Makala
Siri nyuma ya biashara za vipuri, vyuma chakavu
Dar/Arusha. Ni mtaa wenye pilikapilika, pikipiki zilizopakia watu wenye nguo zilizochafuka ‘grisi’ zinaingia na kutoka. Kuna biashara za vipuri vilivyotumika vya magari sambamba na vyuma chakavu na bei zake zinatajwa kuwa rafiki.
Hapa ni Tandale, jijini Dar es Salaam, lakini hali kama hii utaishuhudia pia katika mitaa mingi kama Manzese, Tabata Dampo, Temeke na kwingineko, vivyo hivyo eneo la Wakereketwa – Unga Limited jijini Arusha.
Mbali na biashara hii kushamiri, yapo maneno kuwa baadhi ya watu wanaofanya biashara hizi wanahusika pia katika wizi wa vipuri na magari, jambo linaloamsha shauku ya kuchunguza undani wa biashara hii.
James Muhinga, mkazi wa Msasani jijini Dar es Salaam anasimulia tukio lililomkuta la kuibiwa vioo vya pembeni (side mirror) za gari lake kisha baada ya miezi kadhaa alimkuta nazo mtu mwingine ambaye alidai amevinunua Manzese.
“Mwaka jana (2022) niliibiwa ‘side mirrors’ za gari langu na baada ya miezi kama minne hivi nilizikuta kwenye gari la mtu mwingine aliyedai amenunua Manzese,” anasema.
Kufuatia maelezo hayo, mwandishi wa Mwananchi aliamua kuweka kambi katika maeneo zinakofanyika biashara hizo jijini Dar es Salaam akichunguza namna zinavyofanyika na ikabainika kuwa wateja wengi hufuata bei ya chini ya vifaa hivyo.
“Hapa nikija ni fasta (haraka) tu napata spea ninayoitaka narudi zangu gereji, bei yao ipo chini sana,” anasema mteja mmoja aliyevaa nguo zinazoashiria kuwa ni fundi magari.
Pamoja na urahisi huo, Exaud Mbise, mfanyabiashara wa vipuri vilivyotumika na vyuma chakavu katika eneo la Manzese, anasema tuhuma za kuuzwa kwa vipuri vya wizi katika eneo hilo zipo na vitendo hivyo hufanywa na vijana ambao ni madalali.
“Hii kwetu ni ajira, lakini wapo vijana wasiokuwa waaminifu, hasa hawa wanaojifanya madalali (wasio na maduka), lakini unakuta wana mambo yao na wanauza vifaa vya wizi, hili pia ni tatizo,” alisema Mbise.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoa huo wa kipolisi, Mtatiro Kitinkwi, alisema “taarifa rasmi hatuna, lakini jukumu letu ni kulinda raia na mali zao, kama kuna madai ya eneo hilo kuwa na vifaa vya wizi na kutumika kama maficho ya wahalifu, tutayafanyia kazi.”
Pamoja na kauli hiyo, wananchi waliozungumza na Mwananchi, wameeleza kukerwa na biashara hiyo karibu na makazi yao, huku wakiiomba Serikali kuangalia namna ya kuwatafutia wahusika eneo litakalokuwa rafiki kwa ajili ya biashara hiyo.
Mbali na tuhuma za wizi wa vifa hivyo, kero nyingine inayotajwa na wakazi wa eneo hilo ni uchafuzi wa mazingira na kelele.
Mwanahamisi Hamza, mkazi wa Tandale ameshauri wafanyabiashara hao wahamishiwe mbali na makazi ya watu.
“Watu wengine wana watoto wachanga wengine wana wagonjwa, licha ya biashara hii kuwa ajira lakini kwetu imegeuka kero, isingepaswa kuwa katikati ya makazi ya watu, watafutiwe eneo la mbali,” alisema Hamza.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Obadia Shayo alisema licha ya kwamba biashara hiyo imeanza muda mrefu, kutokana na ongezeko la watu imeshakuwa hatarishi.
“Asilimia kubwa hapa watu wanaleta magari mabovu au yaliyopata ajali na kuja kuyakata, baadhi yanakuwa na mafuta na yanaweza kuwa hatari kwa sababu mara kadhaa milipuko hutokea,” alisema Shayo.
Kufuatia malalamiko hayo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mulhatan uliopo Manispaa ya Kinondoni ambapo pia biashara hiyo inafanyika, Sudi Makamba alisema biashara hiyo ilianza siku nyingi zaidi ya miaka 12 iliyopita na Serikali inafahamu kero zote zinazosababishwa na biashara hiyo.
“Kiufupi, ingawa mimi si msemaji, ila biashara hii inasababisha usumbufu mkubwa na Serikali inalifahamu hili,” alisema Makamba.
Hata hivyo, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge alipoulizwa kuhusu biashara hiyo alisema wananchi wenyewe wa maeneo hayo ndio chanzo cha biashara hizo kuendelea katika makazi ya watu baada ya wenye nyumba kuamua kubadilisha matumizi na kuwapangisha wafanyabiashara hao.
“Wananchi wenyewe ndio waliobariki kuwa sehemu ya tatizo, wenye nyumba ndio wameruhusu, tumejaribu kupambana, nao wanapambana na sisi.
“Tulitengeneza njia za watembea kwa miguu, wapo watu wamegeuza sehemu za biashara, hivi karibuni tutaanza operesheni ya kuwaondoa, kama mtu amepangishwa aache njia ya watembea kwa miguu wazi, atakayekamatwa hatua za kisheria zitachukuliwa,” alisema Mnyonge.
Jinsi inavyofanyika
Wafanyabiashara hao wa vipuri na vyuma chakavu, wanaeleza kuwa magari wanayokata huyanunua baada ya kupata ajali kutoka kwenye kampuni mbalimbali za bima na kwa watu binafsi.
“Tunanunua magari mabovu… mengi yanakuwa hayatembei, tunayavuta mpaka hapa. Tunafungua vifaa tunauza dukani kama vipuri vilivyotumika na sehemu zilizobaki tunaziuza kama vyuma chakavu.
“Bei ya gari moja iliyotumika tunanunua kutokana na hali yake kuanzia Sh2 milioni hadi Sh3 milioni. Watu wa bima wanaziuza gari kwa bei ndogo (bei za kutupa), hapo ndo watu wengi wanaziuza pale Manzese kwa ajili ya vipuri,” anasema Mrisho Mbega, mfanyabiashara wa magari yaliyotumika jijini Dar es Salaam.
Ni makubaliano
Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira), Hadija Maulid alipoulizwa kuhusu utaratibu wa kuuza magari yaliyopata ajali, alisema “hapa huwa ni makubaliano kati ya mteja na kampuni ya bima husika. Gari linapoharibika na likawa halifai kabisa, kampuni husika huingia makubaliano na mteja na hapa gari hili hufutwa kabisa kwenye orodha ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),” alisema Hadija.
Alibainisha gari hilo linapofutwa TRA, ina maana halifai tena, hivyo huuzwa kama mali chakavu ambayo itatumika kwa ajili ya vipuri au vyuma chavu kwa kuwa gari linapoharibika si vifaa vyote vinavyoharibika.
Udhibiti vyuma chakavu
Mwaka 2021 aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla alitangaza kuwaondoa wenye gereji bubu wote kwenye maeneo yasiyo rasmi, ikiwamo wanaofanya shughuli hiyo pembezoni mwa barabara na juu ya mifereji.
Makalla alieleza hayo wakati akizungumza na wananchi wa Jimbo la Kinondoni, akibainisha kuwa biashara hizo kwenye maeneo ya hifadhi za barabara zimekuwa chanzo cha uchafuzi wa mazingira.
Alibainisha kuwa suala la kuwatafutia maeneo mengine haliwezekani na kuwataka walioziba njia za watembea kwa miguu, ikiwa ni pamoja na wenye gereji bubu kuondoka ili kupisha maeneo hayo kuwa wazi.
Mpango huo wa Makalla bado haukufua dafu katika Jiji la Dar es Salaam lenye wakazi milioni 5.4, kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
Kuhusu udhibiti wa uchafuzi wa mazingira na kelele unaosababishwa na biashara hiyo ya vyuma chakavu kama inavyolalamikiwa na wananchi, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 vifungu namba 133 hadi 139 pamoja na kanuni za usimamizi na udhibiti wa taka hatarishi za mwaka 2009, vinapiga marufuku suala hilo.
Katika moja ya machapisho, Mkurugenzi Uzingatiaji na Uteketezaji wa Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC), Redempta Samwel, anabainisha mikakati ya kudhibiti na kuboresha biashara hiyo.
Mikakati hiyo ni pamoja na kukuza uelewa wa wadau kwenye masuala yanayohusu usimamizi na udhibiti wa taka hatarishi ili kulinda afya za binadamu na mazingira na kuleta maendeleo endelevu.
“Wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara ya ukusanyaji, usafirishaji na urejeleshaji na uteketezaji ni lazima kuwa na kibali kutoka mamlaka husika kama Sheria ya Mazingira 2004 inavyotaka,” linabainisha andiko hilo.
Kanuni zilizomo kwenye kanuni hizo, zinapiga marufuku kibali cha mfanyabiashara mmoja kutumiwa na mtu mwingine, kuimarisha uzingatiaji na utekelezaji wa sheria zinazohusu taka hatarishi.
Tanzania imeridhia na kusaini mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda ya mazingira, ikiwemo Mkataba wa Basel unaohusu usafirishaji wa taka hatarishi baina ya nchi na nchi na utupaji wake; na mkataba wa Bamako unaozuia uingizaji wa taka hatarishi katika nchi za Afrika.
Uuzwaji nje ya nchi
Licha ya malalamiko ya uchafuzi wa mazingira na kuwa maficho ya wahalifu, biashara ya vyuma chakavu kwa upande mwingine, inatajwa kusaidia katika usafi wa mazingira kwa kufanya urejelezaji wa taka hatarishi na uuzwaji wa bidhaa hizo nje ya nchi.
Utafiti uliofanywa na wanazuoni Clashon Onesmo, Edmund Mabhuye na Patrick Ndaki wenye kichwa cha habari, Uhusiano kati ya usimamizi endelevu wa taka ngumu na hali ya uchumi katika miji ya Tanzania: Biashara ya vyuma chakavu Arusha ya mwaka 2023, umebainisha hilo pia.
“Biashara ya vyuma chakavu huchangia katika urejelezaji, kurekebisha hali ya hewa, kukuza uchumi na kuboresha maisha. Kwa hivyo, tunatoa wito kwa ajili ya maendeleo endelevu na mfumo wa usimamizi wa taka ngumu uboreshwe ili ulete tija ya kimazingira na kiuchumi,” imebainisha sehemu ya majibu ya utafiti huo.
Suala hilo halijazungumziwa tu na wanazuoni hao, hata ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2021, inaonyesha Tanzania ilisafirisha nje ya nchi kilo milioni 8.01 za vyuma chakavu na kuingiza Sh4.6 bilioni, na nchi zinazoongoza kununua bidhaa hizo ni India, ikifuatiwa na Kenya na Ujerumani.
Utafiti wa vyuma chakavu Arusha mwaka 2023 unaonyesha zaidi ya tani 314 za chuma chakavu ziliuzwa kila mwezi jijini hapo.