Makala
Hizi hapa sababu unyanyasaji wanawake kukithiri
Dar es Salaam. Takribani wanawake watatu kati ya kumi wenye umri wa miaka 15 hadi 49 wamewahi kupitia unyanyasaji wa namna tofauti wakiwa majumbani mwao, ripoti imeeleza.
Taarifa ilitolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kupitia Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Viashiria vya Malaria inabainisha kati ya wanawake hao, mmoja aliwahi kufanyiwa unyanyasaji wa kingono angalau mara moja tangu alipotimiza miaka 15.
Utafiti huo unabainisha “karibu wanawake wanne kati ya 10 ambao waliwahi kuwa na mume au mpenzi, wamekumbana na ukatili wa kimwili, kingono au kihisia kutoka kwa wenza wao wa sasa”.
Kutokana na utafiti huo, Diana Laston, mkazi wa Kimara, Dar es Salaam anasema vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake ni matokeo ya wanaume wengi kukosa huruma kwa wenzi wao.
“Wanaume wengi wanamchukulia mwanamke kama chombo cha starehe, na hiyo husababisha kuwachukulia kawaida na hapo ndipo thamani ya mwanamke inaposhuka,” alisema Diana.
Alisema licha ya vipigo ambavyo wanawake wamekuwa wakivipata kutoka kwa wenzi wao, pia kuna unyanyasaji wa kihisia ambao umekuwa ukisababishwa na udanganyifu wa kimapenzi kutoka kwa wanaume.
Pia Diana alisema wanawake wengi wamekuwa hawaripoti ukatili dhidi yao kwa sababu wengu hawatamani kuachana na wenzi wao, hivyo huamua kunyamaza ili kutetea mahusiano yao.
“Unakuta anapitia ukatili lakini kwa sababu ana watoto na mume ndiye chanzo cha mapato, anaamua kunyamaza kwani anaogopa akiripoti huenda akaachwa na akapata shida kuwalea watoto peke yake,” alisema.
Diana aliongeza kuwa wengi huamua kuvumilia vitendo hivyo ambavyo mwishowe hupelekea ulemavu wa kudumu au vifo kuyokana na vipigo.
Naye Catherine Lyimo wa Mabibo, Dar es Salaam, alisema ili kupunguza ukatili dhidi ya wanawake elimu haina budi kuendelea kutolewa kwa wanawake hususani kuelezwa madhara ambayo yanaweza kutokea, ikiwemo vifo, ulemavu wa kudumu, msongo wa mawazo na magonjwa.
“Ni muhimu wanawake wajitafutie vitu vya kufanya, waache kuwategemea wanaume kiuchumi, itasaidia hata wanaume kuwapa heshima na thamani,” alisema.
Catherine aliongeza kuwa elimu ya ukatili iwekewe msisitizo kwa watoto shuleni ili kuwajengea uelewa kuhusu ukatili, hali ambayo itasaidia kuwa na kizazi ambacho kitaweza kupinga ukatili na hatimaye kuondoa ukatili katika jamii.
Takwimu zaidi
Licha ya matukio hayo kuwa tishio, inaelezwa kuwa vitendo vya ukatili wa kimwili, kingono au kihisia miongoni mwa wanawake waishio na wenza umepungua kutoka asilimia 50 mwaka 2015 hadi 39 mwaka jana.
Vilevile mwanamke mmoja kati watatu waishio na wenza wamepitia ukatili wa kimwili, kingono au kihisia ndani ya kipindi cha miezi 12 iliyopita.
Aidha, wanawake wanne kati ya 10 wamepata majeraha kutokana na unyanyasaji wa kingono na kimwili kutoka kwa wenza wao.
Pia ripoti hiyo imebainisha takriban nusu ya wanawake ambao wamewahi kufanyiwa ukatili wa kimwili au kingono hawajawahi kuripoti taarifa hizo au kutafutwa kutoa taarifa hizo.
Mikoa ambayo wanawake wamepitia zaidi unyanyasaji kuanzia umri wa miaka 15 ni pamoja na Arusha 45 na Mara 49 iliyopo Kandaya Ziwa iyoongoza ikiwa na asilimia 33.
Mikoa ya Kusini Pemba na Kaskazini Unguja ni ya mwisho ikitajwa kwa asilimia 5 na asilimia 6 mtawalia. Kwa ujumla, Zanzibar ni ya mwisho mwisho ikiwa na ukatili kwa asilimia 8.
Sababu, suluhu ya tatizo
Mtaalamu wa saikolojia, Neema Mwankina anasema mfumo dume bado upo na ndio sababu vitendo hivyo vimeendelea kuwepo na watu bado wanaishi katika mila na desturi, jambo lingine ambalo limesababisha vitendo hivyo kuendelea majumbani.
Akiongelea suala la wanawake kutoripoti visa vya unyanyasaji dhidi yao, Mwankina alisema uelewa mdogo ni changamoto inayosababisha wengi kushindwa kutoa taarifa hizo katika mamlaka husika.
“Wengi huwaza kwamba akimpeleka mume wake au mtu wake wa karibu kwenye vyombo vya sheria, jamii na ndugu yake watamuonaje, kwa hiyo bado kuna mawazo ya namna hiyo katika jamii zetu,” alisema.
Akitolea mfano jamii za Kimasai, alisema katika jamii hizo wanawake hawaruhusiwi kwenda kushtaki popote, pale wanapokutana na unyanyasaji wa aina yoyote isipokuwa kwenye mabaraza maalumu ya wazee wa jamii hiyo.
“Mifumo ya namna hiyo ni rahisi kuchangia kushindikana usuluhishi wa changamoto wanazopitia majumbani. Ni muhimu kapambana na mifumo kama hiyo,” alisema.
Kwa upande wake John Ambrose, mtaalamu mwingine wa saikolojia, alisema licha ya vitendo hivyo kuonekana kupungua bado, iko haja ya elimu kuendelea kutolewa ili kuvitokomeza kabisa.
“Bado kuna jamii zinaamini kwamba mwanamke kupigwa ni haki yake. Wengine hawajui kuhusu ukatili, hawajui waende wapi kushtaki wanapokutana na ukatili. Elimu ikiendelea kutolewa itasaidia kupunguza zaidi vitendo hivyo,” alisema Ambrose.
Alisema wanawake wakipata ufahamu kuhusu namna ya kuripoti unyanyasaji dhidi yao ikiwemo kwenye madawati ya jinsia, italeta urahisi hususani kwa wale ambao hujihisi aibu kuripoti pale wanakutwa vitendo hivyo.
Ambrose alisema kama kesi za unyanyasaji zitaripotiwa ipasavyo itasaidia kupunguza athari za kisaikolojia ambazo zinaweza kusababishwa na mtu kutoshirikisha watu wengine tatizo lake.