Kitaifa
Mapya bungeni, ataka wasilipwe posho, mshahara
Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum, Kunti Majala amependekeza kwa Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kuwa wabunge wasilipwe posho za vikao na mishahara ya mwezi huu ili waonje uchungu wanaokutana nao Watanzania ambao hawajalipwa mafao yao ya kustaafu.
Wameyasema hayo leo Jumamosi Novemba 4, 2023 wakati wakichangia taarifa za kamati za Bunge za kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka ulioishia Juni 30, 2022.
Taarifa hizo ni za Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC).
Amesema watumishi wanadai Sh119 bilioni na kwamba anajiuliza kama kuna mbunge anayedai Serikali hata Sh100.
Amesema watumishi wanadai malipo ya muda mrefu huku akitoa mfano wa Halmashauri ya Chemba ambayo ina watumishi 79 wanaodai tangu wako katika halmashauri ya Kondoa.
“Kama sio kikao hiki basi kikao kijacho na sisi usitulipe mwezi huu, usitulipe mshahara na posho za bunge lijalo…usitulipe ili tuonje uchungu huu ambao wanakumbana nao Watanzania wenzetu waliolitumikia Taifa hili, pamoja na wazee wastaafu ambao wamelitumikia Taifa hili,” amesema.
Ameitaka Serikali kuwalipa watumishi wastaafu wanaodai malipo yao.
Hoja ya mbunge huyo ilimfanya Spika kuwahoji wabunge kama wanaafikiana na kile kilichopendekezwa, hata hivyo ilisikika minong’ono ya chini na ndipo Dk Tulia akasema kuwa ni mbunge mmoja aliunga mkono kwa hivyo ni wachache.
Naye Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Kilumbe Ng’enda alimpa taarifa Kunti kuwa jukumu la kuwalipa wafanyakazi wasiolipwa, lipo mikononi mwa Serikali hivyo akapendekeza kuwa mawaziri ndiyo wanaotakiwa kuzuiliwa ni mishahara yao.
Akiendelea kuchangia, Kunti amesema amefanya hivyo kwa sababu alitaka kuona ni kwa namna gani mawaziri wanaweza kunyoosha mkono kwa makosa yao ya kushindwa kuwasimamia watendaji wao.
“Umeona uzalendo wa mawaziri wetu, kosa wamefanya wao la kushindwa kuwasimamia watumishi wao, wanashindwa kunyoosha mkono kwa makosa ambayo wameshindwa kuwasimamia watu wao,” amesema.
Amewataka kutimiza majukumu yao na kwamba mawaziri wana magari ya kutembelea lakini watumishi wanatembea kwa miguu.