Kitaifa

TRAB na TRAT tena bungeni

Telegram

Dodoma. Serikali imesema hadi kufikia Oktoba mwaka 2023, ilikuwa na mashauri 889 yenye kiasi cha kodi kinachobishaniwa cha Sh6.46 trilioni na Dola za Kimarekani milioni 4.66.

 Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba ameyasema hayo wakati akijibu swali la msingi leo Ijumaa Novemba 10, 2023 akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Janejelly Ntate.

Mbunge huyo ametaka kufahamu ni lini Serikali itaweka mkakati maalum wa kumaliza mashtaka katika Bodi na Mahakama za Rufaa za Kodi (TRAB) ili Serikali na wafanyabiashara wapate stahiki zao.

Akijibu swali hilo, Dk Mwigulu amesema hadi Oktoba 2023, ilikuwa na mashauri 889 yenye kiasi cha kodi kinachobishaniwa cha Sh6.46 trilioni na Dola za Kimarekani milioni 4.66.

Amesema katika kipindi hicho, bodi imesikiliza mashauri 167 yenye kiasi cha kodi kinachobishaniwa cha Sh2.66 trilioni na Dola za Kimarekani 201,242.51 yamesikilizwa.

Aidha, Dk Mwigulu amesema Baraza la Rufani za Kodi (TRAT) lilikuwa na mashauri 176 yenye kiasi cha kodi kinachobishaniwa cha Sh266.94 bilioni ambapo mashauri 91 yenye kiasi cha kodi kinachobishaniwa cha Sh166.32 bilioni yamesikilizwa.

Amesema TRAB na TRAT zinaendelea kutekeleza mpango maalumu yaani “Special Sessions” ambapo kuanzia Novemba, 2023 hadi Juni, 2024 watasikiliza na kumaliza mashauri ya kodi yaliyofunguliwa.

“Kupitia mpango huo, mashauri mengi zaidi yatasikilizwa katika mikoa mbalimbali nchini kwa kuzingatia wingi wa mashauri haya, ikiwemo Dar es Salaam, Arusha, Morogoro, Ruvuma, Tabora, Mara, Manyara, Kilimanjaro, Iringa, Mbeya, Songwe na Njombe,”amesema.

Amesema Serikali pia imeanzisha taasisi ya Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi, “Tax Ombudsman” ambayo jukumu lake kubwa ni kupokea malalamiko na kutatua masuala ya kikodi yanayotokana na huduma, hatua za kikodi na utekelezaji wa sheria za kikodi kati ya mlipakodi dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Amesema zitakuwa fedha za Serikali hadi pale mkono mwingine hadi hapo TRAB ama TRAT itakaposema sasa ni fedha ya serikali lakini ikiwa bado zinabishaniwa serikali inatoa fursa ya haki kutendeka.

Katika swali lake la nyongeza Janejelly amehoji Serikali inawapa muda gani watamaliza mashauri hayo ili fedha hizo zirudi katika mfuko wa serikali zikafanye kazi za maendeleo.

Pia ametaka kufahamu  katika kusuasua na kuchelewa kwa mashauri hayo hawaoni kwamba yanaharibu mahusiano kati ya Serikali na wafanyabiashara ambao ni tegemeo lao la mapato.

Akijibu swali hilo, Dk Mwigulu amesema mashauri hayo kabla hazijaamuliwa haziwi fedha za Serikali na kwamba kubishaniwa kwake  ni kutaka kujenga mahusiano na walipakodi.

Amesema iwapo wangesema kile ambacho Serikali inataka ndio walipe hiyo ingeharibu mahusiano na walipa kodi.

Kuhusu kurakisha mashauri hayo, Dk Mwigulu amesema wameanzisha vikao (session) maalumu ili mambo hayo yasiwe yanakaa sana kwa sababu yanaondoa utulivu katika ufanyaji wa biashara.

Amesema pia uwepo wa ofisi ambayo wafanyabiashara wameitamani siku nyingi ya msuluhishi wa masuala ya kikodi itakwenda kupunguza mashauri hayo.

Amesema hatua hiyo inatokana na masuala ya kodi ambayo hawakuridhiana sasa yataenda kwa mtu mwingine ambaye hayuko mfumo wa kodi.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi