Connect with us

Kitaifa

Muswada bima ya afya kwa wote watua bungeni

Dodoma. Hatimaye Serikali imeweka wazi vyanzo vya mapato katika safari ya kutunga sheria ya Muswada wa sheria namba 8 ya Bima ya Afya kwa Wote ambavyo ni kodi za vipodozi, kodi ya vyombo vya moto na vinywaji vikali.

Vyanzo hivyo vimetajwa leo Jumatato Novemba 01, 2023 bungeni na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati akiwasilisha muswada huo bungeni.

Muswada huo ambao ulikwama kuwasilishwa mwaka jana 2022 kwa kilichoelezwa ni kukosekana kwa vyanzo halisi vya kugharamia matibabu ambapo kulikuwa na mvutano baina ya Serikali na Kamati ya Bunge.

Leo Waziri amesema Serikali kupitia Wizara ya Fedha imeridhia na kutoa fedha zitokanazo na vyanzo hivyo kwa ajili ya kusaidia gharama hizo.

Hata hivyo, vyanzo hivyo vya mapato siyo kitu kipya kwa ukusanyaji wa mapato kwani vilikuwepo tangu mwanzo licha ya kuwa fedha zake huelekezwa katika matumizi mengine.

“Tunamshukuru Waziri wa Fedha kwa kuridhia vyanzo vya mapato ambavyo vitasaidia kwenye mfuko huu ambavyo ni sehemu ya ushuru wa vinywaji, vipodozi na ushuru wa vyombo vya maoto hivyo kuwa na uhakika wa upatikanaji wa fedha,” amesema Ummy.

Kwa mujibu wa Waziri, kutungwa kwa sheria hiyo na utekelezaji wake kunakwenda kuondoa malalamiko ya misamaha kwa watu wasiojiweza ambayo amekiri kuwa licha ya kuwepo lakini hakuna uhalisia kwenye vituo vya kutolea huduma za tiba.

Waziri amesema jumla ya Watanzania 15.8 milioni sawa na kaya zaidi ya 3.6 milioni wanakwenda kunufaika na muswada huu jambo litakalosaidia pia kuondoa malalamiko na kelele za kuzuiwa kwa maiti katika hospitali kutokana na kudaiwa kwa gharama za matibabu.

Katika hatua nyingine Waziri ametaja sababu za kuzuia kwa Bima ya Watoto kwamba kulitokana na uchunguzi kubaini kuwa asilimia 99 ya watoto waliokuwa wanajiunga kwenye Bima ya Afya Toto walikuwa ni wagonjwa tayari.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi