atangaze matokeo ya mwisho. Alipoona tayari maji ni mengi kuliko unga, alinyanyua simu na kumpigia Boakai, akampongeza kwa ushindi.

Hivyo ndivyo inapaswa kuwa ndani ya taifa linaloishi ndani ya demokrasia. Kwa Weah, mwanamichezo wa daraja la juu, mchezaji bora wa soka duniani, Ulaya na Afrika. Akiwa Mwafrika pekee kutwaa tuzo ya Ballon d’Or na ya Fifa mwaka 1995, ameonesha uanamichezo, hulka na utamaduni wake.

Kwa mwanamichezo, kushinda na kushindwa ni sehemu ya mchezo. Mwisho kabisa, baada ya mashindano, jasho limevuja, jumlisha maumivu ya kushindwa, ila inakupasa kupeana mikono na mshindi, kukumbatiana au kubadilishana fulana. Ni tukio lenye maana kubwa kwa uungwana kwa wanamichezo duniani.

Lugha ya michezo, inaitwa “fair play”, yaani haki, heshima na usawa mchezoni. Weah, ameonesha fair play dhidi ya Boakai. Inafundisha kuwa ustaarabu wa kimichezo ukiambukizwa kwenye siasa duniani kote, uchaguzi hautakuwa mchakato wa kufa au kupona.

Katika mchezo wa soka ambao Weah ameucheza kwa kiwango cha juu kabisa ulimwenguni, ukishindwa leo, unakwenda kujipanga kwa michuano inayofuata. Ndivyo Weah alivyofanya. Alihutubia taifa na kuwaahidi Waliberia kuwa mwaka 2029, atarejea ulingoni.

“Waliberia wameongea na sauti yao imesikika. Huu ni wakati wa neema kwenye kushindwa, wakati wa kuiweka nchi yetu juu ya chama, na uzalendo juu ya masilahi binafsi,” alisema Weah, akilihutubia taifa, Ijumaa, Novemba 17, 2023.

Jumapili, Novemba 19, 2023, Weah alihudhuria ibada kanisani, Monrovia, alipopewa nafasi ya kuzungumza, alisema: “Tusingekuwa kanisani leo kama ningefanya kile ambacho wengine walitaka nifanye. Hatuwezi pia kujilaumu kwa kushindwa uchaguzi. Ni mchakato wa kujifunza.”

Weah alishinda uchaguzi wa urais Liberia mwaka 2017. Alimshinda Boakai, ambaye kwa wakati huo alikuwa Makamu wa Rais. Boakai hakukubali kushindwa, wala hakumpongeza Weah. Hivyo, matendo ya kiungwana ya Weah, yanajenga sura mpya, yanaambukiza ustaarabu wa soka kwenye siasa.

Desemba 2016, aliyekuwa Rais wa Gambia, Yahya Jammeh, alipiga simu kumpongeza mpinzani wake, Adama Barrow kwa ushindi. Hata hivyo, haikufika wiki, Jammeh, alikataa matokeo, hivyo kukaribia kuiingiza nchi kwenye machafuko. Ilibidi, jeshi la nchi za Magharibi, likiongozwa na Senegal, lihami hali ya amani na kumlazimisha Jammeh kuachia madaraka kwa amani.

Weah, atatakiwa kukabidhi nchi Januari 2024, atakapokuwa anahitimisha muhula wake wa miaka sita madarakani. Anapaswa kusimamia uungwana wake hadi siku anakabidhi madaraka kwa Boakai. Hapaswi kurudi nyuma kama ilivyokuwa kwa Jammeh Gambia. Atajivunjia heshima.

Boakai, mgombea wa chama cha UP, ameshinda urais Liberia kwa kupata kura 814,428, sawa na asilimia 50.64, Weah, chama cha CDC, aliambulia kura 793,910, asilimia 49.36. Liberia ina watu milioni 5.5. Jumla ya watu waliojiandikisha kupiga kura ni 2.498 milioni.

Liberia ngumu kisiasa

Kipindi cha kampeni, Weah alishambuliwa na wapinzani, vilevile wachambuzi wa kisiasa na kiuchumi, walimkosoa kwa kufumbia macho rushwa serikalini, kutotoa ajira mpya, vilevile kukosa mbinu za kukabiliana na dawa za kulevya, wakati vijana wengine wanaangamia mitaani.

Kwa kutambua hoja hizo, Boakai aliendesha kampeni zake kwa kujipambanua kwenye mambo mawili; kudhibiti rushwa na kupambana na dawa za kulevya. Bila shaka, ahadi zake ziliwagusa wengi, hivyo kumchagua makamu huyo wa rais kwa mihula miwili, 2006 mpaka 2018. Pamoja na hivyo, Weah alichukua nchi kipindi ikikabiliwa na athari za janga la Ebola, ambalo liliitesa Liberia kati ya mwaka 2013 na 2016. Kisha, miaka miwili ya urais wake, janga la Covid-19 liliitesa dunia. Tangu wakati huo, hali haijawa salama tena.

Uchaguzi 2023, unakuwa wa nne kwa Liberia kutopata mshindi wa urais mzunguko wa kwanza. Awali, Weah aliongoza kwa kura 804,087, ambazo ni asilimia 43.83. Boakai alipata kura 796,961, asilimia 43.44.

Wagombea urais walikuwa 20. Kwa vile Weah aliongoza kwa kura lakini hakuvuka asilimia 50, inayohitajika kikatiba, ilibidi mchuano urudiwe baina ya mshindi wa kwanza na wa pili. Nyota njema ikamwakia Boakai.

Uchaguzi Mkuu Liberia, uliofanyika Oktoba 10, 2017, Weah pia aliongoza lakini hakuvuka asilimia 50, hivyo ngwe ya pili ilirudiwa dhidi ya Boakai. Duru ya pili, Weah alishinda kwa asilimia 61.

Awali, Weah wa CDC alipata kura asilimia 39.2 na Boakai wa Unity asilimia 29.6. Kwa vile na mwaka 2023 mshindi amepatikana duru ya pili, inafanya Liberia, ndani ya miaka 18 sasa, liwe taifa ambalo mshindi wa urais hapatikani kwa urahisi. Mwaka 2005 na 2011, Rais wa Liberia alichaguliwa baada ya kufanyika uchaguzi wa marudio.

Ikumbukwe pia Weah aliongoza kura mwaka 2005, tena kwa tofauti kubwa dhidi ya Ellen Johnson Sirleaf. Alipata asilimia 28 na Sirleaf asilimia 19. Uchaguzi uliporudiwa, Sirleaf alivuna kura asilimia 59.4 na Weah 40.6. Sirleaf akatangazwa Rais, akaweka rekodi kuwa mwanamke wa kwanza Afrika kuwa mkuu wa nchi.

Mwaka 2011, Sirleaf akitetea kiti chake kwa muhula wa pili kwa tiketi ya chama chake cha Unity, alikabiliana vilivyo na Winston Tubman wa CDC, mgombea mwenza wake akiwa Weah. Mgombea mwenza wa Sirleaf alikuwa Boakai.

Matokeo ya awali mwaka 2011 ni kuwa Sirleaf alipata asilimia 43.9, Tubaman asilimia 32.7. Uchaguzi wa marudio ulipofanyika, Sirleaf alishinda kwa kura asilimia 90.7, wakati Tubman alipata kura asilimia 9.3. Sirleaf akawa amefanikiwa kutetea kiti chake.

Imekuwa sasa mazoea kwamba Liberia hawapati mshindi wa urais katika matokeo ya awali. Tangu kuvunjwa kwa utawala wa Waliberia waliotokea Marekani, Rais wa zamani wa nchi hiyo, Charles Taylor ndiye pekee aliweza kushinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu 1997. Taylor alishinda kwa kura zaidi ya asilimia 75.

Taylor aliwateka vijana. Wazee waliwaonya kuwa ni mtu hatari kwa sababu alisababisha mauaji ya watu wengi katika Vita ya Kwanza ya Kiraia. Vijana waliibuka na kauli mbiu; He Killed My Ma, He Killed My Pa, but I Will Vote for Him (Alimuua mama, alimuua baba lakini nitampigia kura). Taylor alijiuzulu urais mwaka 2003 kwa shinikizo la kimataifa, ikiwa ni baada ya kumalizika kwa Vita ya Pili ya Kiraia Liberia.

Katika kutawala siasa za ukabila Liberia, hakuna kabila hata moja linalofikia wingi wa watu japo asilimia 25 ya nchi. Kabila kubwa zaidi ni Kpelle ambalo watu wake wanakadiriwa kuwa asilimia 20.3, mengine yote idadi yake ya watu ni chini ya asilimia 14.

Hali hiyo inasababisha mpaka watu wasio na nguvu kabisa kisiasa, wawe na uamuzi kwenye matokeo ya mwisho ya urais.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi