Kitaifa
Serikali kuwarejesha vijijini watumishi waliohama bila utaratibu
Dodoma. Serikali imesema watumishi waliohama kabla miaka mitatu tangu kuajiriwa kwao, watarejeshwa katika maeneo vijijini waliyopangiwa wakati wakipewa ajira.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Novemba 2, 2023 na Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange wakati akijibu maswali ya nyongezeka yaliyoulizwa na Mbunge wa Mpanda Vijijini (CCM) Moshi Kakoso.
Kakoso amesema walimu wamekuwa wakijitolea lakini ajira zinapotoka hawapati nafasi wanaojitolea.
Amesema katika halmashauri yake ina walimu zaidi ya 60 wanaojitolea lakini zilivyotoka nafasi za ajira wamepata walimu watatu.
“Je Serikali haioni kuwa inavunja moyo walimu wanaojitolea na wanaopata ajira ni wale ambao wako mitaani tupate mwongozo na majibu stahiki kwa wale ambao wanajitolea,”amesema.
Aidha, Kakoso amesema kuna tabia iliojengeka katika halmashauri za pembezoni ambapo wanapokea waajiriwa lakini ndani ya miezi mitatu wote wanarejea mijini.
Amehoji kama Serikali haioni tabia hiyo itakuja kuuwa mfumo wa walimu na watumishi katika maeneo ya vijijini.
Akijibu maswali hayo, Dk Dugange amesema Serikali imeendelea kuajiri watumishi wote bila kujali kama wanajitolea ama hawajitolei.
Amesema changamoto ya kuajiri walimu wanaojitolea ilitokana na utaratibu usioeleweka wa kuwasilisha majina ya walimu wanaojitolea.
“Baadhi ya wakuu wa shule wasiowaaminifu walikuwa wanatumia fursa hiyo kuingiza majina ya walimu ambao hawajitolei na mara nyingine kuwaacha wale wanaojitolea,”amesema.
Amesema kwa kutambua hilo ndio maana Serikali imeandaa mwongozo mahususi na mfumo ambapo walimu wataingia wenyewe na kujiorodhesha kwamba ni walimu wanaojitolea katika shule fulani.
Amesema Serikali itafanya uhakiki kuthibitisha kama kweli wanajitolea kwenye maeneo hayo na hivyo kusaidia ajira zinavyotokea kuona ni nani amejitolea kwa muda mrefu ili apewe kipaumbele cha kupata ajira hizo.
Amesema kazi hiyo inafanyika na Serikali watahakikisha kuwa inakamilika mapema iwezekanavyo.
Kuhusu walimu wanaohama, Dk Dugange amesema wameshatoa maelekezo kwa watumishi wa afya na elimu kutohama ndani ya miaka mitatu tangu kuajiriwa, isipokuwa kama kuna sababu ya msingi ikitokea.
“Waheshimiwa wabunge yale maeneo ya vijijini ambayo watumishi wameajiriwa kabla ya muda huo tupate majina hayo tumeshapa Ludewa, tumeanza kushughulikia na watarejeshwa kwenye halmashauri zile zile kutoa huduma kwa wananchi,”amesema.
Awali katika swali la msingi Kakoso amehoji Serikali ina mkakati gani wa kuwapa ajira walimu wanaojitolea katika shule za msingi na sekondari pindi ajira zinapotoka badala ya kuwaacha.
Akijibu swali hilo, Dk Dugange amesema
Ofisi ya Rais Tamisemi kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeandaa mwongozo wa kuwatambua walimu wanaojitolea katika shule zote nchini.
“Mwongozo huo umeipa Ofisi ya Rais –Tamisemi jukumu la kuandaa mfumo wa walimu wanaojitolea. Kwa sasa mfumo huo unaendelea kuandaliwa, utakapokamilika walimu watajulishwa ili waanze kufuata utaratibu wa kujisajili katika mfumo huo ili kurahisisha utambuzi wao,”amesema.
Akizungumza baada ya Serikali kujibu maswali hayo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema Serikali imeahidi mara kadhaa wakati wakijibu maswali ya wabunge bungeni.
“Mjipangie muda gani ili ajira zinapoanza kutangazwa basi tufahamu kuwa ni ndani ya mwaka ama miaka mitatu utakamilika (mwongozo) kwa sababu swali hili linajirudia kila mara ili wale wanaojitolea wasikatishwe tamaa kuendelea kujitolea,”amesema.