Kitaifa
Mafuriko Jangwani mfupa mgumu kwa Serikali
Dar es Salaam. Safari ya kusaka suluhu ya mafuriko eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam, inaonekana kuwa mfupa mgumu uliowashinda viongozi wengi, baada ya ahadi na hatua walizowahi kutangaza kukosa matokeo chanya.
Historia ya janga la mafuriko eneo hilo ina miongo kadhaa, huku vifo na familia kuachwa bila makazi.
Kukithiri kwa mafuriko kulisababisha Serikali ya awamu ya nne, mwaka 2010 kuamua kuwahamishia Mabwepande wakazi wa eneo hilo, ingawa wengine waligomea uamuzi huo.
Mgomo wao uliisababisha Serikali kusaka mbinu za kudhibiti mafuriko katika eneo hilo na ndipo mwaka 2011, Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete alipokuja na mpango wa kusafisha Mto Msimbazi.
Uamuzi huo ulitokana na alichoeleza kuwa, wananchi wamegoma kuhama angalau mto usafishwe kuruhusu maji yapite bila usumbufu.
Mpango huo nao haukufua dafu, mafuriko yaliendelea kushuhudiwa Jangwani, huku kila kiongozi akizungumza lake bila kupata utatuzi wa tatizo.
Baadaye mwaka 2018, aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango aliutaarifu umma juu ya kupatikana suluhu ya kudumu.
Dk Mpango alisema Benki ya Dunia (WB) imekubali kufadhili maboresho ya Bonde la Mto Msimbazi yatakayohusisha ujenzi wa Daraja la Jangwani.
Mwaka mmoja baadaye, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alitangaza kujengwa daraja hilo ingawa hakufafanua kwa kina kuhusu utekelezwaji wa mradi huo.
Desemba 2020, Mfuko wa Barabara ulitangaza utayari wa kupitisha Sh4 bilioni kwa ajili ya kugharimia ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 300 eneo la Jangwani.
Kabla ya mpango huo kutekelezwa, Novemba 2022, Serikali ilisema ujenzi wa Daraja la Jangwani utatekelezwa, hivyo mikataba ya mradi huo kati yake na WB ilisainiwa.
Juzi, katika eneo hilo kumeshuhudiwa mafuriko tena yaliyosababisha kukwama kwa shughuli za usafiri na usafirishaji kwa watumiaji wa Barabara ya Morogoro kutoka na kuingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Suluhu ya kudumu
Akizungumza na Mwananchi jana, mratibu wa mradi wa Bonde la Mto Msimbazi, Nyariri Nanai alisema kutekelezwa kwa mradi katika bonde hilo ndiko kutaleta suluhu ya kudumu ya changamoto hiyo.
Alisema mradi huo unatekelezwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).
Katika mradi huo, Nanai alisema Tamisemi itahusika na ujenzi wa maeneo salama ya kuishi na maeneo ya burudani, huku Tanroads ikihusika na ujenzi wa daraja kutoka Magomeni Mapipa hadi Faya.
Nanai alisema fedha za kutekeleza mradi huo Dola 260 milioni za Marekani (Sh651.3 bilioni) kutoka Benki ya Dunia, Serikali ya Uholanzi na Hispania, zimeshapatikana na mchakato wa utekelezaji wa mradi husika umeanza.
Nanai alichanganua fedha hizo akisema, Benki ya Dunia imetoa Dola 200 milioni za Marekani (Sh501 bilioni) ambazo ni mkopo, Serikali ya Hispania Dola 30 milioni za Marekani (Sh75.15 bilioni) za mkopo na Uholanzi imetoa Dola 30 milioni za Marekani ambazo ni ruzuku.
“Kwa sasa tupo katika hatua ya fidia na tunatarajia kuanza kuitoa Jumatano (Novemba 15, mwaka huu) baada ya hapo tutatangaza zabuni kumpata mkandarasi,” alisema Nanai.
Alisema kazi zitakazotekelezwa na Tamisemi mbali ya ujenzi wa maeneo ya burudani ni kuongeza kina cha mto kwa kuondoa mchanga na udongo utakaohifadhiwa kwa ajili ya shughuli nyingine.
Nanai alisema Desemba mwaka huu hatua ya ununuzi itaanza na hadi Aprili mwakani, mkandarasi atakuwa amepatikana kwa ajili ya kazi hizo.
Kuhusu ujenzi wa daraja, alisema Tanroads wameshatangaza zabuni na kupata mkandarasi. Alisema Januari mwakani ataanza ujenzi.
“Hakuna suluhu nyingine zaidi ya mradi huu, hizi shughuli zinazofanywa sasa ni kupanua mto ili kurahisisha maji yapite, kwa sababu changamoto kubwa ya jangwani ni mto kujaa mchanga,” alisema.
Alisema upanuzi wa mto unaofanywa na Tanroads ikiwa ni hatua za muda mfupi, zinalenga angalau kupunguza kiwango cha athari.
“Kazi inayofanywa sasa ni hatua za muda mfupi kupunguza kiwango cha athari nyakati za mvua, inafanywa na Tanroads, wakati kuna suluhu ya kudumu inaendelea,” alisema Nanai.
Kauli ya Waziri
Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa alipotembelea eneo hilo jana, alieleza kusudio la Serikali kufumua ramani ya ujenzi wa daraja hilo.
Uamuzi huo unatokana na kile alichofafanua kuwa, ramani iliyopo isingeweza kuleta suluhu ya changamoto hiyo.
Bashungwa alisema itachorwa mpya kwa ajili ya kufanikisha hilo na uamuzi huo umetokana na ushauri wa Rais Samia Suluhu Hassan ili kupata ufumbuzi wa kudumu na kuondoa tatizo hilo linalojirudia.
“Novemba 16, tutafanya kikao na mkandarasi anayetakiwa kujenga mradi huu, kupitia upya ramani ya ujenzi ili tuje na nyingine. Tunatamani ianzie Magomeni hadi Faya ili kuondoa kabisa changamoto hii ya muda mrefu,” alisema Bashungwa.
Alisema mazungumzo hayo hayataathiri ujenzi uliotarajiwa kuanza Februari mwakani, isipokuwa kinachofanywa ni kuboresha ili athari zisijirudie.
“Pamoja na Serikali kuendelea kujenga miundombinu ya barabara na madaraja kukabiliana na athari za mvua zinazonyesha kutokana na mabadiliko ya tabianchi, tunavyoishi tunapaswa kuwa sehemu ya suluhu kwa kuacha kutupa takataka ovyo, chupa na mifuko ya plastiki,” alisema Bashungwa.
Kuhusu suluhisho la muda mfupi, alimtaka Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, John Mkumbo kuendelea kuondoa uchafu na mchanga katika mto huo ili maji yapite kwa urahisi.
“Najua umeripoti na hujamaliza hata mwezi, sasa kipimo chako cha kwanza ili niweze kujiridhisha kwamba unatosha ni hapa kwenye kuzibua tope kutoka katika daraja hili na wakandarasi wasiwe wavivu kwenye kutafuta suluhu,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Tamisemi Mohamed Mchengerwa aliwataka watendaji wa mikoa mbalimbali kuangalia athari za mvua katika maeneo yao.
“Wakati wa ukaguzi ni huu kwa sababu mvua zikinyesha ndizo zinazotuonyesha matobo yalipo. Tokeni maofisini mkaone changamoto zilizopo na mjipange kuona ni namna gani tutaweza kujenga barabara ambazo hazitaathiriwa na mvua,” alisema Mchengerwa.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila aliahidi kusimamia hatua ya kuondoa mchanga na taka katika mto huo ili kuruhusu maji yapite.
“Tutatoa elimu ya usafi wa mazingira ukiangalia daraja hili na siku mbili zilizopita kulikuwa na chupa na uchafu mwingi uliojaa ukionyesha kuna shughuli nyingi za binadamu zinafanyika,” alisema.
Maeneo mengine
Mkoani Arusha nako hali si shwari, baada ya mvua kusababisha vifo vya watu watano, kujeruhi sita huku wengine wakiachwa bila makazi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Salvas Makweli aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Living Shirima, Ally Abdi, Wilson Lesikar, Zamzam Masudi na Innocent Shirima.
“Hadi sasa waliopatikana ni hao, bado askari wetu wako kazini kuona kama kuna wengine, lakini hawa pia tupate taarifa zao vizuri, hivyo tunawaasa wananchi watoe taarifa wanapoona madhara mengine,” alisema Makweli.
Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji mkoa huo, Osward Manjejele alisema watu sita wameokolewa.
“Mbali na hao tumeokoa watu sita usiku wa saa saba katika maeneo mbalimbali. Niwaombe wana Arusha wachukue tahadhari kwa maisha yao hasa wanaoishi mabondeni,” alisema Manjejele.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella alisema kamati za maafa na ya ulinzi na usalama zinafanya tathimini kujua madhara zaidi ya mvua na taarifa rasmi itatolewa.
“Madhara bado ni makubwa na hatukutarajia, niombe wakazi wa Arusha wachukue tahadhari juu ya mvua zinazoendelea kunyesha. Pia, watoe taarifa juu ya mambo yote yanayotokea katika maeneo yao, maofisa wetu wanaweza kuwahi na kupunguza athari,” alisema.
Wasomi washauri
Kukithiri kwa matukio ya mafuriko, kunaonyesha kuna haja ya kupitiwa upya kwa mipango miji, kama anavyofafanua Mkurugenzi wa Taasisi ya Tathmini ya Rasilimali ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Pius Yanda.
Alisema shughuli hiyo ihusishe usanifu wa miundombinu inayotarajiwa na kuhakikisha ushirikishwaji wa wataalamu wa hali ya hewa katika kupanga na kutoa makadirio sahihi ya mabadiliko ya tabianchi katika siku zijazo.
“Hii ni muhimu kwa sababu mabadiliko ya hali ya hewa yapo hapa. Athari zinashuhudiwa zitakuwa kwa kiasi kikubwa baada ya muda,” alisema.
Baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam na wafanyabiashara walisema mvua imekwamisha baadhi ya shughuli zao kwa kiasi kikubwa, hivyo kuongeza wasiwasi wa kiusalama.
“Sisi wakazi wa mabondeni tunalala kwa wasiwasi tukihofia maji yasiingie majumbani mwetu, tunakaa usiku kucha tukijaza mchanga ili kuzuia mafuriko,” alisema Khadija Ali mkaazi wa Kawe Marani.
Dereva wa bodaboda, Omary Pambe alisema mvua inawakosesha abiria kwa sababu wateja wao wengi ni wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali ikiwamo Mwenge.
“Abiria ninaowapakia huwa wanafanya biashara Mwenge, mvua ikinyesha wanasema hakuna biashara, wanabaki nyumbani, abiria tunaowapata wanasema hatuna miamvuli, hawataki kupanda bodaboda tena,” alisema Pambe.