Kitaifa
Hatimaye CHADEMA wakubali kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025
Mara kadhaa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekuwa
kikigomea chaguzi kwa sababu ya kila wanachoeleza kuwa ni kutoridhishwa na
namna chaguzi zinavyoendeshwa nchini. Kutokana na kutoridhika huko, CHADEMA
wamekuwa wakishinikiza mabadiliko ya sheria za uchaguzi na hata Katiba. Mfano,
Chadema iligomea kabisa uchaguzi mdogo uliofanywa Desemba 17, 2022 na chama
hicho kutoa tamko kwamba, kitagomea pia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na
Uchaguzi Mkuu 2025 kama hakutakuwa na mabadiliko ya katiba.
Hata hivyo, Oktoba 30 mwaka huu chama hicho kimetengua uamuzi wake huo wa
kugomea Uchaguzi sasa kimesema kimesema kitashiriki chaguzi zote mbili,
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 pamoja na Uchaguzi Mkuu 2025.
Kupitia Katibu Mkuu wake, John Mnyika na kurasa zake za mitandao ya kijamii
amewataka wanachama wa Chadema na Watanzania kwa ujumla kuelekeza nguvu
zao kuitaka serikali iwasilishe miswada miwili muhimu bungeni wakati Mkutano wa
Bunge la 14 unaoanza tarehe Oktoba 31, 2023 jijini Dodoma ili kuwa na chaguzi
bora zaidi.
Katika Mkutano wa 14 wa Bunge utakaoanza Oktoba 31, 2023, Serikali itapeleka
miswada miwili inayohusiana na masuala ya uchaguzi.
a. Muswada wa Sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali (Na.4) wa mwaka
2023 [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2023]
b. Muswada wa Sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali za sekta ya sheria
wa mwaka 2023 [The Legal Sector Laws (Miscellaneous Amendments) Bill,
2023]
Wachambuzi wa masuala ya siasa ndani na nje ya Tanzania wanaona kauli hii ya
CHADEMA kama kukosa msimamo na mbinu mbadala kwani wanafahamu kuwa
Bunge linalokwenda kujadili na kupitisha sheria hizo wanazotarajia kuwaokoa ni
Bunge ambalo karibu asilimia 100 ni la CCM. Kutokana na ukweli huu, CCM
inatarajiwa kuendelea kushinda kwa kiasi kikubwa katika Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa mwakani, na Uchaguzi Mkuu 2025.