Connect with us

Kitaifa

Tahadhari ya mvua siku nne mfululizo

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa tahadhari ya kuwapo kwa mvua kubwa kuanzia leo Jumatano Novemba 22 hadi Novemba 25 ambazo huenda zikasababisha vifo ikiwa tahadhari hazitachukuliwa.

TMA imesema mvua hizo zinatarajiwa kunyesha katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Pwani, Lindi, Mtwara, Tanga na visiwa vya Mafia, Unguja na Pemba.

Taarifa ya mamlaka  hiyo iliyotolewa jana Jumanne Novemba 21, 2023 katika mitandao yao ya kijamii inaeleza athari zinazoweza kujitokeza ni pamoja na baadhi ya barabara kutopitika kutokana na mafuriko pamoja na vifo, hivyo wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari.

Pia, TMA imetoa angalizo kwa mvua hizo kuendelea  hadi Ijumaa na Jumamosi katika maeneo machache ya mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Mafia Unguja na Pemba, huku ikionya baadhi ya makazi kujaa maji na kuathiri shughuli za kiuchumi.

Agosti 26, 2023 TMA ilitoa taarifa ya uwezekano wa kuwapo kwa mvua kubwa za El-Nino ambazo huenda zikasababisha vifo, magonjwa ya mlipuko na uharibifu wa miundombinu kuanzia Oktoba hadi Desemba 2023.

TMA ilisema mvua hizo zitasababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi, upotevu wa mali na madhara kwa binadamu na mazingira.

Kutokana na hali hiyo, TMA ilizishauri sekta na taasisi mbalimbali, zikiwamo za kilimo, mifugo, uvuvi, utalii, wanyamapori, uchukuzi, mamlaka za miji, nishati, maji na madini, sekta binafsi, Wizara ya Afya na menejimenti za maafa kuchukua hatua mapema kabla ya kuanza kwa mvua hizo.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Ladislaus Chang’a alisema utabili unaonyesha mvua zitakuwa juu ya wastani, huku akishauri sekta mbalimbali zijiandae kukabiliana na majanga.

“Mvua za vuli zinatarajiwa kuanza Oktoba mwaka huu katika maeneo mengi nchini na zitakuwa za wastani na wastani wa juu itanyesha Pwani ya kaskazini na ukanda wa Ziwa Victoria,”alisema Dk Chang’a.

Maeneo mengine ni magharibi inayojumuisha mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara pamoja na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma (wilaya za Kakonko na Kibondo), ukanda wa pwani ya kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro, Pwani, Dar es Salaam, Tanga na visiwa vya Unguja na Pemba.

“Hivyo, Idara ya menejimenti ya maafa nchini inashauriwa kuendelea kuratibu utekelezaji wa mipango itakayosaidia kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza,” alisema Dk Chang’a.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi