Makala

Bima kwa wote ilivyopita kwenye tanuru la moto

Dodoma. Licha ya kupitishwa na Bunge, Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote wa mwaka 2022 umepita katika tanuri la moto kutokana na baadhi ya wabunge na Spika wa Bunge hilo, Dk Tulia Ackson kuonyesha shaka kwenye baadhi ya vifungu vya muswada huo.

Wasiwasi wao ulijikita zaidi kwenye vifungu viwili, kwenye vyanzo vya fedha za kugharimia mfuko huo ambavyo havikueleza asilimia ya kiwango kitakachotolewa kwa ajili ya wanufaika wasio na uwezo na kingine cha wanufaika, ambacho hakielezi jinsi watakavyohudumiwa.

Kutokana na hofu hizo, Spika Tulia aliiagiza Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi kwenda kutazama upya muswada huo na ikibidi warudi na majibu katika mkutano wa Bunge unaofuata Januari mwakani.

Muswada huo uliwasilishwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kisha kujadiliwa na kupitishwa na Bunge juzi, huku ukiainisha pamoja na mambo mengine, vyanzo mbalimbali vya mapato vitakavyogharamia watu wasiojiweza.

Vyanzo hivyo ambavyo vilisababisha muswada huo uondolewe bungeni mara mbili ni mapato yatokanayo na vipodozi, vinywaji vikali, michezo ya kubahatisha, vinywaji vyenye kaboni, mapato yatokanayo na ushuru wa miamala ya kielektroniki, fedha zitokanazo na Bunge, mapato yatokanayo na uwekezaji wa mfuko, zawadi na misaada kutoka kwa wadau.

Katika muswada huo yamewasilishwa marekebisho kadhaa, tofauti na ulivyokuwa Novemba mwaka jana na Februari mwaka huu ulipoondolewa na Serikali bungeni.

Moja ya marekebisho hayo ni kuondoa sharti kwamba Mtanzania yeyote asingepata huduma za namna nyingine kama leseni ya udereva, vitambulisho vya Taifa na vitu muhimu kama hatakuwa amesajili na mfuko wowote wa Bima ya Afya.

Juzi, Bunge lilipokaa kama kamati kwa ajili ya kupitisha muswada huo, Spika Tulia alieleza shaka na kutaka ufafanuzi kwenye kifungu cha ugharimiaji, akitaka kiwekwe vizuri kwenye sheria, la sivyo kitakuwa na mkanganyiko.

Hofu ya Spika ilizua mjadala mrefu uliosababisha mawaziri watatu, Dk Mwigulu Nchemba (Fedha), Jenista Mhagama (Ofisi ya Waziri Mkuu) na Ummy Mwalimu (Afya) na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Patrobas Katambi kusimama kila mmoja zaidi ya mara mbili kutoa ufafanuzi.

Pia, wabunge watatu kutoka kwenye kamati husika walitoa ufafanuzi ambao hata hivyo, haukumshibisha Dk Tulia, ambaye pia ni mbunge wa Mbeya Mjini, aliyesema “bado haijakaa sawa kisheria.”

“Huwezi kukubaliana kwamba ‘watakuwa wanatenga fedha’ lakini hujui ni asilimia ngapi, kuna wakati tutakuta zimetengwa asilimia 0.0009, je, tunaweza kuwahudumia wananchi wetu kwa namna hiyo kweli,” alihoji Spika Tulia.

“Bunge kazi yetu ni kutunga sheria, kwa hiyo hatupangiwi ni lini tutunge sheria, leo tutapitisha lakini tuwape kazi kamati yetu, wakalitazame kwa undani, nadhani mwezi Januari mwakani mtakuwa mmelitazama,” aliagiza.

Kabla ya agizo hilo, Waziri Ummy alimwomba Dk Tulia kutokuwa na wasiwasi kwa kuwa Wizara ya Fedha iliwahakikishia “hakuna kitakachokwama kwenye uchangiaji huo”.

Alisema licha ya kutokuwekwa asilimia, bado wana imani na Serikali kwa juhudi zilizowekwa na Waziri wa Fedha, kwa kuwa vyanzo vilivyotajwa vimekuwa na uhakika wa kuipatia fedha wizara, ndiyo maana hawana shaka navyo.

Kutokana na kauli hiyo, Spika Tulia alimhoji Waziri Ummy kwamba yeye (Ummy) akiwa mwanasheria, ni kwa namna gani amejiridhisha kutunga sheria ambayo mbeleni inaweza kuwa na ukakasi.”

Hata kabla hajajibu hilo, alisimama Waziri wa Fedha, Nchemba akiwataka wabunge kutokuwa na wasiwasi “kwa kuwa hakuna kitakachoharibika, kwani Serikali itafanya mapitio kila mwaka kuangalia uhitaji”.

Hata hivyo, Waziri wa Fedha alibainisha kuwa kiasi kinachotoka kwenye vyanzo vilivyotajwa kwenye sheria hiyo ni sehemu ya makusanyo hayo, si fedha zote.

 Ndipo akaomba apewe muda kwenda kuliweka vizuri jambo hilo, “hata kama hakutakuwa na asilimia.”

Alisema fedha zote ni mali ya Serikali na Serikali ndiyo yenye wananchi, kwa hiyo kupanga ni kuchagua na utakapofika wakati wa kufanya hivyo wataona nini kianze na kwa kiasi gani.

Awali, Katambi alimwomba Spika Tulia aruhusu muswada huo kupita kwa kuwa upungufu uliojitokeza ungerekebishwa kwenye kanuni.

Katambi, ambaye pia kitaaluma ni mwanasheria, alikiri sheria kwa jinsi ilivyo katika kifungu hicho ina upungufu, hivyo akaomba ikubaliwe waingize marekebisho kwenye kanuni.

Katika suala hilo, Waziri Mhagama alisema Serikali imepokea vifungu hivyo na inakwenda kuvifanyia kazi ili kuweka sawa jambo hilo, ikiwemo kueleza kutakuwa na mabadiliko kabla ya kuanza kwa mwaka mpya wa fedha.

Mbali na mjadala huo, juzi, Mwenyekiti wa Kamati ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Stanslaus Nyongo alisema kifungu hicho pia kiliwapa wakati mgumu wakati wa kuchambua muswada huo kwenye kamati na ilikuwa moja ya sababu za kuuondoa muswada huo bungeni.

Nyongo alisema ndani ya kamati walihoji namna gani fedha hizo zingepatikana bila kuwa na uwiano wa asilimia kutoka kwenye vyanzo hivyo, lakini Serikali iliwatoa shaka kwamba itakuwa ikifanya mapitio kila mwaka wa fedha unapoanza.

Kwenye kifungu cha usimamizi wa wanufaika, nako Spika Tulia alisema hakujakaa vizuri kwa kuwa kifungu hakielezi namna gani watapatikana na jinsi ya kuwahudumia, kwani sheria haielezi kwa mawanda mapana, kitendo kinachoweza kuleta mkanganyiko mbele ya safari.

Kiongozi huyo wa Bunge ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alisema hatua ilipofikia muswada usingerudishwa nyuma lakini Bunge lisichoke kutunga sheria kwa kuwa haijaandikwa mahali popote kuhusu muda kamili wa kutunga sheria.

Mengi hayako wazi

Kauli ya Spika Tulia iliungwa mkono na Msemaji wa ACT-Wazalendo katika Wizara ya Fedha, Dk Elizabeth Sanga alipozungumza na gazeti hili jana, akisema mambo mengi hayako wazi kwenye sheria hiyo kama walivyotarajia.

Dk Sanga alisema muswada huo ni mzuri kwa ajili ya Watanzania, lakini ulivyowekwa ni sawa na kusema tatizo halijatatuliwa, hivyo kuna haja ya kuuangalia upya.

Alisema kuendelea kuweka afya za Watanzania katika vyanzo ambavyo makusanyo yake yana shaka, ni sawa na kuweka rehani afya zao na kuongeza tatizo juu ya lingine.

“Sisi (ACT Wazalendo) tulishasema mpango wa bima ya afya utakuwa na maana ikiwa tutaainisha ukusanyaji wetu iwe kama mifuko ya hifadhi ya jamii,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk Sanga, moja ya maeneo ambayo yanaweza kutoa vyanzo vizuri vya mapato ya mifuko ya bima ni kwenye fedha za mikopo ya asilimia 10 katika halmashauri, ambayo itawekewa utaratibu mzuri wa kila mmoja si tu kuishia kwenye mikopo, bali itawajengea uwezo wa kuwa kwenye pensheni.

Unaweza kukwama

Nje ya Bunge, mchambuzi katika masuala ya uchumi, Donald Mmari alikubaliana na hoja za Serikali, huku akihadharisha kuwa kama hakutakuwa na umakini katika baadhi ya maeneo, ikiwemo kufanya mapitio kila mwaka, huenda mfuko huo ukakwamba mapema.

Mmari aliungana na Spika na wabunge, akisema bila kuweka asilimia kutoka kwenye chanzo chochote, kunaweza kuwa sehemu ya kukosa mapato hayo kwa wakati, hasa pale zinapohitajika fedha za kutosha kuwahudumia wananchi wasio na uwezo.

Mchumi huyo alisema hana shaka kwa namna yoyote kuhusu kutengwa kwa vyanzo hivyo, kwani waliopitia wizarani kuna vitu vingi walivyojiridhisha navyo, hivyo asingebeza licha ya kusisitiza kuwa utengaji wa asilimia lingekuwa jambo la maana zaidi.

“Tuanze na kilichopo ndipo mambo mengine tutaendelea kurekebisha kadiri tunavyokwenda mbele. Hapa wizara itakuwa na jukumu la kufanya marekebisho ya maboresho kila mwaka ili wasiyumbe.

Alipoulizwa ni vyanzo gani angependekeza vitasaidia, alisema mfuko huo ungepelekwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambako kungewekwa sehemu ya asilimia za makusanyo na kuwekwa kwenye mfuko huo.

Wakati maoni hayo yakitolewa, mtaalamu mmoja wa uchumi katika Ofisi ya Rais (Tamisemi)ambaye aliomba jina lake lisiandikwe, alisema uamuzi wa Serikali kuchukua kwenye vyanzo vilivyotajwa ni sahihi, lakini unaweza kupeleka malalamiko ndani ya Wizara ya Afya, kwa kuwa havitakuwa endelevu kama inavyotarajiwa.

Mtumishi huyo alisema Serikali ingeweka malengo ya kuwa na kiasi kamili kwenye utekelezaji, ambacho kitaangalia mahitaji, lakini kutamka kwenye sheria bado kutakuwa na mkanganyiko, tena mkubwa.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi