Connect with us

Kitaifa

Mageuzi ya historia katika sheria

Dodoma. Serikali imewasilisha bungeni muswada unaokwenda kutunga sheria mpya itakayoanzisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi itakayojitegemea kwa kuwa na muundo wa utumishi, kama lilivyo Bunge na Mahakama.

Sheria hiyo inakwenda kuondoa Sheria ya Uchaguzi iliyokuwapo tangu uhuru, huku Tume ya Taifa ya Uchaguzi ikiajiri watumishi wake, badala ya utaratibu wa sasa wa kuazima watumishi kutoka maeneo mengine.

Miswada iliyosomwa kwa mara ya kwanza bungeni jana ni wa Tume ya Uchaguzi, wa Mabadiliko ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani na wa Sheria ya Vyama vya Siasa.

Sheria mpya ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi itabainisha upatikanaji wa wajumbe wa tume, majukumu ya tume na uendeshaji wa shughuli za tume.

Sababu za mabadiliko hayo ni kuongeza uwazi katika utaratibu wa kuwapata wajumbe wa tume, ikiwamo utekelezaji wa maoni ya wadau wa uchaguzi kuanzia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, 2000, 2010, 2015 na 2020.

Pia, marekebisho hayo yanafanyika kwa kuzingatia uzoefu kutoka Zanzibar na nchi nyingine duniani.

Kuhusu kutungwa sheria moja ya uchaguzi, imeelezwa ni kutokana na kuwa na sheria mbili zenye maudhui yanayofanana zinazosimamia uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani. Sheria moja inasimamia uchaguzi wa Rais na wabunge, na ya pili inasimamia uchaguzi wa madiwani.

Mabadiliko haya yataondoa mkanganyiko kwa wadau wa uchaguzi katika kuzitumia sheria hizo mbili, hususan vyama vya siasa na watazamaji wa uchaguzi.

Serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa kuchapisha sheria zote mbili wakati wa uchaguzi.

Vyama vya siasa

Kuhusu maboresho ya Sheria ya Vyama vya Siasa, inagusa zaidi masuala ya jinsia na ujumuishaji makundi maalumu kutopewa kipaumbele inavyostahili katika shughuli za siasa.

Pia, kumekuwapo vitendo au lugha zinazochochea uvunjifu wa amani na kuhatarisha usalama wa nchi. Mfano, maneno ya kuhamasisha mapinduzi dhidi ya Serikali, vitendo vya kushambulia Jeshi la Polisi, kushambulia wanachama wa vyama vingine.

Maboresho mengine ni kuhusu uwepo wa vitendo vya ukatili wa jinsia katika shughuli za siasa na vitendo vya uvunjifu wa maadili katika shughuli za kisiasa. Mfano, matumizi ya lugha za matusi na udhalilishaji katika shughuli za siasa.

Wakurugenzi kusimamia uchaguzi

Sheria ya Msajili wa Vyama vya Siasa, imefanya maboresho kwa kufuta maneno “Executive Director” na District Administrative Secretary katika kifungu cha 7 (3) (b) badala yake kuweka maneno “Returning Officer” na kufuta maneno “Ward Executive Officer” katika kifungu cha 7 (3) (c) badala yake kuweka maneno “Assistant Returning Officer”.

Pia, sheria mpya inaboresha utaratibu wa kuchukua na kuwasilisha fomu za tamko la gharama za uchaguzi kwa kumtaka mtia nia kuchukua fomu za tamko la gharama za uchaguzi siku anayochukua fomu za kuomba uteuzi kwa msimamizi na kuweka muda wa chama cha siasa kuwasilisha ripoti ya marejesho ya gharama za uchaguzi katika uchaguzi mdogo.

Hali ilivyo sasa ni kuwa, kifungu cha 7(3)(b) kinaeleza mgombea ubunge anapaswa kuwasilisha timu ya kampeni kwa mkurugenzi wa halmashauri kwa Tanzania Bara na kwa Katibu Tawala wa Wilaya kwa Zanzibar na mgombea udiwani anapaswa kuwasilisha kwa ofisa mtendaji kata.

Utekelezaji wa suala hili umekuwa mgumu kwa sababu kuna wakati mkurugenzi wa halmshauri na katibu tawala wa wilaya wanakuwa si wasimamizi wa uchaguzi.

Maoni ya viongozi wa dini

Akizungumza na gazeti hili nje ya ukumbi wa Bunge jana, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima, alisema matumaini yao ni kwamba Kamati ya Bunge inayohusika na miswada itawashirikisha watu na wapigakura wa ngazi ya chini katika kupata maoni.

Kitima alisema kuwasilishwa kwa miswada hiyo, Watanzania watakuwa na imani kwamba chaguzi zijazo zitakuwa huru na haki.

“Huko nyuma tumeona tume inakuwa chombo cha Serikali, kwa kweli wakati mwingine inafanya kazi ya chama kinachoongoza nchi. Tanzania sasa inaenda kuondokana na tatizo hilo na tuna imani tutarejesha heshima ya Taifa letu kimataifa,” alisema na kuongeza:

“Nchi ambayo ilikuwa ina sifa kubwa ya kuwa na viongozi ambao wananchi wanawataka, mnaangalia uchaguzi uliofanyika wa Serikali za Mitaa mwaka 2019, vijiji vingi havikupatiwa viongozi waliowataka wananchi, waliwekewa viongozi.”

Padri Kitima alisema huwezi kuwa nchi ya vyama vingi, halafu Bunge likawa la chama kimoja na kwamba, kinachofanywa ni kurejesha matumaini ya wananchi kwa Serikali.

Aliwataka Watanzania kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kufanya mabadiliko ya kidemokrasia nchini.

“Tumuunge mkono katika mabadiliko haya, tushiriki kuhakikisha sheria itoke nzuri kwa kuwafanya Watanzania wachague viongozi wao, hasa kule chini, watu wasiwekewe viongozi wachague viongozi wao ndivyo watu wanavyofanya,” alisema.

Askofu wa Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza, akizungumza kwenye viwanja vya Bunge jana alisema Serikali imetekeleza ahadi ya kuwasilisha bungeni muswada wa mabadiliko.

“Sasa sijasoma content (maudhui) yenyewe, lakini, kwa kuitaja tu bungeni mimi kwangu nasikia faraja,” alisema.

Kwa upande wake, Askofu Emmaus Mwamakula wa Kanisa la Morovian la Uamsho Tanzania, alisema miswada hiyo ni hatua njema, lakini watashangilia kama imebeba maudhui muhimu waliyopendekeza.

“Kikubwa kinachotakiwa ni kwamba kila mtu anapogombea anapigiwa kura, kura ya mtu inahesabika na anatangazwa mshindi kwa kura alizozipata, kwa sababu sasa ukimpeleka mtu bila kupingwa tutakuwa na wabunge wengi au madiwani wengi au wenyeviti wa Serikali za Mitaa wengi ambao ni ‘incompetent’ (wasio na uwezo), hawana uwezo wa kufanya mambo,” alisema.

Kauli vyama vya siasa

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliiomba Serikali kuja na muswada wa nne wa marekebisho madogo ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kwa vyovyote vile tutahitaji mabadiliko madogo ya vifungu vya Katiba (Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) ili kuhakikisha miswada inakuwa na maana,” alisema na kuongeza:

“Kwa mfano, muswada wa Tume ya Uchaguzi. Tume imeanzishwa na ibara ya 74 ya Katiba, kwa hiyo namna gani wajumbe wa tume na mkurugenzi wa tume wanapatikana ni vizuri pia kwenda kuiangalia Katiba. Eneo la kupita bila kupingwa kuna baadhi ya vifungu vya Katiba lazima virekebishwe ili kuwezesha hilo la kupita bila kupigwa, liweze kuwa na msingi imara.”

Alisema wao kama wanasiasa wataendelea kuishawishi Serikali kuleta muswada wa nne wa mabadiliko madogo ya Katiba ili kuwezesha sheria zinazotungwa ziweze kuwa na maana.

Alisema baada ya muswada kusomwa kwa mara ya kwanza, kuna miezi mitatu ya kuijadili kabla ya kuwasilishwa tena bungeni Aprili mwakani.

“Kwa hiyo niwatake wadau wa demokrasia, vyama vya siasa, asasi zisizo za kiserikali na wadau wengine wote wa kidemokrasia, huu ndio muda sasa wa kuhakikisha tunashirikiana na Kamati ya Bunge ili kuweza kuboresha,” alisema.

Zitto pia alizungumzia kesi iliyofunguliwa Mahakama Kuu ya Tanzania na Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Joran Bashangwe kupinga kifungu cha sheria kinachoruhusu watu kupita bila kupingwa.

Alisema uamuzi wa Mahakama wa kumpa ushindi Bashangwe, Serikali pia imeheshimu na kuleta sheria hiyo bungeni kwamba kupita bila kupingwa ni kinyume cha Katiba.

“Na sasa kukiwa na mgombea mmoja kwenye uchaguzi basi mgombea yule apigiwe kura ya ndiyo au hapana, badala ya kutangazwa kwamba ameshinda, wakati labda wagombea wenzake waliondolewa kwa hila,” alisema.

Zitto alisema kupita bila kupingwa kulileta matatizo kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani.

“Humu ndani humu (bungeni) kuna wabunge 28 walipita bila kupingwa, hawakuchaguliwa na wananchi, watu wao ama wengine walinyang’anywa fomu au wengine walipotea,” alisema.

Makamu Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi (Bara), Joseph Selasini alisema miongoni mwa mapendekezo yao hayajahusishwa kwenye muswada kama lile la matokeo ya uchaguzi wa rais kupingwa mahakamani na ruhusa ya mgombea binafsi.

“Pia kuna lile la ili rais ashinde anapaswa kupata kura kuanzia asilimia 50 + 1, yaani zaidi ya asilimia 50,” alisema.

Kuhusu wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuomba kazi alisema: “Suala ni kwamba wajumbe ni kina nani, sisi tulipendekeza wajumbe watakaokuwa neutral (wasio na upande), unaweza kulishangilia hilo lakini ukakumbana na wajumbe watakaoleta jambo baya zaidi.”

Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema hakuwa tayari kueleza chochote kwa kile alichofafanua bado hajasoma miswada.

“Nikishasoma nitakuwa na nafasi nzuri ya kutoa maoni, kwa sasa bado,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano wa CUF, Mohammed Ngulangwa, alisema hatua ya kusomwa miswada hiyo ni zao la mashinikizo ya vyama vya upinzani juu ya kuandaliwa kwa mchakato wa demokrasia huru na ya haki.

Alieleza ili kufikia hatua hiyo, kulihitajika vyombo vinavyosimamia uchaguzi viwe huru na vitende haki, ndiyo sababu hadi sasa muswada huo umefika bungeni kusomwa.

Hata hivyo, alieleza hatua ya kusomwa kwa miswada hiyo ni jambo moja, lakini kilichomo ndani yake ni lingine.

Kauli za wabunge

Mbunge wa Mwanga (CCM), Joseph Thadayo alisema, “Muswada huu umezingatia hata maoni ya wale wasimamizi wa uchaguzi tangu mwaka 2015 mpaka hivi sasa. Pia umezingatia maamuzi mbalimbali ya Mahakama ambayo yametolewa. Kwa mfano, kulikuwa na kilio kuhusu mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi kuteuliwa na Rais.”

Alisema kwenye muswada pia kuna kamati ya usaili ambayo imeundwa, ambayo watu watakuwa wanapeleka maombi na watafanyiwa usaili, watateuliwa kwa mujibu wa vigezo ambavyo vitakuwa vimewekwa.

“Kulikuwa na maamuzi ya Mahakama Kuu ya Tanzania iliyotoa maamuzi kwamba haifai wakurugenzi wa halmashauri kusimamia uchaguzi, lakini sheria imeweka sifa, vigezo vya msimamizi wa uchaguzi na namna ambavyo atapatikana kwamba watakaopatikana sasa watakuwa wanafanya kazi chini ya sekretarieti ya tume ambayo ni sekretarieti huru kama ilivyo sekretarieti ya Tume ya Utumishi ya Mahakama, Tume ya Utumishi ya Bunge, kwa uhuru katika ngazi hiyo utakuwa umepatikana,” alisema.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Neema Lugangira alisema alishawahi kupendekeza Serikali ipeleke bungeni sheria ya usawa wa kijinsia bungeni.

“Sheria ya vyama vya siasa imeweka kifungu kipya, kifungu namba 10 (c) ambacho sasa kinaelekeza vyama vyote vya siasa katika kile ambacho kinafanya, lazima kizingatie masuala ya jinsia na ujumuishaji wa makundi maalumu,” alisema.

Alisema kifungu hicho kipya kitakwenda kuweka mazingira ya lazima kwa kila chama kiwe na sera, mipango na mikakati ambayo itakwenda kuongeza ushiriki na ushirikishwaji wa wanawake.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi