Makala
Sababu wenye kipato kidogo kuongoza kwa ndoa za mitala
Dar es Salaam. Wanawake na wanaume wasiokuwa na elimu na wanaoishi kwa kipato cha chini, ndio wanaoongoza kuwa na ndoa za mitala ikilinganishwa na wasomi, ripoti ya utafiti inaeleza.
Hata hivyo, Kadhi Mkuu wa Dar es Salaam, Sheikh Ramadhani Kitogo alisema hakubaliani kuwa watu wenye kipato cha chini ndio wanaongoza kuoa mke zaidi ya mmoja.
Alisema anachofahamu ni kuwa wanaooa mke zaidi ya mmoja wanafuata maelekezo ya dini yaliyowaruhusu kufanya hivyo.
“Kusoma au kutosoma, kuwa na kipato kidogo inategemea na sehemu waliyopo, kuna waliosoma na wana kazi nzuri na wameoa mke zaidi ya mmoja, mimi mwenyewe nina mke zaidi ya mmoja na wamesoma,” alisema.
Alisema anachofahamu kwa watu wa kipato duni, hofu ya kuolewa ndoa za mitala imekuwa kubwa zaidi ya wale wenye kipato bora kila wanapofikiria maisha ya baadaye.
“Kila akifikiria watoto, hali yangu duni niliyonayo, mtoto hajasoma, hajala, hajaenda hospitali, hajapata mahitaji, wanakuwa na hofu zaidi na ndoa hizi kuliko wenye kipato,” alisema Kitogo.
Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria (TDHS-MIS) ya mwaka 2022 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza ndoa za mitala zimekuwa zikipungua kulingana na kiwango cha elimu na hali ya maisha.
Jambo hilo linatajwa na wadau kuwa linachangiwa na mila na desturi zilizopo katika jamii, kutokujitambua na kutafuta ahueni ya maisha kwa baadhi ya watu bila kuangalia athari za mbele.
Uchambuzi wa ripoti unaonyesha asilimia 26 ya wanawake wasiokuwa na elimu wameolewa katika aina hiyo ya ndoa ikilinganishwa na asilimia tisa ya wanawake wenye elimu ya sekondari na zaidi.
Hilo linaenda sambamba na kiwango cha kipato cha watu, ikionyesha ni asilimia nane pekee ya wanawake wanaoishi katika kaya za kipato cha juu ndio wenye wake wenza ikilinganishwa na asilimia 24 ya wanawake walioolewa katika kaya za kipato cha chini.
Licha ya kuwapo kwa takwimu hizo, kwa jumla, kiwango cha wanawake walio na wake wenza kimepungua kutoka asilimia 21 katika utafiti uliofanywa mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 15 katika utafiti wa TDHS-MIS wa mwaka 2022.
“Kwa jumla, wanawake walio na umri mkubwa ndio walikuwa wakikubaliana na kuolewa mke wa pili kuliko wale wenye umri mdogo,” inaeleza sehemu ya utafiti.
Jambo hilo linashuhudiwa na Asha Juma (si jina halisi) anayeeleza alitishia kuiacha ndoa baada ya mume kutaka kuoa mke wa pili.
“Ndoa ndiyo ilikuwa na miaka mitatu, nilipojifungua akataka kuongeza mke mwingine, nikaona nikikubali hili akija mwingine naye akiwa mjamzito ataongezwa mwingine, mimi mwenyewe bado mdogo,” alisema Asha, licha ya dini yake kuruhusu mke zaidi ya mmoja.
Wakati Asha akisema hayo, takwimu zinaonyesha upande wa wanaume, kiwango cha walio na mke zaidi ya mmoja kimepungua kutoka asilimia 10 hadi asilimia sita katika kipindi kama hicho.
Ndoa za aina hii pia zinakubalika zaidi vijijini kuliko mijini, takwimu zikionyesha asilimia 18 ya wanawake waishio vijijini wako katika ndoa za mitala ikilinganishwa na asilimia tisa ya wale wa mjini.
Wanaume waishio vijijini, wasio na elimu na wanaotoka kaya masikini pia wanapenda kuwa na mke zaidi ya mmoja.
Leah Kassim (si jina halisi) alisema akiwa katika umri wa kuolewa alipata mwenza ambaye walikubaliana kuanza maisha, lakini baadaye aligundua ni mume wa mtu.
“Lakini dini yetu inaruhusu, nilikuwa nimemaliza chuo na tayari nafundisha (mwalimu), ilibidi niongee na mama, nikamuelezea. Swali la kwanza lilikuwa ni kuhoji ikiwa mi mjamzito,” alisema Neema.
Alisema haikuwa rahisi kumshawishi mama yake kwa kuwa hakuamini kama ndoa yake ingefanikiwa kwa kike alichokieleza kuwa ni ushuhuda wa ndoa nyingi za aina hiyo zilizokwama.
“Baba ndiyo alinisaidia, mwisho akasema yakikushinda urudi hapa ni kwenu, ila sasa ni mwaka wa 10 tuna watoto wawili maisha yanaendelea,” alisema Leah.
Masanja Bokobora (31), mkazi wa kijiji cha Mwabalebi wilayani Meatu ambaye ana mke mmoja alisema nia yake ni kuongeza wake wengine, lakini hajafanya hivyo kwa sababu ya kutokuwa vizuri kifedha.
“…pamba haitoki sana na mahindi pia, lakini nimeshapanga nitaongeza mke kwa sababu mashamba yapo na Mungu atajalia chakula kitapatikana,” alisema Bokobora, mwenye watoto wanne.
Wasemavyo wadau
Oscar Mkude, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uchumi alisema wakati mwingine wanaume wanaoishi vijijini wamekuwa wakioa ndoa za mitala kwa lengo la kuongeza nguvu kazi ambayo itasaidia katika uzalishaji mali.
“Mtu anaona tukiwa watatu au tukiwa wangapi tunaweza kulima kwa kiasi hiki tukafanya uzalishaji kuongezeka, hii ni tofauti na ndoa za mitala za mijini ambazo mara nyingi si rasmi na wanaume huwa wanatafuta ahueni kulingana na yale wanayopitia,” alisema Mkude.
Alisema watu wasiokuwa na elimu na wenye kipato cha chini wanaonekana kuongoza kuwa na ndoa za mitala kwa sababu mara nyingi hupata wale walio na sifa kama zao, kama ni kipato au kiwango cha elimu.
Neema Mwankina, mwanasaikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) alisema kutokujitambua, mila na desturi za jamii waliyopo ndiyo jambo ambalo limekuwa likichochea kuwapo kwa ndoa za mitala.
Alisema baadhi ya wanawake wamekuwa wakiolewa si kwa ajili ya kutimiza ndoto zao, bali kwa ajili ya kupata ahueni ya maisha kutoka kwa wanaume watakaowaoa bila kuangalia mbele itakuwaje.
“Wakati mwingine ni wazazi wasiokuwa na uelewa wa kutosha, wakiona mwanamume amekuwa akiwasaidia mahitaji madogo madogo ya nyumbani wanaona bora tu waruhusu binti yao aolewe, bila kujali nini kitamkuta mbele,” alisema Neema.
Mila na desturi zilizopo katika baadhi ya maeneo pia zimefanya ndoa za mitala kuonekana ni jambo la kawaida, kwa kuwa historia zinazokuwapo kwa ndoa hizo kuendelea vizazi na vizazi zimekuwa zikifanya zionekane ni jambo la kawaida.
“Kikubwa wanawake wanapaswa kutambua kuwa wanatakiwa kutimiza ndoto zao, wasiolewe kwa sababu watasaidiwa chakula na unga, bali kwa kuangalia mtu anayeenda kuishi naye atamsaidia vipi kutimiza malengo yake,” alisema Neema.
Alisema katika dini ya Kiislamu pia jambo hilo limeruhusiwa kisheria, huku akieleza kwa Wakristo ambao wanaruhusiwa kuwa na mke mmoja, wengi wao wamekuwa na ndoa za mitala zisizokuwa rasmi hadi linapotokea tatizo ndipo mke atajua kuwa hayupo peke yake.