Kitaifa
Utata matibabu bure wajawazito
Dar es Salaam. Baadhi ya wananchi wametofautiana na msimamo wa Serikali kwamba huduma kwa wajawazito ni bure, wakieleza wamekuwa wakitozwa fedha kuchangia matibabu.
Kauli hiyo wameitoa kwa nyakati tofauti baada ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kutoa tamko juzi akizungumzia tukio la kifo cha mjamzito na mtoto wake kilichotokea Wilaya ya Handeni mkoani Tanga Novemba 11, mwaka huu, katika Kituo cha Afya Kabuku kwa kinachodaiwa kutokana na uzembe wa watumishi wa kituo hicho.
Ndugu wa mjamzito huyo walidai walitakiwa kulipa Sh150,000, fedha ambazo familia hiyo haikuwa nazo, hivyo kusababisha kukosa huduma.
Alipotafutwa jana kuzungumzia utozwaji wa gharama, Mkurugenzi Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto wa Wizara ya Afya, Dk Ahmed Makuwani alisema taarifa rasmi ilishatolewa na Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu, hivyo hawezi kuzungumza tofauti na taarifa hiyo ambayo ndiyo msimamo wa Serikali.
Waziri Ummy katika tamko lake juzi kupitia mtandao wa X aliwataka watumishi wa afya nchini wafanye kazi kwa kuzingatia maadili ya taaluma zao na sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Ingawa hakuzungumza kuhusu utoaji huduma bure kwa wajawazito katika tamko lake, Sera ya Afya ya Juni, 2007, kuhusu afya ya mama na mtoto inasema:
‘‘Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inayotoa huduma bila faida na mashirika ya kimataifa, itaendelea kutoa huduma bila malipo kwa wajawazito, watumiaji wa huduma za uzazi wa mpango na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.’’
Kuhusu msamaha wa uchangiaji gharama huduma za afya kwa makundi maalumu, sera inaeleza Serikali inatambua kuwepo kwa wananchi wasio na uwezo wa kuchangia gharama za huduma za afya, ikiwa ni pamoja na wale walio katika makundi maalumu ya kijamii. Miongoni mwa wanaotajwa ni wajawazito.
Maoni ya wananchi
Ndugu na wajawazito waliozungumza na gazeti hili jana, baadhi wakiwa maeneo ya hospitali wameeleza wamekuwa wakitozwa fedha kwa huduma za kujifungua.
Aisha Athuman, aliyempeleka mwanawe kujifungua katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke alisema kujifungua kwa njia ya kawaida unalipia Sh85,000.
“Gharama hizi hazijumuishi gharama ya vifaa ambavyo mjamzito anapaswa kuingia navyo chumba cha uzazi ikiwemo pamba na glovu,” alisema Aisha.
Naye Fatuma Mbega, mkazi wa Temeke alisema: “Nimejifungua mwezi uliopita nimelipa Sh95,000. Rafiki yangu amejifungua juzi kalipa Sh70,000, sasa sijui wanaangalia sura au wanakadiria kila mmoja na gharama zake.”
Licha ya kuwapo bango linaloonyesha gharama za huduma kwa wanaojifungua hospitalini hapo, kumekuwa na mabadiliko ya kulipa malipo kwa kila anayekwenda kujifungua.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Temeke, Dk Joseph Kimaro alisema kutofautiana kwa gharama kunategemea huduma aliyopatiwa mgonjwa.
Naye Johnson Njari, alisema mkewe amejifungua kwa upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana, ambapo aliambiwa alipie Sh200,000 na dawa Sh49,000.
“Nilielekezwa dirisha la kulipia na nimelipia kihalali kabisa na risiti nimepewa, nilishuhudia mama mmoja akizuiwa kuondoka wodini baada ya ndugu zake kushindwa kulipa gharama za matibabu,” alisema.
Dareen, mkazi wa Ilala aliyekwenda kumfuata wifi yake Hospitali ya Amana alisema alipewa karatasi ya malipo ya gharama ya Sh70,000 ambazo alilipa na waliruhusiwa kuondoka.
“Nimefika hapa wifi yangu kaniambia nikalipie gharama hiyo la sivyo hawezi kuruhusiwa, nikaenda kwenye dirisha la malipo nikapewa namba ya kulipia na hapa tunaondoka,” alisema.
Mkazi wa Kigamboni aliyejitambulisha kwa jina la Alawi alisema kuna haja ya Serikali kuzungumza ukweli kuepusha migogoro ya ndugu wa mgonjwa na wahudumu kutokana na uwepo wa kauli ya huduma bure.
“Tumempeleka ndugu yetu hospitali ya Vijibweni, Kigamboni wametutoza Sh40,000 kujifungua kawaida. Tumeambiwa na mgonjwa wetu kwa upasuaji wanatoza kuanzia Sh100,000,” alisema Alawi.
Zainab Shaban, mkazi wa Mbagala alisema alitoa Sh110,000 katika Hospitali ya Mbagala Zakhiem baada ya kufanyiwa upasuaji. Alisema gharama za kujifungua kawaida ni Sh35,000 zinazoelezwa ni gharama ya dawa.
“Wangeweka wazi gharama tunazotakiwa kutoa, sikujua kama kuna gharama hadi nilipokuwa natoka. Niliambiwa kama sina pesa siwezi kutoka hadi nilipe na si mimi tu wapo wengine wametozwa fedha za dawa,” alisema.
Akizungumzia gharama alizotumia kwa mkewe kujifungua kwa upasuaji katika kituo cha afya Kimara, Harif Musa alisema alitumia zaidi ya Sh170,000 ambazo alinunua vifaa tiba na dawa.
Katika Kituo cha Mnazi Mmoja, Saida Hussein alisema amejifungua kwa upasuaji na amelipa Sh105,000.
“Ninavyofahamu kujifungulia hapa ni bure, ukiwa na changamoto unapewa rufaa kwenda Amana ila wapo wanaotoa asante kwa manesi. Mimi nimelipa Sh105,000 kwa sababu nimefanyiwa upasuaji na mtoto amepata changamoto napelekwa Amana,” alisema Saida.