Kitaifa

Serikali yaomba Bunge kupitisha mkataba, yatilia shaka

Dodoma. Serikali imeliomba Bunge kuridhia azimio la mkataba wa kuanzisha Taasisi ya Dawa ya Afrika la mwaka 2023 huku ikatilia shaka vipengele vitatu katika ibara ya sita.

 Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amewasilisha azimio hilo bungeni leo Jumanne Oktoba 31, 2023  na kuvitaja vipengele  6 (i), 6(m) na 6(o) kwamba vikiridhiwa vinaweza kuwa na tatizo kwa nchi.

Hata hivyo, Kamati ya Bunge imeomba ibara ya 26 na 26(4) zifanyiwe marekebisho kwa kuwa zikiachwa kama zilivyo zitakuwa na shida.

Ummy amesema ukiondoa vipengele hivyo, mkataba huo ni muhimu na una faida na masilahi ya nchi kwa kuwa katika mkutano wa kawaida uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia Februari 11 2019, walikubaliana kuanzishwa kwa Taasisi ya Dawa ya Afrika na tayari nchi zingine zimeanza kunufaika.

Amesema mkataba huo unalenga kuratibu na kusaidia nchi wanachama wa Umoja wa Afrika katika kuboresha uwezo wa kudhibiti ubora wa bidhaa tiba, suala ambalo ni changamoto kwa nchi nyingi barani Afrika.

“Kwa kuwa hadi kufikia Julai 31,2023, nchi 30 (ikiwamo Tanzania) kati ya nchi wanachama  55 wa Umoja wa Afrika zilikuwa zimesaini mkataba huo, nchi 23 kati ya 30 zilizosaini zilikuwa zimeridhia zikiwamo  Rwanda na Uganda kwa ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni muda sasa Tanzania kuridhia ili iwe sehemu ya wanufaika,” amesema Ummy.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya na Ukimwi Stanslaus Nyongo amesema mkabata huo kama utaboreshwa vipengele vichache, ni muhimu kwa masilahi ya nchi.

Hata hivyo, Nyongo ameliambia Bunge kuwa, pamoja na umuhimu na faida za mkataba huo, lakini hakuna mtu aliyefika mbele ya kamati hiyo kwa ajili ya kutoa ushauri na maoni.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi