Kitaifa
Bashe agoma korosho ya Nagurukuru kuuzwa bei ya chini
Lindi. Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, ameitata Bodo ya Korosho nchini (TCB), kujiridhisha juu ya ubora wa korosho zilizopo katika ghala la Nangurukuru, ambazo ziko chini ya Chama Kikuu cha Ushirika Lindi Mwambao, kutokana na wanunuzi kuzipa bei ya chini wakidai zina ubora wa chini.
Waziri Bashe ametoa agizo hilo jana jumapili Oktoba 29, 2023; baada ya wanunuzi, kutaka kununua korosho hizo kwa Sh1, 705 kwa kilo, jambo ambalo halikumridhisha wazir huyo, na hivyo kumuahgiza Mkurugenzi wa TCB, Francis Alfred kujiridhisha juu ya ubora wake.
Maagizo ya Waziri Bashe ni kuona korosho zilizohifadhiwa kwenye ghala hiyo haziuzi kwa Sh1705 kwa kilo kama ambavyo imependekezwa na wanunuzi na badala yake anataka kuona bei ya chini ikiwa ni Sh1, 900 kwa kilo.
“…nimesikiliza bei zote, lakini bei ya Sh1, 705 kwa ghala la Nangurukuru sikubaliani nayo hata kidogo. Nataka kuona bei ya mwisho ya korosho kwa ghala la Nangurukuru kuwa ni Sh1, 900 kwa kilo, nimemuagiza, Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho kuhakikisha anakwenda kwenye ghala la Nangurukuru kuangalia ubora wa korosho zilizopo,” amesema Bashe
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa bodi ya korosho Tanzania, Francis Alfred amesema kuwa korosho za Tanzania huuzwa nje ya nchi na kwamba wakulima wanasitizwa kila wakati kuzingatia ubora.
Alfred ameendela kusema kuwa agizo la Waziri amelipokea na atakwenda kuziangalia korosho zilizopo kwenye ghala hilo, huku akibainisha kuwa juma lijalo baadhi ya vyama vya ushirika vya msingi (Amcos), vitafungwa kutokana na kukaidi maagizo waliyopewa na bodi.
“Kuna baadhi za Amcos hawatekelezi maagizo tuliyowapa ya kuzingatia ubora, ninachokifanya kwa kuwa wamekaidi maagizo, hizo Amcos nitakwenda kuzifunga, kwa sababu tumeshwaeleza kuhusu ubora, lakini naona wanakaidi,” amesema Alfred na kuongeza;
“Waziri ameniagiza kwenda kuangalia korosho kwenye ghala la Nangurukuru kwa sababu, kuna mashaka ya kwamba korosho zilizopo pale yawezekana hazina ubora ndio mana bei imeshuka hadi 1705 kwa kilo, jambo ambalo Waziri amelikataa.”
Aidha Mkurugenzi huyo amewasihi wakulima kwa kuwaambia: “Niwaombe wakulima wajitahidi kuzingatia ubora, korosho zikiwa na ubora lazima bei itakuwa nzuri, mnada wa kwanza tuliuza korosho Sh.2000 bei ya juu mnada waleo korosho Sh2750 bei ya juu, korosho ikiwa na ubora inapanda kila mnada.”
Aidha Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Lindi Mwambao, Nurdin Swallaa amesema kuwa jumla ya Tani 4000, zimeuzwa kwenye mnada w apili na bei ya juu ikiwa Sh2750 na bei ya chini ikiwa Sh1900.
Somoe Shabani, mkulima wa Kijiji cha Nyangao, ameishukuru Serikali kwa kuwekea mfumo wa stakabadhi ghalani ambao unawanufaisha, na kwamba katika minada yote miwili, bei zinapanda japo amewaomba wanunuzi kujitahidi kuongeza bei.
“Bei zinazopatikana kwenye mnada sio mbaya, ila wanunuzi kwa kushirikiana na Serikali wajitahidi korosho isiuzwe kwa bei ya chini ya Sh2000 kwani ikiwa chini ya hapo mkulima hapati chochote kutokana na makato ya Serikali pamoja na gharama za upuliziaji,” amesema Somoe.
Kwa upande wake Zaituni Jumbe amesema kuwa bodi ya korosho kuhakiki ubora ni jambo sahihi, kwa kuwa, korosho inapokuwa na ubora mzuri, hata bei inakuwa nzuri, amewaomba wakulima kujitahidi kuzingatia ubora.
“Niwaombe wakulima wenzangu, tuzingatie ubora, korosho zikiwa na ubora mzuri mnunuzi hawezi kununua korosho kwa bei ndogo, lazima atapandisha bei iliapate mzigo,” amesema Zaituni.