Connect with us

Kitaifa

Kiama cha wasanii ‘mateja’ chanukia

Dar es Salaam. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imewaonya wasanii wanaojihusisha na dawa za kulevya, ikisema imejipanga kuwashughulikia.

Mbali ya wasanii, mamlaka imewaonya wananchi wote ambao kwa nafasi zao wanazitumia kuhamasisha dawa za kulevya, ikiwataka waache.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alitoa onyo hilo jana jijini hapa katika semina kwa wahariri wa vyombo vya habari iliyoandaliwa na mamlaka hiyo ikilenga kuwajengea uelewa kuhusu utendaji kazi wake. Alisema mamlaka ina orodha ya wasanii wanaotumia dawa za kulevya.

“Wapo wasanii wanaotumia cocaine tunayo orodha yao, wapo wanaotumia heroine tunayo orodha yao na wapo pia wanaotumia bangi. Tunawapa muda wa kujirekebisha. Mitambo yetu ikikamilika tutaanza ku-deal nao (kuwashughulikia),” alisema.

Alisema wasanii hao wanaihamasisha jamii kwa kutumia nyimbo zao, mavazi yao yanayokuwa na majani ya bangi, maneno na matendo yao, ambayo yanaonyesha dhahiri kwamba wanatumia dawa za kulevya.

“Kwa nini hatufanyi hivyo sasa wakati sheria inaturuhusu, ni kwa sababu tulikuwa hatujakamilisha ujenzi wa maabara yetu, ukikamilika tutaanza kuwashughulikia wote,” alisema.

Lyimo alisema anayehamasisha atakamatwa na kwenda kupimwa na iwapo atagundulika anatumia dawa za kulevya atafikishwa mahakamani kwa sababu sheria inaruhusu hilo kufanyika.

“Akishahukumiwa miaka mitatu jela kama vipimo vitathibitisha kwamba amekuwa mraibu, pia atapatiwa huduma ya dawa ili aondokane na matumzii ya dawa za kulevya,” alisema.

Alisema walishafanya mawasiliano na Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) kuhusu wasanii wanaohamasisha dawa za kulevya, hivyo hawatajali ukubwa wa msanii yeyote bali watawashughulikia.

“Wasanii ni kioo cha jamii wanatakiwa wapeleke ujumbe mzuri kwa jamii, lakini baadhi yao wanatumia dawa za kulevya na wengine wanashawishi wenzao,” alisema.

Alitoa wito pia kwa wananchi wote ambao kwa nafasi zao wanazitumia kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya, akiwaomba waache kufanya hivyo.

“Kuanzia sasa wale wote watakaokuwa wanahamasisha dawa za kulevya ikiwemo kwa mavazi, maneno na kwa kutumia majukwaa yao, pia tutachukua hatua ikiwa ni pamoja na kuwapima kuhakikisha kama wao wanatumia dawa wanazohamasisha, tukikuta wanatumia sheria itachukua mkondo wake,” alisema.

Lyimo alisema kwa sasa wametoa onyo, lakini baada ya kukamilika maabara ya mamlaka watafanya ukamataji wa wote wanaohamasisha matumizi ya dawa za kulevya.

Mjadala kuhusu bangi

Akizungumzia mjadala kwa nini bangi isiruhusiwe ambao umekuwapo kwenye mitandao ya kijamii na hata bungeni kwa baadhi ya wabunge kutaka Tanzania iruhusu matumizi yake ili kuongeza mapato, alisema:

“Kwa sheria haiwezi kuruhusiwa, bado udhibiti wake kwa nchi zilizoruhusu haujawa mzuri.”

Alisema bangi inayokamatwa nchini inatoka kwenye nchi zilizoruhusu kilimo cha dawa hizo za kulevya na kwamba, zinakabiliwa na matatizo ya usalama, mauaji na hata vita.

 

Mwandishi matatani

Pia alisema watamtafuta mwandishi wa habari wa kituo kimoja na kumpima kwa kuwa amejitangaza kuwa anatumia dawa za kulevya na ikithibitika anazitumia atachukuliwa hatua za kisheria.

Lyimo alisema mwandishi huyo alikuwa akijadili taarifa ya mamlaka kwamba ubongo ukiathiriwa na dawa za kulevya mtu huanza kuona vitu visivyoonekana.

Mwandishi huyo katika mjadala kwenye chombo chake cha habari alisema yeye anatumia lakini hajaona vitu hivyo.

“Ipo sheria inaruhusu, kwa kuwa amejitangaza mwenyewe, huo pia ni uhamasishaji wa matumizi ya dawa za kulevya,” alisema Lyimo.

Kemikali bashirifu

Katika semina hiyo ya siku mbili, mada sita zilijadiliwa ikiwamo kuhusu kemikali bashirifu na udhibiti wake, ambazo mbali ya matumizi mengine ya kawaida, huchepushwa na kutumika kutengeneza dawa za kulevya, ikiwamo heroine.

Kamishna msaidizi wa ukaguzi na sayansi jinai wa DCEA, Ziliwa Machibya, alisema pasipo kemikali bashirifu hakuna dawa za kulevya, hivyo mamlaka inafanya kazi ya kuzidhibiti.

Alisema uchepushaji wa kemikali bashirifu hufanyika wakati wa ununuzi, usafirishaji, uteketezaji na uzalishaji. Alitoa mfano wa kemikali itumikayo kutengeneza dawa ya kikohozi ambayo iliwahi kuchepushwa kwa kuwekwa kiwango kidogo kwenye dawa hiyo, hivyo walilazimika kufuatilia kujua nyingine ilikwenda wapi.

Kemikali bashirifu ni zile zenye matumizi ya kawaida katika kutengeneza bidhaa mbalimbali viwandani, lakini zikichepushwa huweza kutumika kutengeneza dawa za kulevya.

Machibya alisema pia kuna dawa tiba ambazo huchepushwa kutoka kwenye matumizi ya kawaida na kupelekwa kwenye matumizi ya dawa za kulevya, zikiwamo dawa za usingizi kama vile valium.

“Kwa nini ununue dawa ya usingizi, mwili wako umeumbwa vizuri umekamilika unapoongezea kingine ndani unaharibu, hivyo tunadhibiti vitu hivyo kwa kuwa havitakiwi kufanyika,” alisema.

Kwa upande wake, Kamishna wa huduma za kinga na tiba wa mamlaka hiyo, Dk Peter Mfisi, akizungumzia afya ya akili na dawa za kulevya, pamoja na tiba kwa waraibu, alisema DCEA kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), zimetia saini makubaliano ya kushirikiana kutoa elimu kwa wanafunzi.

Alisema kupitia klabu za kupinga rushwa, sasa zitahusika pia katika kupambana na matumizi ya dawa za kulevya, lengo likiwa kuwapatia stadi wanafunzi ili kujiepusha na matumizi ya dawa hizo. Kuhusu waraibu wanaotumia dawa ya ‘methadone’, alisema mkakati unaandaliwa kuwawezesha baada ya kupona wajifunze ufundi ili waweze kujipatia kipato.

Dawa mpya za kulevya

Naye Kamishna Msaidizi wa Kinga na Huduma za Jamii wa DCEA, Moza Makumbuli, alisema hivi sasa kuna dawa mpya za kulevya ambazo hutengenezwa katika maabara na haziko kwenye udhibiti chini ya mikataba ya kitaifa na kimataifa.

Dawa hizo zinaweza kusababisha madhara makubwa kwa afya ya mtumiaji, zinafahamika kama dawa za kulevya zikiwa zenyewe au katika mchanganyiko na dawa nyinginezo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Dk Rose Reuben, alisema: “Dawa za kulevya zina madhara makubwa kijamii, kiuchumi na hata kisiasa. Wanawake ndiyo huathiriwa zaidi.’’

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi