Connect with us

Kitaifa

Ufaulu watema wanafunzi 200 mfuko wa Samia

Dar es Salaam. Wakati wanafunzi 226 wakitemwa katika ufadhili wa masomo wa Samia ‘Samia Scholarship’ kutokana na kushindwa kukidhi vigezo vya kuendelea kupata ufadhili huo, Serikali imewahakikishia kupata mikopo ili waendelee na masomo yao.

Wanafunzi hao ni kati ya 640 walionufaika na ufadhili huo katika mwaka wa kwanza 2022/2023 ulipoanza kutolewa nchini ambapo ufadhili huo ulihusisha ada ya mafunzo, posho ya chakula, malazi, vitabu, mahitaji maalumu ya vitivo, vifaa saidizi kwa wenye mahitaji maalumu na bima ya afya.

Pia wanafunzi 68 wamefanya mitihani ya marudio (supplementary) na wanasubiri kujua hatima yao baada ya matokeo kutoka.

Kupata ufaulu wa chini ya GPA 3.8 ikiwa ni moja ya kigezo cha kuondolewa katika ufadhili huo.

Ufadhili huo uliwalenga wanafunzi waliopata ufaulu wa juu katika masomo ya sayansi kwenye mitihani ya kidato cha sita ambao wataendelea na kozi mbalimbali vyuoni kulingana na machaguo yao.

Akizungumza na Mwananchi jana, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Caroline Nombo alisema kilichofanyika ni kwa mujibu wa kigezo namba 8 na 9 (d) na (e) na tayari utaratibu wa kuwapatia mikopo ya kawaida wanafunzi hao umefanyika na wameshapata ujumbe ufupi kupitia simu zao.

“Wanasubiriwa wajaze fomu, viwango vya mikopo walivyotengewa hawa ni sawa na walichokuwa wakipata katika ufadhili na hadi Novemba 4 mwaka huu, wanafunzi 226 walikuwa wamepata ujumbe mfupi wa maandishi kwa ajili ya mikopo kwenye anuani zao na wengine 68 wanafanya supplementary na hatma yao itajulikana baada ya hapo,” alisema Profesa Nombo.

Kwa mujibu wa mwongozo huo, vigezo vilivyotajwa awali vinavyoweza kukatisha ufadhili huo mbali na kushindwa kufikia ufaulu wa GPA 3.8 ikiwa katika hatua yoyote mnufaika ataamua kuahirisha masomo kwa sababu binafsi isipokua za kiafya, kwa mwaka husika, hadi mwaka unaofuata.

Pia, mnufaika kubadilisha au atajiondoa kwenye programu yake ya masomo aliyopatia ufadhili kwa hiari yake bila idhini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

“Pia mnufaika akifukuzwa kwa tabia/maadili mabaya, kusimamishwa masomo au kushindwa kitaaluma, kubadilisha chuo alichokuwa anasoma bila idhini ya maandishi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia au kuongeza programu nyingine ambayo inaongeza muda wa kuhitimu kwa programu yake ya masomo aliyopewa,” inaeleza sehemu ya mwongozo huo.

Akizungumzia suala hili, Mkurugenzi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (Heslb), Omega Ngole alisema litafunguliwa dirisha maalumu la maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao kwa ajili yao ili kuwapa nafasi ya kuomba mkopo.

Kuhusu hilo, mchambuzi wa elimu, Muhanyi Nkoronko alisema mwanafunzi anaweza kuwa alifanya vizuri shule alikotoka, lakini si sababu kuwa akifika chuo ataendelea kufanya vizuri.

Alisema wakati mwingine ugumu wa fani wanazochagua kusoma huwa tatizo kutokana na kushindwa kuzimudu huku akiongeza kuwa wakati mwingine uzembe wa wanafunzi unaweza kuwa tatizo.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi