Connect with us

Kitaifa

Tahadhari mpya ya mafuriko Dar

Dar es Salaam. Wakati Bodi ya Bonde la Wami Ruvu ikitoa tahadhari ya mafuriko kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, tayari athari zimeanza kujitokeza.

Tahadhari hiyo ilitolewa kwa maeneo ya Gongo la Mboto, Ulongoni, Vingunguti, Tabata Matumbi, Darajani, Jangwani na Miyombo-Kilosa mkoani Morogoro.

Katika taarifa ya bodi hiyo iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, inawajulisha wakazi wa maeneo hayo kuwa kuna uwezekano wa kupata mafuriko kati ya Novemba 2 hadi 9, mwaka huu.

Mkazi wa Kitunda, Robert Mega, akizungumzia athari za mvua alisema juzi alishindwa kwenda kazini kwa sababu barabara zilijaa maji. “Kwa kawaida nafika nyumbani saa moja usiku, lakini Jumatano nilifika saa 4.30 usiku kwa sababu hapakuwa na mabasi. Alhamisi nilishindwa kwenda kazini kwa sababu barabara imejaa maji na mabasi bado hayapiti,” alisema Mega. Alisema barabara nyingi za Kitunda ni za changarawe na zenye mashimo, hivyo daladala nyingi hubadilisha njia.

Dereva wa daladala kati ya Mwanagati na Mnazi Mmoja, Aboubakar Athuman, alisema mvua kubwa iliyonyesha Jumanne na Jumatano iliathiri biashara.

Mudhihir Ismail, mkazi wa Gongo la Mboto, alisema wanakabiliwa na changamoto ya usafiri kutokana na mvua pamoja na ujenzi unaoendelea wa barabara ya mabasi yaendayo haraka (BRT).

“Tunakaa vituoni zaidi ya saa nne kwa kukosekana usafiri, magari yanakwama kwenye foleni, hivyo wengine wameshindwa kuvumilia wanarudi nyumbani na kusitisha kwenda kwenye shughuli zao za kila siku,” alisema.

Alisema kuna baadhi waliamua kupanda treni, ijapokuwa nayo ilijaa na abiria wengine kuning’inia, kitendo ambacho ni cha hatari kwa usalama wao.

Katika kuchukua tahadhari, eneo la Jangwani kuanzia juzi usiku hadi jana kulifanyika usafi kwa kuondoa takataka zilizokwama kwenye daraja la mto Msimbazi.

Mtumishi wa jiji la Dar es Salaam, aliyekuwa akisimamia kazi ya kuondoa taka eneo hilo aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina gazetini kwa kuwa si msemaji alisema juzi usiku Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alitembelea eneo hilo.

Alisema aliagiza watendaji wote kuondoka ofisini na kwenda kutembelea maeneo hatarishi katika kipindi hiki cha mvua.

“Jana kuna picha ilikuwa inasambaa mtandaoni ikionyesha uchafu kwenye mto huu, usiku mkuu wa mkoa alitutaka tuje hapa kusafisha eneo hili,” alisema.

Juzi gazeti hili liliripoti taarifa ya madhara ya mvua katika eneo la Jangwani ambako kulifurika maji.

Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Dar es Salaam, Elisony Mweladzi alisema kazi ya kusafisha maeneo ya mito itafanyika jiji zima na kwamba kuna timu inaendelea na kazi hiyo. Usafishaji wa mito umewapa matumaini wakazi wa bonde la Mkwajuni, ambao walisema maji hayatuami kwa muda mrefu tofauti na miaka mingine.

Neema Clementino, mkazi wa Bonde la Mkwajuni, alisema mvua zinaponyesha wanaishi kwa wasiwasi, lakini kwa kipindi hiki imekuwa ntofauti.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi